Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria Abubakar Shekau, amejiua mwenyewe , wanamgambo wa kundi hasimu wamesema katika sauti iliyorekodiwa.
Katika rekodi ya sauti iliyopatikana na mashirika ya habari, kundi la Islamic State katika mkoa wa Afrika Magharibi (Iswap) lilisema Shekau alifariki baada ya kujilipua kwa kutumia vilipuzi wakati wa mapigano kati ya makundi hayo mawili.
Shekau aliripotiwa kufariki mwezi uliopita na awali ashawahi kuripotiwa kuuawa. Boko Haram wala serikali ya Nigeria haijathibitisha kifo chake.
Rekodi hiyo ilisema nini?
Katika sauti ambayo haikuwa na tarehe iliyorekodiwa, sauti inayodhaniwa kuwa ya kiongozi wa Iswap Abu Musab al-Barnawi ilisema Shekau "alijiua kwa kujilipua na vilipuzi".
Wapiganaji wa Iswap walimsaka mbabe huyo wa kivita na kumpatia nafasi ya kutubu na kujiunga nao, al-Barnawi alisema.
"Shekau alipendelea kudhalilishwa katika maisha ya baadaye kuliko kudhalilika duniani," alisema.
Wakati ripoti za kifo cha Shekau katika mapigano ziliposambazwa mwezi uliopita, jeshi la Nigeria lilisema litachunguza.
Msemaji wa jeshi Brigedia Jenerali Mohammed Yerima aliiambia BBC wakati huo kwamba jeshi lilikuwa linachunguza kile kilichotokea, lakini halitatoa taarifa hadi lipate uthibitisho rasmi.
Mwandishi mmoja aliye na uhusiano wa karibu na vyombo vya usalama alisema kuwa Shekau alikufa wakati Iswap iliposhambulia ngome za Boko Haram katika msitu wa Sambisa, kaskazini mashariki mwa Nigeria
Aliripotiwa kufa mara kadhaa, lakini akijitokeza tena.
Abubakar Shekau ni nani?
Baada ya kuchukua uongozi wa of Boko Haram mwanzilishi wake alipofariki katika kizuizi cha polisi mwaka 2009, Shekau aliongoza mabadiliko yake kutoka kwa dhehebu la kawaida hadi uasi mbaya ambao umeenea kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Shekau alitumia video za propaganda kukuza itikadi yake ya vurugu. Chini ya uongozi wa Shekau, Boko Haram walifanya mashambulio ya mabomu, utekaji nyara na kuvamia magereza katika eneo hilo.
Kuanzia mwaka 2014, kundi hilo lilianza kuvamia miji katika juhudi za kuunda jimbo la Kiislamu kwa kutumia sheria za Kiislamu.
Akisadikiwa kuwa na miaka arobaini na kitu, Shekau aliunga mkono kampeni ya umwagaji damu katika video za propaganda ambazo zililinganishwa na Osama Bin Laden.
"Nafurahia kuua ... jinsi ninavyofurahia kuchinja kuku na kondoo," alisema katika moja ya video hizo mwaka 2012.
Tangu alipochukua uongozi, zaidi ya watu 30,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili kufurushwa makwao. Kundi hilo lilipata umaarufu kimataifa mwaka 2014 wakati lilipowateka nyara mamia ya wasichana katika shule moja mjini Chibok katika jimbo la Borno na kuchochea harakati za #BringBackOurGirls. Wengi wao mpaka sasa hawajulikani waliko.
Muda mfupi baadaye, Marekani ilimtaja Shekau kuwa "gaidi wa kimataifa" na kutangaza zawadi ya dola milioni saba kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.
Ajenda ya Shekau ilikuwa kali sana na ilikataliwa na Dola la Kiisilamu, ambalo liligawanyika kutoka Boko Haram na kuunda Iswap mnamo 2016.
Je Boko Haram sasa inaelekea wapi?
Endapo kifo cha Shekau kitathibitishwa, haijulikani kama itakuwa mwisho wa Boko Haram, wachambuzi wanasema. Tangu walipotengana, Iswap imesambaratisha nguvu ya Boko Haram kama kundi la kigaidi katika eneo hilo.
Baadhi yao wanatabiri kifo cha Shekau' huenda kikakomesha uhasama mkali kati ya makundi hayo mawili, wengine wanasema watadumisha maoni yake.
BBC