Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Shaka Hamdu Shaka leo akiwa katika kata Mudida ameendelea na kazi za kisiasa akishiriki mikutano ya ndani ya kampeni ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida Kaskazini unaotarajiwa kufanyika Januari 13 Mwaka huu
Mapema asubuhi amepokewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida Vijijini William Nyalandu , Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Singida Vijijiji Amos Kimasi na Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Singida Vijijini Neema Isambaa na Katibu wa UVCCM wilaya ya Singida vijijini Zainab Abdallah.
Amepokewa katika ofisi za CCM Kata ya Mudida na baadae akazungumza na wanachama wa CCM na jumuiya zake Mkoani hapa.
Katika msafara wake amefuatana na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Denise Nyihara, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida Mjini Lucia Mwilu na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Singida Hemed Ferej.
Wengine ni Katibu wa CCM Singida Mjini Sylvester Yared , Naibu Meya wa halmashauri ya Manispaa ya Singida Yagi Maulidi Kiharatu.
Akishiriki kwenye mkutano huo wa ndani Shaka amesema CCM itaendelea kufungua milango ya kuwakaribisha wanachama na viongizi toka upinzani wenye nia ya dhati katika kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli.
Amesema Wapinzani hawarudi CCM kwa kushinikizwa na Mtu yeyote bali utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ndiyo unaowavutia na kuwajengea matumaini mapya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Aidha Kaimu Katibu Mkuu UVCCM, Shaka amewatolea wito Wanasiasa wawili wa upinzani Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, warejee CCM kwakuwa mahali waliko hakufanani na heshima zao.
Amesema Maalim Seiif kabla hajaenda upinzani amewahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri Kiongozi wa SMZ na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM huku Lowassa akibahatika kuwa Waziri Mkuu, Mbunge, Waziri na Mjumbe wa Kamati Kuu hivyo hadhi zao hazifanani na maeneo waliko .
"Wasione aibu au noma kurudi katika chama walichokitumikia toka wakiwa vijana wadogo na kuwafikisha mbali kisiasa kwani waliokuwa wakiyatamani yatokee sasa yanatekelezwa kwa ufanisi na serikali zote mbili "Alisema Shaka.
Shaka alisema ikiwa Maalim Seif na Lowassa kwa nyakati tofauti wamejenga uthubutu wa kusifu utendaji wa Rais Dk Magufuli kwa hatua anazizichukua ikiwemo kupambana na rushwa , ufisadi na ubadhirifu, hawana haja ya kubaki upinzani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida Mjini Lucua Mwilu amesema wapinzani wamekuwa na tabia kama chura kwani hutokea nyakati za masika ila vipindi vya kipupwe na kiangazi hapotea.
Shaka amesema uhodari wa upinzani ni kuziponda Serikali bila ya kuwa na hoja za maana wakati hawana ubavu wa kutenda jambo lolote.
"Kazi yao ni ulalamishi na kususa wakati Serikali ndiyo inayojenga zahanati, barabara, kupeleka miradi ya maji, umeme na kusaidia Wakulima na Wafanyakazi" Alisema Shaka