MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imepanga kusikiliza kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5, Juni 21 mwaka huu, kesi hiyo inawakabili vigogo watatu wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Asteria Mlambo,anaandika Faki Sosi.
Washtakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Fedha, Evodius Katale na Mwanasheria Mwandamizi, Francis Kugesha wote wa Dart na mfanyabiashara Yuda Mwakatobe.
Kesi hiyo iliitwa mbele Respicious Mwijage Hakimu Mkazi, kwa ajili ya kutajwa
Awali washitakiwa walisomewa maelezo ya mashtaka yao Mei 31.
Inadaiwa kuwa, Septemba Mosi na Oktoba mwaka 2013, mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu, wakiwa watumishi wa Dart walishindwa kutimiza majukumu yao kwa weledi na kuisababishia serikali hasara ya Sh 83,564,367.
Katika mashtaka mengine inadaiwa, Machi 26, 2005 na Juni 26, mwaka 2004 katika ofisi ya TRA, zilizopo wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Mwakatobe aliwasilisha nyaraka za kughushi kuhusu taarifa ya mahesabu ya Kampuni ya Yukan Business Co. Ltd kwa maofisa wa TRA na kusababisha kulipa kodi ndogo.Washtakiwa walikana mashtaka yote yanayowakabili na wote wapo nje kwa dhamana