Kiswahili chatambulika kama Lugha rasmi ya Kikazi ndani ya Umoja wa Afrika

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,106
10,173
Muungano wa Afrika (African Union) umeipitisha lugha ya Kiswahili, kuwa lugha rasmi ya kikazi ndani ya Umoja huo. Lugha hiyo huzungumzwa katika nchi kadhaa za Mashariki mwa Afrika pamoja na jamii za Waswahili katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman.

Huu ni uamuzi ambao umekuwa ukitarajiwa kwa miongo kadhaa sasa. Miaka mingi watu wamekuwa wakiuliza kwa nini ni lugha moja tu ya nchi za Kiafrika iliyo lugha rasmi ya Muungano wa Afrika (African Union)?

Inakisiwa kwamba zaidi ya watu milioni 150 barani Afrika wanazungumza Kiarabu, wengi wao wakiwa Afrika ya Kaskazini. Na lugha hiyo ilikuwa pekee miongoni mwa lugha za Afrika iliyotukuzwa hivyo kabla ya Kiswahili nacho kutangazwa hivi majuzi kuwa ni lugha rasmi ya AU.

Idadi hasa ya wanaozungumza Kiswahili haijulikani. Kuna wasemao kwamba ni baina ya watu 50 milioni hadi 150 milioni.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ambaye ndiye aliyewasilisha pendekezo la kutaka Kiswahili iwe lugha rasmi ya AU, amesema kwamba idadi halisi ya wanaozungumza Kiswahili ni ya takriban watu milioni 100 walio ndani na nje ya Afrika.

Dkt. Mpango ndiye aliyeuongoza ujumbe wa nchi yake katika mkutano mkuu wa viongozi wa nchi wanachama wa AU jijini Addis Ababa wiki iliyopita.

BBC Swahili

Idadi aliyoitaja yeye iko chini ya ile iliyotajwa na Shirika la Unesco lililosema kwamba watu wanaozidi milioni 200 wanazungumza Kiswahili.

Mwaka jana Shirika hilo liliitaja tarehe 7 Julai kuwa ni 'Siku ya Kiswahili Duniani"; hivyo, kuanzia mwaka huu wa 2022, kila ifikapo tarehe 7 Julai Kiswahili kitakuwa kinaadhimishwa duniani. Kwa hivyo, lugha hiyo inakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika iliyo na heshima hiyo.
Kujitanua kwa Kiswahili

Pamoja na kuwa Kiswahili ni lugha rasmi ya AU inayotumika katika Muungano huo, Kiswahili pia ni lugha rasmi inayotumika katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Bendera za nchi wanachama wa Afrika Mashariki

Hali kadhalika, Kiswahili kinasomeshwa katika nchi nyingi za Kiafrika na zisizo za Kiafrika. Afrika Kusini na Namibia zimetangaza kuwa kufundisha Kiswahili mashuleni. Na Chuo Kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia, nacho kimesema kina nia ya kuanza kufundisha Kiswahili.
Changamoto zinazoikabili AU

Bado Muungano wa AU unakabiliwa na changamoto nyingi za kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili itaanza kutumika katika muda usio mrefu.

Kwa mfano, linapozungumzwa eneo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Tanzania na, kwa kiwango fulani, Kenya, ndizo zilizo safu ya mbele.

Nchi nyingine katika kundi hilo ziko nyuma katika matumizi yao ya Kiswahili na panahitajika mkakati wa pamoja kukiimarisha kwanza Kiswahili nchini Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini ambako huko Kiswahili hakizungumzwi kabisa.

Sababu kubwa ni kwamba lugha za kienyeji (kikabila) ndizo zenye nguvu na zinazotumika sana katika mawasiliano baina ya watu wao kuliko Kiswahili.

Aidha, wananchi wengi wa nchi hizo hawaoni umuhimu wa kujifunza Kiswahili bila ya sababu maalum.

Lugha inayozungumzwa zaidi katika nchi kama Uganda ni Kiingereza. Hata Comoro ambako lugha za visiwa vyake vinne zinalingana na Kiswahili pana haja ya kukifundisha Kiswahili sanifu ili wananchi wengi wa visiwa hivyo waweze kukielewa.

Pia kumezuka mtindo wa wasomi kuzungumza Kiswahili wakikichanganya na maneno ya Kiingereza. Hili linaonekana kuanzia kwa wanasiasa kwenye mijadala bungeni hadi kwa watu wa kawaida mitaani.

Katika nchi za Rwanda na Burundi Kiswahili kinazungumzwa zaidi na jamii za walio wachache wanaojulikana kama "Waswahili" na wanaoishi katika maeneo yao hasa katika miji mikuu ya Kigali na Bujumbura. Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Kiswahili kinazungumzwa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo tu.
Kiswahili kipi cha kuzungumzwa

Ingawa azimio la AU la kukubali kutumia Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Muungano huo linakaribishwa na kupongezwa kote ambako Kiswahili kinazungumzwa barani humo na nje ya bara hilo, swali linaloulizwa na wengi ni Kiswahili kipi kinachokusudiwa?

Mnamo miaka ya karibuni kumekuwa na mabishano hata miongoni mwa wasomi ni wapi lugha hii inazungumzwa kwa ubora wake.

Pamoja na hayo inakubalika pasi na shaka kwamba chimbuko la Kiswahili fasaha ni maeneo ya Mwambao wa Kenya, Lamu, Mombasa na Zanzibar. Kwa hivyo kuna hoja yenye nguvu kwamba kwa vile Kiswahili kina wenyewe Kiswahili kilicho bora ni kile chenye kuzungumzwa na wenyewe Waswahili popote pale walipo.

Afrika kusini imeidhinisha lugha ya kiswahili kufunzwa shuleni kuanzia 2020

Ninasema hivyo kwasababu lugha hii imetanuka na kutanuka kwake kunakihatarisha kutokana na wale wenye kudhania kwamba wana haki ya kukitumia watakavyo.

Siku hizi Kiswahili kinatumika na kusomeshwa katika vyuo vikuu duniani, vikiwemo vya Ulaya na Marekani na vilevile kimekuwa kikitumiwa na mashirika makubwa vya utangazaji kama Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) , lile la Ujerumani (DW) na Sauti ya Amerika (VOA, kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Pia kuna redio nyingine za kimataifa kama Redio ya Kimataifa la Ufaransa (RFI) na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Kimataifa ya China.
Kuna haja ya Tahadhari

Hata hivyo kuna haja ya kuchukuliwa tahadhari kutokana na kuzorota kwa matumizi bora ya Kiswahili hasa katika vyombo vya habari, redio, televisheni na magazeti. Kwa jicho langu sababu mojawapo ni kukosekana waandishi habari na wahariri wenye kuijua lugha hiyo na mila zake.

Kwa upande mwingine kuilinda lugha hii adhimu kutakuwa na tija tu ikiwa kutakuweko na vyombo vya , kuisimamia.

Haitoshi tu mabaraza ya lugha ya Kiswahili iwe Tanzania au Kenya kusimamiwa na wenye ujuzi wa kitaalamu tu, bali watu wenye mchanganyiko wa utaalamu na kuwa ni lugha yao ya kuzaliwa. Mtindo wa kuondolewa maneno asilia na kuwekwa maneno mengine kwasababu ya utashi wa watu au wa kisiasa tu ni dosari kubwa inayotishia uimara wa lugha ya Kiswahili.
Uganda ilipongezwa kwa kuendeleza Kiswahili Afrika mashariki

Ni vyema kutambua kwamba huwezi kubadili chimbuko la lugha kwa sababu lina maneno ya kigeni.

Kwa hivyo itakuwa jambo la busara kulirudisha Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki lililokuweko miaka mingi iliopita na lililotoa mchango mkubwa kukikuza na kukiendeleza Kiswahili. Kazi si nyepesi. Kuna umuhimu pia wa kukipa nguvu Kiswahili kwa kuwa na waalimu waliohitimu. Kwa sasa kuna upungufu wa waalimu wa aina hiyo.
Pongezi kwa Tanzania

Kwa ujumla jitihada ya Tanzania kupigania lugha ya Kiswahili itumike katika Umoja wa Afrika, ni ya kupongezwa katika safari ya kupigania Afrika kuwa na lugha moja iliyo rasmi bila ya kuzidumaza lugha nyingine.

Inatoa fursa kwa Waswahili waliobobea kwa kuizungumza na kuiandika lugha yao kuweza kupata nafasi za ajira katika taasisi mbali mbali kuanzia AU, Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata Unesco.

Itakuwa ni furaha zaidi ikiwa juhudi hizi zitaendelea na kuona lugha hii inakubaliwa pia kuwa moja ya lugha zitakazotumiwa katika shughuli za Umoja wa Mataifa, kama zilivyo lugha nyingine sita — Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kichina, Kirusi na Kiarabu.
 
Vizur naona sasa hadi Egypt wanasoma kiswahili chuoni
 
Back
Top Bottom