Msiwakate watoto vimeo kwa sababu zozote, inaweza pelekea mtoto kupoteza maisha kutokana na kuvuja damu; kama mtoto ana shida yoyote muone daktari atakushauri tiba sahihi.
- Tunachokijua
- Kimeo au kilimi kwa jina la kitaalamu huitwa Uvula.
Hiki ni kiungo kidogo kinachopatikana nyuma ya koo la binadamu. Kinaweza kuonekana kirahisi pindi mtu anapofungua kinywa chake.
Uvula (Kimeo/Kilimi)Kiungo hiki kilichotengenezwa kwa ngozi laini husaidia mambo kadhaa ikiwemo kumeza vyakula na kuzungumza. Huzuia chakula na vimiminika kuingia puani pia huzalisha mate yanayofanya kinywa kibaki kibichi muda wote.
Kimeo au Kilimi sio ugonjwa. Ni kiungo ambacho kila binadamu huzaliwa nacho.
Hata hivyo, kiungo hiki kikivimba au kupata maambukizi kinaweza kusababisha kuwasha kwa koo, ugumu katika kuvuta hewa (kupumua), kikohozi na homa.
Sababu za kukatwa kwa Kimeo
Utafiti wa Siri Lange na Dorcas Mfaume wenye kichwa cha habari "The folk illness kimeo and “traditional” uvulectomy: an ethnomedical study of care seeking for children with cough and weakness in Dar es Salaam" unabaishisha kuwa baadhi ya maneneo nchini, katika kila kundi la watoto 3 mmoja wao huwa wamekatwa kimeo.
Aidha, utafiti huu unafafanua kuwa walezi wengi jijini Dar es Salaam kwa kawaida huwapeleka watoto wanaougua kikohozi, kutapika na udhaifu kwa mhudumu wa afya ili watibiwe. Mtoto asipopona haraka kiasi, wengine huanza kuhofia kwamba mtoto huyo anaweza kuugua ugonjwa wa kienyeji wa kimeo.
Kimeo huchukuliwa kuwa ugonjwa mbaya, unaohatarisha maisha ambao watoa huduma za afya hawana uwezo wa kutibu. Ikitoea kikohozi hicho hakijapona kwa haraka kwa tiba za hospitalini, walezi huamua kutibu kwa njia zisizo rasmi ambazo hazijathibitishwa kitabibu.
Walezi huwachukulia wahudumu wa kitamaduni kama wataalam wanaotoa huduma ambayo inachukuliwa kuwa bora na salama.
Maelezo ya kitabibu kuhusu ukataji wa kimeo
Juni 24, 2021, Gazeti la Nipashe lilifanya mahojiano na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo (ENT) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dr. Jaria Rahib aliyebainisha kuwa kukata kimeo ni nadharia isiyokubalika kwenye taratibu za kitabibu, badala yake zipo tiba zinazohusiana na koo na daima hospitalini hakukatwi kimeo.
“Hata wanaokata kimeo sio wataalamu wa afya, magonjwa ambayo yanaonekana yanayohusu kimeo ni magonjwa mengine ambayo yanahusu sehemu zingine za koo na si kimeo.
Magonjwa ambayo yanahusu kimeo ni mengine kabisa. Kama una shida yoyote ambayo unadhani ni kimeo, ni bora ufike hospitalini.”
Aidha, Septemba 9, 2019, Mwandishi Deo Kaji Makomba kupitia Makala ya afya yako inayoandaliwa na idhaa ya DW aliwahi pia kufanya mahojiano na Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno kutoka kitengo cha afya cha Chuo Kikuu Dodoma Dr. Zacharias Shukuru aliyesema kuwa utamaduni huu umekuwepo kwa muda mrefu, na sehemu nyingi za Tanzania huchukulia tatizo la kukohoa au kubana kwa kifua muda mrefu husababishwa na kilimi (kimeo).
“Kilimi ni sehemu ya mwili wa binadamu katika sehemu ya juu ya kinywa. Sio ugonjwa, ni sehemu ya mwili wa binadamu.
Kilimi hakina madhara kwa afya ya binadamu, kinasaidia wakati wa kumeza chakula, lakini pia tunapozungumza ili tuweze kutoa sauti sahihi tunahitaji kuwa na kilimi. Na ndio maana hata pale kinapokuwa kinakatwa, kati ya vitu ambavyo wagonjwa watakuja kulalamika ni chakula au maji akinywa yanatokea puani au wakati mwingine analalamika sauti imebadilika, ni kwa sababu ya eneo lile kuwa limekatwa.”
Utamaduni huu unafafanuliwa zaidi na Prof. Francis Furia, Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili aliyezungumza na JamiiForums Agosti 9, 2023 na kubainisha kuwa kitaalamu kimeo hakipaswi kukatwa.
Wanaofanya hivyo ni Wataalamu wa Tiba Asilia wakiamini kuwa Mtoto akiwa anakohoa sana ndipo anatakiwa kukatwa.
Zaidi, Prof. Furia anafafanua;
“Kitaalam Mtoto kukohoa inamaanisha kuna changamoto nyingine ya kiafya ambayo inafanya iwe hivyo na inatakiwa kupatiwa tiba sio kuondoa ‘uvula’ ambacho pia kinafahamika kwa majina mengine mengi kama Kimeo, Kidaka Tonge.
Kwa asilimia kubwa wanaokatwa inatokea katika maeneo ambayo si salama kiafya, hivyo kuna Watoto wanapoteza damu nyingi, wanameza damu, wanapata maambukizi ya bakteria na wengine wanapoteza maisha.
Pia inaweza kusababisha upungufu mkubwa wa damu.”
Prof. Furia anatoa wito kwa Jamii itambue kuwa kimeo si ugonjwa wala hakina madhara ya uwepo wake hapo na kinakuwepo siku zote hadi mtu anapokua mtu mzima.
Hivyo, kwa kutumia rejea hizi pamoja na tafiti mbalimbali ambazo JamiiForums imezipitia, imethibitika kuwa kimeo ni kiungo kisichopaswa kuondolewa na uondoaji wake unaweza kusababisha madhara makubwa kwenye afya ya mhusika.
Ushahidi wa madhara ya kuondoa kimeo
Februari 13, 2015, Gazeti la Mwananchi liliwahi kuripoti kisa cha mtoto aliyekatwa kimeo kwa maelekezo ya shangazi zake walioshauri wazazi afanyiwe hivyo ili apone tatizo la kikohozi lililokuwa linamkabiri.
Badala ya kupata ahueni, mtoto huyo alianza kukohoa damu, kujisaidia choo cheusi, homa kali na baadae aliishiwa damu, hali iliyomfanya apewe rufaa ya kufika Muhimbili ili apatiwe matibabu ya kibingwa zaidi.
Madhara mengine yanafafanuliwa na utafiti mwingine wenye kichwa cha habari “Morbidity and Mortality following Traditional Uvulectomy among Children Presenting to the Muhimbili National Hospital Emergency Department in Dar es Salaam, Tanzania” wa HR Sawe et al (2015) uliofanyika kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili unabainisha kuwa watoto wengi waliofikishwa hapo na kugundulika kuwa wamekatwa vimeo walikuwa na homa kali, upungufu mkubwa wa hewa mwilini, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kuvujia kwa damu kwenye mfumo wa chakula, maambukizi makubwa ya vimelea vya magonjwa na upungufu mkubwa wa damu.
Aidha, kwa kuwa zoezi hili hufanyika kienyeji, baadhi ya watoto hupoteza maisha na wengine wakiishia kupatwa na Pepopunda (tetanus), maambukizi ya VVU na homa ya ini kutokana na matumizi ya vifaa visivyotakaswa kitaalamu ambavyo hutumika kwa kila mgonjwa.