WAZIRI Mkuu wa India, Narendra Modi amewasili nchini usiku wa kuamkia leo, kuanza ziara rasmi baada ya kuzuru nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.
Ziara yake nchini ni sehemu ya ziara ya siku kadhaa katika mataifa ya Afrika, ambapo baada ya kutoka hapa atakwenda Kenya. Tunamkaribisha Tanzania na kumtaka yeye na ujumbe wake, kujisikia kama wapo nyumbani katika kipindi chote watakapokuwa hapa nchini.
Tunaelewa kuwa lengo la kwanza la safari hiyo ni kuboresha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya India na nchi za bara la Afrika. Lakini, pia ujio wake hapa nchini ni furaha ya aina yake, kutokana na mengi tutakayojifunza kutoka kwake na kwa taifa la India.
Furaha hiyo inatokana na ukweli kuwa taifa letu, limeanza safari ya kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda, hivyo ujio wa kiongozi wa taifa hilo, ambalo limetoka katika umaskini na kuongeza kipato kwa taifa na wananchi wake, ni fursa adimu ya kujifunza kwa wenzetu hao.
Aidha, tunaamini kwamba ujio wake, utasukuma mbele makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano mkubwa wa mataifa ya Afrika na India, uliofanyika New Delhi nchini India Oktoba mwaka jana.
Katika mkutano huo wa New Delhi, serikali ya India iliwaeleza marais na mawaziri wakuu wapatao 40 wa nchi za Kiafrika, nia ya kushirikiana na mataifa ya Afrika katika nyanja za uchumi, viwanda na biashara.
Tunatambua kwamba kwa mwaka India huwekeza karibu dola bilioni 75 katika sekta za nishati, viwanda na madini barani Afrika, kwa hiyo ujio wake utasaidia kuleta makubaliano ambayo yatawezesha kuhamisha teknolojia kutoka India ili watanzania waweze kushiriki katika kuvuna rasilimali zao za asili ipasavyo.
Pia, tunatambua kwamba kwa miaka minne iliyopita, wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara wa India, wamewekeza barani Afrika karibu dola bilioni saba na milioni 400 na ujuzi wao, hasa kwa kuwekeza kwenye viwanda vidogo na utengenezaji malighafi kwa viwanda vikubwa.
Ziara hii ni neema kwa Tanzania kutokana na ukweli kuwa tuna rasilimali nyingi ya gesi asili na makaa ya mawe, wakati India wao wana mahitaji makubwa ya nishati. Kutokana na mwingiliano wa mahitaji, tunaamini kwamba ziara ya Modi ina baraka za aina yake; na ndio maana tunamkaribisha ili tuweze kugawana neema ambazo Mungu amejaalia kila nchi, ambapo wenzetu wana teknolojia na sisi tuna rasilimali.
Ziara yake itatuwezesha wananchi wetu kushirikiana kwa dhati kwa manufaa ya wote na kuimarisha uchumi wa mataifa yetu. Uchumi wa India unakua kwa kasi ya asilimia nane na nchi hiyo ni mshirika wa sita wa kibiashara na bara la Afrika. Watanzania wanatakiwa kusaka teknolojia na mitaji ya uwekezaji kutoka katika taifa hilo.
Tunasema kusaka teknolojia na uwekezaji kwa kuwa hilo likiwezekana, tutakuwa tumewakomboa pia wakulima wetu, ambao wamekuwa wakilazimika kuuza bidhaa nje zikiwa ghafi.
Sifa moja ya India ni kuwa ni nchi yenye viwanda vingi vidogo na vikubwa na kwa kiasi kikubwa ina rasilimaliwatu wenye uwezo wa ufundi mchundo. Hili linaweza kuangaliwa na Watanzania katika safari yetu kuelekea uchumi wa kati.