Kisa cha mwanamke wa ziwani – 1

Ashura9

JF-Expert Member
Oct 21, 2012
740
485
Kisa cha mwanamke wa ziwani – 1


  • Aliuawa, mwili ukazamishwa majini kwa miaka 21
  • Ulizamishwa kwa kufungashiwa vitu vizito usiibuke

AGOSTI 12, mwaka 1997, majira ya mchana katika Wilaya ya Lake nchini Uingereza, kundi la wazamiaji kutoka mji mdogo wa Kendal lilikwenda kufanya mazoezi katika mto wa Caniston, ulioko jirani na eneo hilo.
Mmoja wa wazamiaji wale alifanikiwa kwenda kina kirefu zaidi ya mita 21 na ndipo alipohisi harufu kali ya kitu kinachonuka. Alipozidi kusogelea eneo lile aligundua ni mabaki ya mwili wa mwanadamu uliofungwa kwenye mfuko wa plastiki.
Mzamiaji yule pamoja na wenzake ilibidi wasitishe mazoezi yao na kuwafahamisha polisi. Baadaye, mchana huo huo kikosi cha polisi wazamiaji kilifika kwenye eneo la tukio na kufanikiwa kuyatoa mabaki ya mwili ule.

Walipofungua ule mfuko wa plastiki walikuta mabaki ya mwili wa mwanamke ambaye alikuwa akionekana dhahiri kwamba alikuwa na umri wa chini ya miaka 30, na ilionekana dhahiri kwamba alikaa ndani ya maji kwa miaka mingi sana kwani hata mavazi aliyokuwa ameyavaa yalionyesha hivyo.

Alikuwa amevaa vazi la usiku la miaka ya 70 na alionekana kwamba alikuwa amepigwa kwa kitu kizito kichwani na kisha kutupwa mtoni. Ndani ya mfuko wa plastiki uliokuwa umehifadhi mwili huo, kulikutwa pia vipande vizito vya vyuma ambavyo viliwekwa kwa makusudi na muuaji, ili ule mwili uzame moja kwa moja bila kuibuka.

Katika hatua za awali za uchunguzi, askari wa upepelezi walianza kuchunguza kesi zaidi ya 50 za watu walioripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwenye miaka ya 70. Ukweli ni kwamba, hata vazi alilokutwa nalo mtu huyo (marehemu) lilirahisisha sana kutambuliwa kwake. Haikuwachukuwa polisi muda mrefu kutangaza kuhusu kutambuliwa kwa mwili ule ambao ulikwishaharibika vibaya kutokana na kukaa katika maji kwa takribani miaka 21.

Agosti 21, 1997 ikiwa ni siku tisa baada ya kugundulika kwa ule mwili, polisi wa upelelezi walitangaza rasmi kwamba ni mwili wa Carol Park, mama wa watoto watatu ambaye pia ni mwalimu wa shule ya msingi aliyekuwa na miaka 30 wakati huo alipotoweka.
Taarifa za polisi zilionyesha kwamba Carol alitoweka nyumbani kwake Julai, 1976. Inadaiwa kwamba tarehe hiyo, familia yao ilikubaliana wafanye safari kuelekea mji wa Blackpool ili kupunga upepo kwenye hoteli za ufukweni, lakini Carol alisitisha uamuzi wa kwenda huko kwa madai kwamba anajisikia vibaya, hivyo mumewe Gordon Park ambaye pia ni mwalimu, pamoja na watoto wao waliamua kwenda wenyewe.
Lakini waliporudi usiku hawakumkuta Carol, na ilimchukua Gordon Park wiki sita kuripoti kutoweka kwa mkewe polisi.
Alipoulizwa sababu ya kuchelewa kutoa taarifa wakati huo aliwaambia polisi kwamba katika miaka ya karibuni mkewe alikuwa akitoka nje ya ndoa na wanaume tofauti tofauti, na ilikuwa hali ya kawaida kujitokeza kwa tabia ya kutoweka pale nyumbani na kurejea akiwa salama. Kutokana na tabia hiyo, mume huyo alidai kuwa hata maisha yao ya ndoa yalishaanza kuyumba.
Polisi walikuja kugundua baadaye kupitia kwa majirani kwamba maisha ya ndoa kati ya Gordon na mkewe Carol hayakuwa mazuri, yalijaa misukosuko mingi. Majirani waliwaeleza polisi kwamba Carol aliwahi kuwaambia kuwa alikuwa katika mapenzi na wanaume wawili waliokuwa wakiishi katika maeneo tofauti na alikuwa akienda kuishi nao katika vipindi tofauti. Taarifa zaidi zilibainisha kwamba kuna wakati aliwahi kutoweka nyumbani kwa miezi 18.

Pia majirani hao walijenga hisia kwamba huenda Carol alikwepa safari ya kwenda Blackpool akichukulia kama ni nafasi muhimu kwake atakayoitumia ili kutoroka pale nyumbani kwake na kwenda kuanza maisha mapya mahali pengine na mwanaume mwingine. Hata hivyo, kaka yake Carol aitwaye Ivor Price, alidai kwamba ni jambo lisiloingia akilini kuamini kwamba dada yake anaweza kuwatelekeza watoto wake watatu na kwenda kusikojulikana bila mawasiliano nao kwa kipindi chote alichopotea kwani hata kipindi cha nyuma alichowahi kutoweka alikuwa akiwasiliana nao.
Pamoja na maelezo yake, polisi hawakuonekana kuyatilia maanani kwani waliona kwamba hakuna haja sana ya kushughulika na kesi ya mtu ambaye alikuwa na tabia ya kutoweka nyumbani kwake mara kwa mara.

Hata hivyo, polisi hawakuipuuza sana ile kesi kwani waliona ni busara kuichunguza kwa makini zaidi, hasa ikizingatiwa kwamba tukio lenyewe lilitokea zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Ili kuthibitisha hayo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali (Detective Superintendent) aliyejulikana kwa jina la Ian Douglas ambaye aliipachika kesi hiyo jina la “mwanamke wa ziwani”(Lady of the Lake) aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi wanaishughulikia kesi ya Carol kama ya mauaji ya kukusudia kutokana na mazingira ya jinsi mwili ulivyopatikana.
Pia msemaji huyo alitanabaisha kwamba polisi watawahoji ndugu na watu wa karibu wa Carol, akiwamo aliyekuwa mumewe Gordon Park, ambaye alikuwa amekwishastaafu kazi yake ya ualimu, na kwa wakati ule ambao mwili wa Carol umepatikana alikuwa amekwenda likizo nchini Ufaransa, akiwa na mke wake wa tatu aitwaye Jenny.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama kuna uwezekano wa Gordon Park kuchukuliwa kama mtuhumiwa wa mauaji hayo, msemaji huyo alisema kwamba haingekuwa vyema kwa polisi kumtuhumu moja kwa moja Gordon, na hawezi kuwaomba polisi wa nchini Ufaransa wamkamate kwa sababu kuna mambo mengi ya kuangaliwa kabla ya kumtia mbaroni.
Kwa maneno yake mwenyewe Douglas alisema; “Bado tuna jukumu la kuwatafuta na kuwahoji watu waliokuwa wakiishi jirani na familia ya Gordon Park wakati Carol alipotoweka, na pia ndugu wa karibu wa familia husika pamoja na marafiki, ni jambo ambalo linahitaji muda na umakini wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kwamba ni siku nyingi tangu tukio hili lilipotokea, na ikumbukwe kwamba tunazungumzia tukio lililotokea miaka 21 iliyopita, ni vigumu watu kuwa na kumbukumbu za tukio zima.”
Alipoulizwa kama polisi watakwenda kuchunguza nyumba ambayo familia ya Gordon Park ilikuwa ikiishi, msemaji huyo alisema hilo linawezekana kwa sababu teknolojia imepanuka katika miaka ya karibuni na kuna uwezekano wa mtuhumiwa kukamatwa.
Siku mbili baada ya Msemaji wa Polisi, Ian Douglas, kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu mwenendo wa upelelezi wa kesi ya Carol Park, akiwa pamoja na timu ya wataalamu wa kuchunguza mazingira ya eneo la tukio, walikwenda kuchunguza nyumba anayoishi Gordon Park iliyoko eneo la Borrow-in-Furness.

Pia timu hiyo ilikwenda kuchunguza boti ya uvuvi (Yatch) ya Gordon ambayo ilikuwa imeegeshwa kando ya Ziwa Caniston. Timu hiyo iliondoka na vitu kadhaa kwa ajili ya kuvifanyia uchunguzi.
Pamoja na kuondoka na ushahidi huo lakini Douglas alionyesha wasiwasi juu ya mwenendo mzima wa maisha ya Gordon, kwa kuwa tayari Gordon alikwishauza boti yake ya uvuvi ya awali ambayo aliipa jina la “Lady J” muda mfupi tu baada ya Carol kutoweka.
Wakati polisi wakiendelea kumsubiri Gordon arejee kutoka Ufaransa alikokwenda likizo, waliona ni vyema kuwahoji watoto wao watatu, Jeremy aliyekuwa na miaka 27 lakini wakati mama yake anatoweka alikuwa na umri wa miaka sita, mwingine ni Rachel aliyekuwa na miaka 26 na Vanessa aliyekuwa na miaka 29 wakati mwili wa mama yao ulipopatikana.
Katika mahojiano hayo, polisi waligundua kwamba Vanessa hakuwa mtoto wa Gordon wa kuzaa, bali alikuwa ni binti wa dada yake Carol aitwaye Christina ambaye aliuwawa na mwanamume wake, mwaka 1969 ambapo Carol na Gordon waliamua kumuasili na kumfanya binti yao. Hata hivyo, polisi walikanusha kuwapo kwa uhusiano kati ya kesi hizo mbili.

Gordon Park na Carol
Ukweli ni kwamba polisi hawakupata ushahidi wowote wa kumtia Gordon hatiani, kwani wale watoto wote watatu hawakuwa na kumbukumbu za matukio yote yaliyotokea kabla na baada ya mama yao kutoweka. Pia polisi walitaka kutengeneza taarifa ya kumbukumbu (profile) ya maisha ya Gordon Park na familia yake mpaka kufikia mwaka 1976.
Kazi hiyo ilikuwa ngumu kwa sababu watu waliotaka kuwahoji walikuwa aidha wamehamia katika maeneo ya mbali au wamefariki dunia. Hata hivyo, polisi walifanikiwa kumpata mama mmoja aitwaye Mary Robins, aliyekuwa na umri wa miaka 61 ambaye alikuwa akifanya kazi ya uyaya kwenye familia ya Gordon Park. Mama huyo alikiri kuwa anakumbuka vizuri sana siku Carol aliyotoweka.
Akizidi kuwasimulia polisi, mama huyo alisema kwamba, hata yeye binafsi alijenga wasiwasi kuhusu namna Carol alivyotoweka, na alihisi huenda kuna jambo ambalo si la kawaida limemtokea. Kwani pale mtaani kila mtu aliliona tukio la kutoweka kwa Carol kama kitu cha kushangaza, kwa mtu kuwatelekeza watoto wake ghafla kiasi kile na kutokomea kusikojulikana bila mawasiliano kama ilivyokuwa awali.
Mama Robinson aliendelea kuwaeleza polisi kuwa, yeye alidhani labda ameamua kwenda kuanza maisha mapya huko nchi za Ulaya kwa sababu hata hivyo, alikuwa ni mwalimu mzuri hasa katika kufundisha lugha ya Kiingereza.
Agosti 24, mwaka 1996, Gordon Park na mkewe Jenny walirejea Uingereza wakitokea Ufaransa. Baada ya kufika nyumbani kwake katika eneo la Barrow-in-Furness ambapo alishusha mizigo kutoka kwenye gari, akaondoka kuelekea Kituo cha Polisi kujisalimisha, kwani pamoja na kwamba alikuwa nje ya Uingereza lakini alikuwa akifuatilia habari ya kupatikana kwa mabaki ya mwili wa aliyekuwa mkewe kupitia vyombo vya habari na hasa televisheni.
Alipofika alishikiliwa kwa muda na kuhojiwa. Wanafamilia na marafiki pamoja na majirani zake walionyesha kusikitishwa kwao kutokana na tukio la kukamatwa kwa Gordon. Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa marafiki zake, Paul Shaw alisema kwamba alitokea kumfahamu Gordon kwa miaka mingi, na walisoma pamoja. Akizidi kumuelezea, Paul kwa maneno yake mwenyewe alisema; “Ni mtu anayejiheshimu, muungwana, anayeheshimu kila mtu, na katika kipindi alipokuwa mwalimu alikuwa akifanya kazi zake kwa uadilifu mkubwa na asiyependa kumkwaza mtu.
Pamoja na kuzungumziwa vizuri na marafiki na majirani zake lakini kulikuwa na wingu la mashaka lililotanda kwa upande wa familia ya Carol dhidi ya Gordon. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya misa ya kumuombea dada yake, kaka yake na Carol alisema; “Bado nina mashaka dhidi yake lakini, mpaka hapo atakapokamatwa muuaji ndio atakuwa hana hatia.”
Baada ya saa 36 tangu Gordon kukamatwa, Msemaji wa Polisi, akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri nje aliwaambia kwamba Gordon Park amefunguliwa mashitaka ya kuhusika na mauaji ya Carol.
Kwa maneno yake mwenyewe msemaji huyo alisema; “Majira ya saa mbili na nusu usiku, kuna mtu amefunguliwa mashitaka ya kuhusika katika mauaji ya Carol Park, na kwa taarifa yenu mtu huyo atafikishwa katika Mahakama ya Barrow siku inayofuata.”
Baadaye msemaji huyo alibainisha kwamba mtu huyo alikuwa ni Gordon Park. Siku iliyofuata, Gordon alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ambapo alikanusha kuhusika na mauaji hayo.
Kesi hiyo iliahirishwa mpaka wiki iliyofuata ili kuruhusu upelelezi wa kesi husika kukamilika. Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Gordon aitwaye Michael Graham aliiomba Mahakama impe dhamana mteja wake, lakini Mwendesha Mashitaka katika kesi hiyo aliyejulikana kwa jina la Elizabeth Grant, alikataa Gordon kupewa dhamana na alitoa sababu zifuatazo, kwanza alidai kwamba mshitakiwa anaweza kuingilia upelelezi wa kesi hiyo, pili alisema kwamba kuna uwezekano wa Gordon kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na mwisho ni kutokana na usalama wake mwenyewe, mama Grant alisema kwamba kuna uwezekano wa mtu yeyote ambaye ameguswa na kifo cha Carol kujichukulia sheria mkononi na kumdhuru mshitakiwa, hivyo kutokana na kukataliwa dhamana ilibidi aendelee kubaki rumande.
Hata hivyo, wiki mbili baadaye Mwendesha Mashtaka mama Grant alibatilisha uamuzi wake na kuruhusu Gordon kuachiwa kwa dhamana kwa masharti kwamba akakae kwa dada yake aliyekuwa akiishi katika mji wa Manchester, pia asalimishe hati yake ya kusafiria na awe anaripoti polisi kila siku na hakutakiwa kutoka nje ya mji wa Manchester.
Kesi yake iliahirishwa mpaka Januari 1998, ambapo iliwapa polisi fursa ya miezi minne kufanya uchunguzi. Januari 7, 1998 ikiwa imebaki wiki moja ili kesi ya Gordon kusikilizwa, Msemaji wa Polisi aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi wameamua kutoendelea na kesi hiyo, kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi madhubuti wa kumtia mshitakiwa hatiani. Taarifa hiyo ilipokelewa kwa furaha sana na Gordon, na kusema wazi kwamba hana hatia ya kuhusika na mauaji ya Carol.
Akizungumza na waandishi wa habari Gordon, kwa maneno yake mwenyewe alisema; “Kwa jinsi Carol alivyonitendea katika ndoa yetu, watu wanadhani nilihusika na mauji yake, lakini ukweli ni kwamba sikuhusika na mauaji hayo, najua watu wanatilia shaka kutokutiwa kwangu hatiani labda mpaka hapo mhusika wa mauaji hayo atapofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani ndio watu wataamini kwamba sikuhusika na mauaji hayo.”

Hata hivyo, Januari mwaka 2002, polisi walianza upelelezi wa siri kwa kuunda timu ya watu sita wakiongozwa na Detective Chief Inspector, Keith Churchman.
Timu hiyo ilitangaza zawadi ya paundi 5,000 kwa mtu yeyote atakayejitokeza kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa muuaji na pia kituo kimoja cha televisheni nchini humo cha Channel 4, kilionyesha kipindi maalumu (documentary) kuhusu kesi hiyo kilichopewa jina marufu la Lady in the Lake wakiifananisha na jina la kitabu cha riwaya kilichotungwa na mwandishi maarufu wa vitabu vya riwaya, Raymond Chandler, ambapo kilikuwa na jina kama hilo.
Hatua hiyo ilizaa matunda baada ya watu wawili ambao waliwahi kufungwa katika jela ambayo Gordons Park aliwekwa rumande kutoa taarifa polisi kuwa Park aliwahi kukiri kumuua mkewe kwa kumpiga na kitu kizito kichwani, watu hao waliokuja kujulikana kwa majina ya Michael Wainwright na mwenzake, Glen Banks walimnukuu Park akiwaambia; “…anastahili kufa, kwani nilimkuta chumbani akiwa na mwanaume mwingine.”

Itaendelea

Chanzo: Raia Mwema - Kisa cha mwanamke wa ziwani – 1
 
Ahahahahaha anayeisimulia ktk RAIA mwema ni mwana Jf nguli
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…