Unapotua tu katika mtaa huu wa Keko Mwanga katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam utagundua mabadiliko ya hewa tofauti na ulipotoka, harufu inayotoka hapa, hewa inayovutwa eneo hili si ya kawaida na maeneo mengine, harufu ni kali na mbaya ya uchafu.
Harufu hii inatokana na mitaro ya maji taka iliyojengewa na ambayo haijajengewa iliyo karibu kabisa na makazi ya watu umbali wa takriban hatua chache tu kutoka makazi ya Watu na shughuli nyingine.
Ukifika katika mtaa huu wakazi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida wapo Wafanyabiashara, wanaolima mbogamboga za majani na wanaoendelea na shughuli za nyumbani.
Barabara, maeneo ya kupumzika na hata nje ya nyuma zao kumetapakaa maji ambayo yanatoa harufu mbaya.
CHANZO CHA MAJI TAKA NI NINI?
Ukuta wa moja ya jengo la mwekezaji ambaye wananchi wanadai kuwa ni Azania Group umejengwa eneo ambalo linapaswa kujengwa mfereji wa kupitisha maji taka, hivyo eneo hilo linazuia maji kupita kwenda katika mfereji unaoenda kumwaga maji baharini na hali huwa mbaya hususani kipindi cha mvua
Tatizo hili lilishawahi kutolewa maamuzi, mmoja wa waliotoa maamuzi ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Mobhare Matinyi, Mwaka 2023 kuwa ubomolewe ili kupisha mfereji lakini mpaka sasa ukuta huo bado upo.
Tatizo lingine ni Mkusanyiko wa maji kutoka katika viwanda vya eneo la Chang’ombe ambapo mitaro inayopitisha maji imepita katika makazi ya watu, hivyo matokeo yake imekuwa njia ya wakazi wa eneo hilo kuelekeza maji taka ya chooni kwenye mitaro hiyo.
Maji taka kutoka Gereza la Keko ambayo yanaingia katika mtaro huo ambayo huchepuka na kwenda katika makazi ya watu
Utiririshaji wa maji ya chooni kutoka kwa wananchi wenyewe na utupaji wa taka ngumu.
HALI YA MITAA IPOJE
Mitaro hii imepita katikati ya makazi ya watu na maeneo mengine kama Morem ambapo maji machafu ya mtaroni yanaingia hadi katika makazi ya watu hali inayowalazimu baadhi kuyasukuma bila kuwa na vifaa kinga vyovyote.
Mtaa huu unatoa harufu mbaya kila eneo, na makazi ya watu, biashara na shughuli za ulimaji mbogamboga zinafanyika karibu kabisa na mitaro hiyo inayotoa harufu muda wote.
Lakini pia njia nyingi za mtaa huu zimejaa maji hayo ambayo yanatoa harufu na ni machafu hata kwa kuangalia kwa macho na Watoto wanapita na kucheza hapo hapo.
Kikubwa kilichopo hapa ni harufu hii na mitaro kupita karibu kabisa na makazi ya watu, kuna maeneo ambayo hayana mitaro iliyojengewa na maji yanasambaa hadi katika nyumba.
AFYA MASHAKANI
Licha ya kuwa wamezoea harufu hiyo kali, Wakazi wa eneo hilo wanahofia hali zao za kiafya hususani kwa watoto.
Mmoja wa wakazi hawa anabainisha walikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu hivi karibuni na hata vifo katika kipindi cha takribani miezi miwili kupita na baadhi ya maeneo katika mtaa huu yalifungwa kuzuia maambukizi, japokuwa haikutangazwa.
Hata hivyo kuvuta hewa chafu kila siku kunaweza kusababisha madhara, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO wa Mwaka 2022 unasema chembechembe zinaweza kupenya ndani kabisa ya mapafu na kwenye mkondo wa damu na kusababisha magonjwa ya moyo na matatizo ya kupumua.
Je, watu wa eneo hili wapo salama kiasi gani?
Wananchi wa Mtaa wa Keko Mwanga wanaomba Serikali iwasaidie kufunika mitaro ya maji taka pamoja na kuirekebisha vizuri ili kuondokana na harufu ambayo imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Wakati wa mvua mitaro hii hufurika maji hayo machafu na huingia katika makazi ya watu.
Serikali ichukue hatua na wawekezaji walionunua maeneo ambao wamejenga kuta ambazo zinazuia maji na kuyafanya yaingie katika makazi ya watu. Moja ya jengo linasemekana ni jengo la kuhifadhi kontena la Azania ambalo ni kero hususani kipindi cha mvua.