Juma Duni Haji na Maalim Seif Sharif Hamad; Usawa na Tofauti zao katika Kuyaendea Mapambano ya Kisiasa Zanzibar

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa kiongozi wa siasa na mapambano ya kisiasa ya kambi ya upinzani Tanzania, ambae alijaaliwa ushawishi mkubwa zaidi kwa upande wa Zanzibar tokea miaka ya 1988 alipofukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi na serikali hadi pale umauti ulipomfika, mwezi Februari, 2020. Katika mstari wa mapambano, Maalim alikuwa na sifa ya misimamo madhubuti kwa alichokipigania. Hakuyumba, hakughilibika na hakurudi nyuma kutoka aliposimama ila kwa lengo la kutafuta hatua na nguvu zaidi za kusonga mbele. Hakuvunjika moyo katika safari yake ya mapambano aliyoiamua kuiendea takribani kwa robo tatu za uhai wake wote, japokuwa nguvu iliyotumika kumvunja moyo ndani na nje ya Chama ilikuwa kubwa.

Maendeleo ya kisiasa yaliyopigwa kwa upande wa Zanzibar hayaachi hata kidogo kunasibiana moja kwa moja na namna Marehemu Maalim Seif alivyoamini katika siasa za kiungwana na kuzibeba ajenda za siasa za kistaarabu za umoja, uzanzibari kwanza, haki kwa kila mwananchi na Maridhiano ya kweli. Mabadiliko chanya ya kisiasa yaliyofikiwa kule Zanzibar katika kipindi cha miaka 10 iliyopita yakiwemo kupunguwa kwa wimbi kubwa la uhafidhina wa siasa za miaka ya 1950 na 60 za uafro, uhizbu, ubwana, utwana, weupe na weusi; kulegezwa kwa kasi ya ubaguzi kwa misingi ya kiasili, kisiasa na kimaeneo kama vile upemba, uunguja, ukaskazini na ukusini; marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kunaakisi matunda ya mapambano yaa Maalim Seif juu ya kile alichoamini kuhusu ipi hasa inapaswa kuwa siasa yenye tija kwa Zanzibar.

Marehemu Maaim Seif alijipambanua kama kiongozi mpole na mwenye subra iliyopitiliza. Alisubiri na kuwa mpole hata pale alipochokozwa na watesi wake katika kilele cha hisia zake. Kila miaka ilivyokuwa inasonga, subra hii iliyopitiliza ilianza kuhojiwa na hata wafuasi wake waliompenda sana. Kuna waliokwenda mbali zaidi wakiihusisha subra hii ya Maalim Seif na sababu ya hali kubaki kama ilivyo kwa upande wa upinzani kutokana na kiwango kikubwa cha subra yake iliyolea muendelezo wa jeuri na kiburi cha watawala wa Zanzibar. Mara nyengine alikuwa mpole katika jambo ambalo watu wengi waliamini hapaswi kuwa mpole bali linahitaji maamuzi magumu.

Subra ya Maalim Seif pia ilidhaniwa ilikuwa ndio sababu kuu ya wapinzani wa serikali upande wa Zanzibar kushindwa kufikia lengo lao kuu la kutwaa hatamu za Dola badala yake kubaki kuwa wahanga wa kila uchaguzi. Wako walioamini kwa dhati kuwa subra na upole wa Maalim Seif ulikuwa mtaji muhimu wa CCM na watawala. Wapo waliojiridhisha kuwa subra ya Maalim Seif pia ilikuwa ikichongwa washauri wake wakuu ndani ya Chama, kundi lililomzunguka linalojiita “wanamkakati” kwa umaarufu (Deep State) ambalo halikuwahi kutamani kuona Maalim Seif anashika hatamu za Dola. Kundi hili siku zote lilikuwa likijaribu kwa kila nguvu waliokua nayo kumfanya Maalim Seif asalim amri kila alipojaribu kukabiliana. Marehemu Maalim Seif alikubali kuingia katika Muwafaka mwengine hata kama watawala walishindwa kuutekeleza kitu chochote cha muhimu katika Muwafaka wa uliotangulia. Alikubali kuingia katika Maridhiano ya Novemba 5, 2009 hata kama ule Muafaka wa Tatu uliishia bila ya kuonesha dhamira njema, uliojaa ujanja, ghilba, jeuri na kiburi kutoka upande wa CCM.

Alikubali kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 hata kama CCM haikushinda uchaguzi ule sawa tu na chaguzi zilizopita, akiwa na lengo la kuyanusuru Maridhiano na hatua za kisiasa zilizokwisha kupigwa kati yake na Rais Mstaafu Amani Karume, akiamini Maridhiano hayo yatakuwa mbegu muhimu na mwanzo mwema katika kuleta salama, amani ya kudumu, kuheshimiana, kuheshimiwa misingi ya demokrasia, haki na siasa za kistaarabu.

Bila shaka subra yake ilimaanisha aliangalia mambo kwa jicho tofauti na wengi, jicho la huruma badala ya jicho la kiburi, jicho la imani badala ya jvisasi, jicho la maslahi mapana ya nchi na watu wake zaidi ya hisia za kibinadamu na faida ya vyama vya siasa ambayo huja na kuondoka.

Maalim Seif, simba aliekuwa na meno na kucha kali lakini ambae hakuwahi kutafuna hata alipovutwa sharubu zake, amekufa, lakini amewacha simba mkali mno. Simba huyu kamwe hatabasamu sehemu ambayo anapaswa kuwa mkali. Hawi mtazamaji na mlalamikaji ambapo anapaswa kukwarura. Simba huyu anaheshimu mstari uliopo baina upole wake, ukali wake na anachokipigania. Huyu yeye katu hakubali kuvaa udhaifu kwa jina la upoe na subra. Huyu kamwe hatishwi na vifaru wala mzinga. Huyu hababaishwi na Deep State waliokuwa wakimzuga Maalim Seif kila wakatiwa Uchaguzi Mkuu. Pale wakati ambao anatakiwa kusimama kama shujaa na kuongoza mapamban husimama na kufanya hivyo bila kujali waoga ndani yake wako tayari au laa. Kwake yeye mapambano ni mapambano kwa tafsiri yake halisi ya vuta nivute mpaka mwenye haki yake aipate.

Juma Duni kamwe haihesabu ile falsafa ya “kukubali yaishe” iiyozoeleka katika CUF na baadae ACT hapa Zanzibar kuwa eti nayo ni hatua ya mapambano. Yaani damu ya upinzani tu imwagwe kila baada ya uchaguzi mkuu na mdogo halafu wapinzani wakubali yaishe. Huyu si mwengine ni Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa sasa wa Chama cha ACT-Wazalendo ambae anaomba tena kurudi kuwa Mwenyekiti wa Chama kwa Awamu ya Pili. Maalim Seif na Juma Duni ni viongozi waliolingana kwa mengi lakini waliotafautiana katika falsafa zao za kuyaendea mapambano yao ya kudai haki dhidi ya watesi wao.

IMG-20240226-WA0007.jpg


Juma Duni nae katika mazingira ya mwanadamu wa kawaida ni mpole sana. Ukikutana nae na kuzungumza nae mambo ya kawaida ya maisha ya kila siku, unaweza ukaamini ni mpole zaidi ya Maalim Seif. Hapendi kujikomba, hapendi anasa. Hapendi ukuu na kujiweka mbele. Hii ndio maana kwake yeye ilikuwa rahisi kuziwacha neema za ukubwa serikalini katika miaka ya 1980 mwishoni na kujiunga katika wimbi la kupigania haki za wanyonge wanaoonewa na kubaguliwa na kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano bila ya kujali kupoteza cheo cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ofis ya Waziri Kiongozi alichokuwa nacho.

Ukikutana na Juma Duni, utakuwa umekutana na mtu aliejaa bashasha, utulivu, wema na ukarimu. Ukimya na utulivu wake utadhani ni mtu mnyonge sana. Hata hivyo unyonge na upole wa Juma Duni unabaki katika kukamilisha haiba yake na heshima yake inayompambanua katika jiha ya mahusiano yake na jamii. Ukimya ni khulka yake ya kipekee ya namna anavyoamiliana na watu., unyonge na ukimya wa Juma Duni haupo kabisa katika misimamo yake ya Upole mapambano ya kudai haki na kukataa dhulma ambayo ndio msingi mkuu wa siasa zake.

Kama Maalim Seif, Juma Duni pia si mtu wa kukurupuka, ni mtu mwenye subra. Yeye hata ukimfika na pupa lako, malalamiko yako dhidi ya mwengine au kumueleza jambo lako unalohisi linahitaji hatua za haraka, yeye hukujibu “Babu tulia wakati utasema”. Juma Duni siku zote huweka mbele uwezekano wa kuepusha shari na kuleta salama katika hali na mazingira yote kwa kadri inavyowezekana hata ikimgharimu kukosa maslahi yake binafsi.

Hii ndio sababu alikuwa mwana mkakati mkuu wa Miafaka ya Kisiasa na utekelezaji wake katika miaka ya 1990 na 2000 pamoja na kwamba anaofanya nao Miafaka hiyo walimueka na kumtesa gerezani huku wakimdhihaki kwa muda wa miaka minne bia hatia yoyote. Ndio maana pia aliweza kuruhusu mpito wa kukabidhi madaraka kuwa mwepesi baada ya kufariki Maalim Seif, kwa hatua yake yeye mwenyewe, ambae alikuwa na sifa zote kurithi wadhifa wa Makamo wa Kwanza wa Rais aliouwacha Maalim Seif lakini akampendekeza Othman Massoud Othman, aliekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kushika nafasi hiyo.

Hata hivyo Juma Duni hana subra iliyopitiiza mipaka. Subra yenye viashiria vya woga na kukosa la kufanya. Subra inayotoka nje ya nidhamu, misingi na hekima ya subra yenyewe. Subra yenye matokeo hasi na subra yenye kumpa dhalimu ushindi wa kudumu wa kudhulumu. Subra ya Juma Duni katika kudai haki ina mstari mwekundu uliokoza mwishoni. Akiufikia mstari huo hutaweza kumrejesha tena nyuma hata hatua moja. Pamoja na kuamini katika subra na uvumilivu kuwa nyenzo muhimu katika siasa na uongozi, Juma Duni anaamini falsafa nyengine muhimu za mapambano ya kudai haki kama vile “haki haiji katika kisahani cha chai”, “haki haiombwi bali inapiganiwa” n.k.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao Maalim Seif alishinda kwa wazi kabisa, chambilecho maneno ya vijana bila chenga ukiwa umemalizika, lakini bado Watawala wakawa wanafikiria njia ya kupindua meza huku wakitoa ishara za kuandaa mazingira ya vita na mauwaji ya wapinzani, timu ya viongozi wa upinzani Zanzibar, waandamizi wa Maalim Seif, walitofautiana juu ya maamuzi sahihi na njia ya busara zaidi ya kufuatwa ili kukabiliana na hali hiyo, katika hatua hiyo ya Wawala kuchanganyikiwa na katika kilee hicho cha matarajio makubwa ya wafuasi wa upinzani kuliko katka vipindi vyote tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Zanzibar.

Wakati huo baadhi ya wasaidizi wa Maalim Seif wa karibu wakiamua kurudi nyuma, kubaki ndani ya ukuta wa subra na kuepuka maamuzi yoyote yatakayosababisha vifo vya wafuasi wao, hali ilikuwa tofauti kwa upande wa Juma Duni. Tulifahamishwa kuwa yeye kwa upande wake alikuwa wazi katika msimamo wake uliotofautiana na wenzake. Yeye aliwahoji wenzake “kwanini tusihamasishe umma ulioko tayari huko nje kuchukua haki yao kwa hofu ya kufa?” “Kwani hatujafa sisi?” “Au tufe mara ngapi?” Aliendelea kupigilia msumari msimamo wake kwa kusema “wacha wa kufa tufe, watakaobaki watarithi Zanzibar yenye heshima na matunda ya kile tunachokipigania”. Hata hivyo msimamo huo wa Juma Duni ulipingwa na viongozi wenzake walioshiba siasa za Maridhiano ya ujanja na subra yenye kujengewa ukuta unaoitenganisha haki na matarajio ya umma.

IMG-20240222-WA0119.jpg


Sasa Juma Duni ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo. Ndani Chama ana ushawishi wa juu wa maamuzi ya kisiasa. Naufikiria sana mwaka 2025 na nauhofia ndio ule wakati ambao yeye mwenyewe amekuwa akisema wakati huo ukifika utasema wenyewe kuwa umefika. Nadhani wakati huo umekaribia. Hakuna ambacho CCM hawajaonesha wanapokuwa katika madaraka katika kupuuza matashi na maslahi ya umma, ubaguzi, ubabe katika ushindani wa kisiasa na katika chaguzi, kutesa na kuuwa bila hofu. Hakuna ambacho CCM hawajaonesha kwamba Maridhiano si lolote si chochote kwao bali ni nyenzo miongoni mwa nyenzo za siasa za hadaa.

Hakuna ambacho CCM hawajafanya kupuuza na kudharau subra na upoe wa Maalim Seif. Wameshaonesha pia kwa kila ishara na kwa vitendo kuwa Maridhiano ya kisiasa aliyoyaasisi Amani Karume kwa wao si chombo wala hatua ya kuleta salama na usuluhishi wa kisiasa bali ni daraja la muda mchache la kufunika damu waliyoimwaga isionekane na dunia. Ni filamu ya kuwapumbaza na kuwasahaulisha wale waliofanyiwa uhalifu na waliopoteza wapendwa wao. Ni mbinu ya kuwawezesha kuendelea kuwatawala kwa mkono wa chuma watu waliokasirika kutokana na uhalifu wa chaguzi zao.

Makala hii imekuja kuwasaidia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa ACT Wazalendo taarifa za mapema ili wafanye Chaguo sahihi. Mkala hii pia imekuja kuwaonya CCM wabadili utaratibu wao wa kufikiri waliouzoea linapohusika suala la maonevu kwa wapinzani Zanzibar kila unapofika uchaguzi mkuu. Makala imekuja kuwaonya CCM wafikirie upya utamaduni wao wa kuwachukulia poa wapinzani, chambilecho maneno ya vijana. Ule ujasiri wa CCM wa kuchafua chaguzi, kujeruhi, kubaka, kufunga watu magerezani na kuuwa ili washike hatamu za Dola na mwisho wa yote hayo, Maalim Seif huwa mtulivu na kutuliza watu wake na kufanya Mwafaka mpya, hautafanya kazi kwa wepesi bila gharama upande wa pili kama ilivyokuwa miaka yote huko nyuma.

Makala hii pia inauupima upepo wa siasa za Zanzibar na chaguzi za mwaka wa 2025 katika mizani ambayo upande mmoja kuna utamaduni wa ubabe na utapeli wa CCM na upande wa pili kuna Kamanda Mkuu mwengine, simba mpole lakini ambae huthubutu kuvutwa sharubu zake akatabasamu. Ni kiongozi wa mapambano aneamini hakuna mapambano yasiobeba gharama. Ni kiongozi ambae anasisitiza kuwa muda ukifika hakuna wa kulizuia linalopaswa kuwa. Hata hivyo tusimame hapa, kama ilivyo kauli Juma Duni “wakati utasema” lakini CCM wajitafakari upya kuwa baada ya kumzika Maalim Seif, mapambano ndio kwanza yanaanza upya na kwa sasa wanaingia katika uwanja wa vita ambao ni tofauti na waliouzoea kwa miaka 30 iliyopita.
 
Back
Top Bottom