KAMPUNI kutoka Falme za Kiarabu, Rental Solutions and Services LLC imeiburuza mahakamani kampuni ya kufua umeme ya Symbion Tanzania Limited, ikidai kulipwa Dola za Marekani 228,070,655.67 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 560 kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya kuzalishia umeme nchini.
Kesi hiyo Namba 234 ya mwaka 2016 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Mdaiwa wa pili katika shauri hilo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo limeunganishwa katika kesi hiyo kama mdau mkuu kwenye sakata hilo ambapo maamuzi yatakayotolewa na mahakama yanaweza kuiathiri.
Katika hati ya madai, Kampuni ya Rental Solutions and Services inadai Symbion Dola za Marekani 28,070,655.67 kama malimbikizo ya gharama za ukodishwaji wa mitambo, ambayo hadi sasa Symbion imeshindwa kulipa na pia katika shauri hilo Symbion itatakiwa kulipa Dola za Marekani milioni 200 ambazo ni fidia kwa kampuni hiyo kula hasara kutokana na Symbion kuvunja masharti ya mkataba na kuchelewesha au kushindwa kufanya malipo hayo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, fedha hizo zinatokana na kazi zilizofanywa na kampuni hiyo ya Uarabuni ya kusambaza, kusimika na kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ambayo ilikodishwa na Symbion kwa matumizi ya miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme kwa ajili ya Tanesco ili usambazwe kwenye Gridi ya Taifa kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Rental Solutions and Services pia katika kesi hiyo, inaiomba Mahakama kutamka kuwa kushindwa kwa Symbion kulipa gharama hizo za ukodishaji kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba na pande zote mbili kumesababisha uvunjifu wa mkataba na hivyo sio halali na haistahili kuendelea.
Inadaiwa kuwa kati ya Septemba 2011 hadi Juni 2013, Rental Solutions and Services iliingia mikataba mbalimbali na Symbion ambapo pale ilipohitajika mikataba hiyo iliongezewa muda ili kukidhi mahitaji kwa mujibu wa mikataba hiyo kwa lengo la kusambaza na kusimika mitambo ya umeme ili kusambazwa kwenye Gridi ya Taifa.
Septemba 21, 2011 kampuni hiyo ya Uarabuni iliingia mkataba na Symbion kwa ajili ya kusambaza na kusimika mitambo ya umeme katika Kituo cha Zuzu cha Tanesco chenye nguvu ya kilovolti 33 kilichoko Dodoma yenye uwezo wa kuzalisha megawati 50.
Katika mitambo hiyo, pande husika zilikubaliana malipo ya Dola za Marekani 1,374,500 kwa mwezi kwa kipindi ambacho kingeishia miezi sita. Inadaiwa kuwa kwa kipindi hicho, Symbion ingepaswa kulipa jumla ya Dola za Marekani 8,247,000.
Hati ya mdai inaonesha kuwa mkataba kama huo uliingiwa na pande zote mbili Februari 12, 2012, kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 55 kwa kipindi cha miezi 12 kwa gharama ya Dola za Marekani 1,666,000 kwa mwezi.
Mitambo hiyo ipo katika vituo vya Arusha na Dodoma. Kwa mujibu wa hati ya madai, kulikuwepo na ongezeko wa muda wa matumizi wa mitambo hiyo katika vituo vya Dodoma na Arusha ambapo Rental Solutions and Services ilitimiza matakwa yake kama ilivyo kwenye mikataba na iliwasilisha hati za malipo kwa Symbion ili kukamilisha malipo ya kukodi kitambo hiyo kama inavyotakiwa.
Pamoja na Rental Solutions and Services kutimiza masharti ya mikataba hiyo, kati ya Dola za Marekani 77,667,666.28, Symbion imelipa dola 49,597,010.61 tu. Hivyo, Rental Solutions and Services inadai kuwa hadi sasa, bila uhalali wowote, Symbion imeshindwa kutimiza masharti ya mkataba kwa kutolipa kiasi cha dola 28,070,655.67.