Juliana Mwakang'ali: Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Ifutwe

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
620
1,543
HOTUBA YA WAZIRI KIVULI WA MALIASILI NA UTALII_ACT WAZALENDO NDG. JULIANA DONALD MWAKAN’GWALI KUHUSU MPANGO WA BAJETI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.

Utangulizi.
Kufuatia taarifa ya utekelezaji wa mujukumu na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ndg. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.) siku ya juzi Ijumaa tarehe 2 Juni, 2022 ambapo ilipokelewa na kujadiliwa na Bunge na kesho Jumatatu itahitimishwa. Sisi, ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii tumeisoma, kuichambua na kuimulika ili kuona kwa namna gani inaakisi matarajio na matamanio ya wananchi.

Aidha, kupitia uchambuzi wetu, tumeweza kutoa mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha na kwa miaka inayofuata. Katika kufanya hivyo, hotuba hii ya Msemaji wa Maliasili na Utalii wa ACT Wazalendo Ndg. Juliana Donald imebeba hoja sita (6) kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Zifuatazo ni hoja sita (6) za ACT Wazalendo kuhusu bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2023/24:

1. Operesheni ya kuwahamisha wananchi katika eneo la Ngorongoro.
Mgogoro wa ardhi kati ya wananchi (jamii ya wafugaji) na Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Ngorongoro na Loliondo umedumu kwa mrefu sana (tangu 1959). Kwa upande wa eneo la Ngorongoro ni eneo linalosimamiwa kwa msingi wa matumizi ya ardhi mseto kwa ajili ya; uhifadhi wa maliasili; kulinda maslahi ya wazawa (shughuli za binadamu); Na shughuli za utalii.

Kiini cha mgogoro ni Serikali na Mamlaka ya Ngorongoro kuweka msisitizo na kupendelea uhifadhi na utalii zaidi huku ikipuuza haki na nafasi ya wananchi katika matumizi ya eneo hilo. Serikali imekuwa ikiwanyima haki za Ardhi na uhakika wa miliki ya Ardhi wananchi wanoishi ndani ya eneo hilo kwa kuminya huduma za msingi (maji, afya, elimu na barabara), kuzuia shughuli za kujipatia chakula (kilimo) na malisho ya wanyama wao kinyume na sheria za ardhi ili kutoa shinikizo la kuwahamisha kwa ajili ya kupisha Kampuni za uwindaji na shughuli za utalii.

Huku ikiendelea na zoezi za kuwaondoa na mpango wa kuwahamisha bila kuwashirikisha na kupata ridhaa zao (free, prior, informed consent).

Mwaka jana (2022) tulionyesha wazi matatizo yaliyowakumba wananchi (wafugaji) katika eneo hili ikijumuisha mateso, manyanyaso, ukandamizaji, udhalilishaji na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vilivyosababishwa na matukio ya operesheni za hivi karibuni (2021, 2022).

Vitendo hivyo vikiwemo kubomolewa au kuchomewa moto makaazi, vitisho, kukamatwa na kubambikiwa kesi (wananchi zaidi ya 200 walipelekwa vituo vya polisi na wengine kushikiliwa zaidi ya siku 60). Vilevile, tulionyesha changamoto za sheria mbalimbali zinazoongoza eneo hilo zinazoipa Mamlaka ya Ngorongoro (NCA) mamlaka makubwa yanayoifanya kuwa nchi ndani ya nchi, kinyume na sheria za nchi.

Ingawa Serikali imetengeneza mwelekeo wa kihabari kwamba kuna wananchi wamejiandikisha kutaka kuhama kwa hiari yao lakini taarifa halisi zinaonyesha shinikizo. Mosi, barua ya Umoja wa Mataifa kwenda kwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania imethibitisha madai yetu na wadau wengine kuhusu hali inayowakumba wananchi wanaoishi eneo la Loliondo na Ngorongoro. Barua hiyo imeonyesha kuwa;

i. Mpango wa Serikali wa kupanua shughuli za uwindaji na utalii wa picha kwa Kampuni za uwindaji zitapelekea kuhamishwa kwa nguvu wafugaji 150,000 kutoka ardhi yao ya asili (Ngorongoro na Loliondo)

ii. Mpango umeandaliwa bila kushirikisha wanajamii na bila kupata kibali chao (free, prior and informed consent)

iii. Wamasai (wafugaji) hawashiriki kikamilifu katika usimamizi wa eneo la hifadhi la Ngorongoro.

iii. Licha ya kuwa vifungu vya sheria vya kulinda na kuendelea wanajamii ikiwemo sheria ya uhifadhi ya Ngorongoro 1975 haki zao zimekuwa zikisiginwa kila uchao ikiwemo kupunguzwa eneo la kulisha mifugo, kilimo na kunywesha mifugo.

iv. Kusitishwa kwa huduma za msingi kama vile elimu, afya na Miundombinu ya Barabara.

v. Jamii ya wamasai na viongozi wao kuwa waathirika wa matumizi ya nguvu, kuongezeka kwa kauli za kibaguzi katika vyombo vya habari na mamlaka za Serikali.

vi. Vitisho, kukamatwa, kufunguliwa kesi na udhalilishaji wa watu

Pili, kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anasema ni jumla ya watu 2,125 sawa na Asilimia 1.93 tu na Mifugo 11,490 Sawa na asilimia 1.53 tu ndio waliohamishwa kwenda Msomera Wilaya ya Handeni. Ripoti hii ukiitazama, Mradi wenye fedha nyingi kiasi hiki wananchi wangekuwa wanapenda kuhama au wameridhia kungekuwa na kundi kubwa la watu ambalo Serikali isingeweza kumudu. Hivyo ni wazi kuwa wananchi wamegomea Mpango huo na haukuwa wa hiyari.

Katika hotuba yake Waziri wa Utalii na maliasili Mhe. Mohamed Mchengerwa amelieleza bunge kuwa Serikali haitositisha operesheni hiyo na hakuna kitachowarudisha nyuma. Ni jambo la aibu sana kuona Serikali inajali tu fedha zinazoletwa na utalii na shughuli za uwindaji unaofanywa na kampuni za kigeni kwa gharama za maisha na hatima ya wananchi wake.

ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Serikali kutambua na kuendeleza uhifadhi wa kijamii kwa malengo ya kulinda rasilimali asili pamoja na haki za ardhi ya wafugaji. Tunasisitiza kuwa Serikali iachane na operesheni ya kuwaondoa wananchi kwenye eneo hili kama ilivyopendekezwa ripoti ya Ardhi Mseto.

Pili, tunaitaka Serikali kurejesha haki za ardhi na umiliki wa uhakika wa ardhi kwa wananchi wa eneo hili ili kurejesha haki ya kufanya shughuli za ufugaji na kilimo cha chakula kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

Tatu, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ivunjwe na badala yake iundwe Kampuni yenye kumilikiwa kwa ubia kati ya wananchi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na Serikali. Wananchi wamiliki 51% na Serikali 49%. Uendeshaji wa kampuni hii uwe mikononi mwa Serikali.

2. Kadhia ya Tembo na Wanyama waharibifu katika mashamba ya wananchi.
Kumekuwepo na malalamiko ya wananchi wanaoishi pembezoni au maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyama au mbuga za wanyama kama vile Selous, Nyasaka, Mkomazi, Biharamulo kuvamiwa au kukabiliwa na changamoto ya wanyama wakali au waharibifu (Tembo). Kuibuka kwa wimbi kubwa la matukio ya uvamizi wa Wanyama hawa limeambatana na athari kubwa kwa wananchi hao ikiwemo uharibifu wa mali zao (mashamba, mazao, mifugo na makazi), kujeruhiwa au vifo na kukamatwa na Serikali watu wanaoamua kujihami na kulinda mali zao kwa kuwaua wanyama hao.

Idadi ya matukio na vijiji vinavyovamiwa na tembo inazidi kuongezeka kila uchao. Kwa utafiti tulioufanya mathalani eneo la Nachingwea kumetokea vifo 5 kati ya mwezi Machi-April 2023 katika vijiji 8 vya wilaya hiyo (Namapwia 3, Ngunichile 1, Namikango 1, Lionja aAna B), vijiji zaidi ya 5 mazao yao yameharibiwa sana. Itakumbukwa mwaka jana tulisikia Nachingwea kuna hatari ya njaa kutokana na mashamba yao kushambuliwa na Tembo. Aidha, wilaya za, Tunduru, Namtumbo Mkoa wa Ruvuma nazo zinaonyesha idadi kubwa ya matukio ya uvamizi wa tembo na athari zake kwa wananchi.

Hatua alizoeleza Waziri katika kukabiliana na changamoto hizi zikiwemo kujenga vituo 16 vya askari wa Wanyama pori kwenye maeneo ya hatari zaidi, kuongeza doria na kuajiri askari ni hatua nzuri lakini zimefanywa kwenye ufanisi mdogo kiasi cha kutoweza kukabiliana tatizo hili kwa haraka.

Aidha, wananchi wanalalamikia viwango vidogo vya fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na wanyama hao kama vile tembo. Viwango vya sasa kwa mujibu wa kanuni ni shilingi 200,000 hutolewa kwa aliyepata majeraha yasiyo ya kudumu na shilingi 500,000 kwa majeraha au kilema cha kudumu huku wakitoa kifuta jasho cha shilingi 100,000 kwa ekari kwa wale ambao mazao yao yameharibiwa na wanyama pori na shilingi 1,000,000 kwa mwananchi aliyeuwawa na wanyama.

ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali kuongeza idadi ya askari kwenye vijiji vyote vinavyokabiliwa na changamoto hizi. Idadi ya Askari 146 pekee walioajiriwa na Serikali ni ndogo sana. Ni wakati Sasa kuishinikiza Serikali kuchukua hatua za kunusuru athari zaidi.

Pili, Serikali ifanye utafiti wa idadi ya Tembo na tabia zao ili kama imeongezeka kuanza kuvunwa ili kupunguza uvamizi wa mara kwa mara. Tatu, Serikali isimamie ipasavyo matumizi bora ya ardhi hususani kati ya shughuli za kilimo na ufugaji ili kudhibiti wafugaji kwenda maeneo ya makazi ya Wanyama pori.

Pia, tunaitaka Serikali itoe fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na wanyama hao kwa kuangalia hali halisi ya maisha kwa mujibu wa Sheria wakati hatua zingine zikiendelea.

3. Utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya wananchi na Mamlaka za uhifadhi.
Tatizo la migogoro ya Mipaka kati ya vijiji na mamlaka ya hifadhi imekuwa na athari kubwa kwa wananchi ikiwepo kunyang’anywa mifugo, mazao, vitisho, vipigo na vifo vya watu (wananchi na askari wa uhifadhi). Kwa mujibu wa taarifa za Serikali Vijiji vinavyoainishwa kuwepo katika migogoro hiyo ni vijiji 975 ambavyo vinapakana na mamlaka za hifadhi kuanzia, hifadhi za taifa, hifadhi ya Ngorongoro, mapori tengefu na mapori ya akiba.

Pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta kushughulikia migogoro hii na kurasimisha vijiji hivyo lakini kasi ya utatuzi ni ndogo sana na kwa maeneo mengine njia za utatuzi hazifanyi kazi kwa ufanisi na hata kupelekea mgogoro mpya au kuendeleza mgogoro. Mifano ipo mingi maeneo yaliyofikiwa na Kamati ya Mawaziri kutomaliza migogoro kama vile eneo la Mbarali ambalo bado unaendelea kuchukua sura mpya kutokana na uamuzi wa Serikali kutoleta ufanisi.

Katika hotuba ya bajeti Waziri amesema Serikali imefanikiwa kutatua migogoro kwenye vijiji 249 tu kati ya vijiji 975 tangu 2016. Ni wazi kuwa kuchelewa kukamilika kwa zoezi hili na kufanywa bila mafanikio kunasababisha usumbufu kwa wanavijiji kutokana na kuendelea kuibuka kwa migogoro ya ardhi na mamlaka za uhifadhi. Tumeshuhudia vitendo vya kinyama kama vile kuuawa kwa wananchi, kuteswa, kuwekwa kuzuizini na kuumizwa, kudhalilishwa, kuzuiwa kwa shughuli za uzalishaji kama vile kilimo, ufugaji au kuokota kuni unaofanywa na maafisa/askari wa hifadhi na wakala wa misitu (TFS).

Hivi karibuni, migogoro iliyojitokeza baina ya wanavijiji vinavyozunguka hifadhi ya Sayaka, Magu, Mwanza dhidi ya maafisa wa mamlaka ya misitu (TFS) kutokana na mamlaka kusogeza vigingi vya mipaka ya hifadhi kwa wananchi. Mgogoro wa hifadhi ya Selous na vijiji vya Kilwa (Mtepera, Zingakibaoni, Ngarambe) nayo kutokana na mipaka. Pia, migogoro ya mipaka kwenye vijiji 45 vinavyopatikana kwenye wilaya za Simanjiro, Karatu, Kondoa, Bariadi na Bunda.

Uhalisia unaonyesha kuwa migogoro hii inatokana na kukosekana kwa mifumo imara inayolinda haki na maslahi mapana ya wazalishaji wadogo (wakulima na wafugaji) katika ardhi. Mfano, mfumo wa umilikaji wa ardhi, changamoto za upatikanaji wa rasilimali za maji na malisho zinazoathiri wazalishaji wadogo.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iongeze kasi ya kurasimisha Mipaka ya vijiji hivyo ili kumaliza migogoro hiyo. Pia, hatua zichukuliwe kwa watendaji, askari na watumishi wa mamlaka wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu katika kutatua migogoro. Tunatoa wito kwa Serikali kuimarisha mifumo itakayolinda haki na maslahi mapana ya wazalishaji wadogo (wakulima na wafugaji) katika ardhi.

4. Kukosekana kwa Mkakati wa kuendeleza na kutangaza utalii kanda ya kusini.
Sekta ya utalii ina nafasi kubwa sana katika kukuza pato la taifa, kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii inaanza kwenye kutengeneza ajira, kuingiza fedha za kigeni na kuuza bidhaa za kijamii kutokana na watalii.
Katika nchini yetu, pamoja na kuwa na vivutio vingi vya utalii ukanda wa kusini bado haujaendelezwa vya kutosha ili kunufaika na sekta hii ya utalii.

Mara zote Serikali inaandaa mikakati ya kusimamia na kuendeleza Utalii kanda ya kusini (Ruvuma, Iringa, Lindi, Mtwara) lakini mikakati hiyo haijatafsiriwi kwenye vitendo. Ni wazi kuwa Serikali kupitia Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) imeitenga mikoa hiyo kwa vile katika maonesho ya Utalii ya Nje za nchi, TTB imekuwa haivitangazi vivutio vilivyoko ukanda wa Kusini na nyada za juu kusini.

Kwa Mkoa wa Lindi uwepo wa magofu ya kale Kilwa kisiwani na Songo Mnara ambayo yameorodheshwa kwenye urithi wa dunia lakini bado hayajatangazwa vya kutosha kuvutia watalii wengi zaidi. Mbuga ya Selous iliyoenea mikoa ya Pwani, Iringa, Lindi na Ruvuma nayo haijawekewa Miundombinu ya kutosha ili kuimarisha utalii wa kutazama wanayama kama ilivyo kwa Serengeti, Mikumi na Ngorongoro; Aidha, Iringa ni moja ya mikoa yenye vivutio mbalimbali vya kitalii ikiwa pamoja na mbuga za wanyama pori za Ruaha na Udzungwa.

Mkoa pia una vivutio vya kihistoria na kitamaduni kama vile eneo la mali kale la Isimila (Isimila Stone Age) na makumbusho ya Mkwawa ya Kalenga
Mradi wa kusimamia na kuendeleza Utalii nyanda za juu kusini (REGROW) hautengewi fedha za kutosha kuhakikisha azma ya kuyaendeleza maeneo haya inafanikiwa kwa ufanisi mkubwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Shilingi 30,495,601,578 ziliidhinishwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za mradi. Hadi mwezi Aprili 2021, Shilingi 5,776,178,445 zimetolewa na kutumika sawa na asilimia 18.9.

Taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2022/23 ni Shilingi bilioni 4.1 tu ndio ilipatikana kwa kipindi cha mwaka mmoja. Mwenendo wa upatikanaji wa fedha unaathiriwa na utegemezi kutoka nje ambao ni zaidi ya asilimia 95.

ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali, mradi wa kusimamia na kuendeleza Utalii ujikite zaidi kwenye kutengeneza Miundombinu ya usafiri, Barabara na viwanja vya ndege, kuzalisha matangazo ya video/filamu fupi fupi na mitandao ya kijamii. Pia, Serikali ihakikishe inatoa kwa wakati fedha zote zilizotengwa kwa ajili kuendeleza na kutangaza vivutio vilivyopo kusini.

5. Kurejeshwa kwa Masalia ya Mjusi mkubwa wa Danosaria nchini.
Katika uchambuzi wa bajeti wa mwaka jana tulielezea madai ya muda mrefu ya Watanzania (wananchi wa kawaida na wanasiasa) kutaka masalia ya Mjusi Mkubwa (Danosaria) kurejeshwa nchini. Na kutaka kuona kwa namna gani taifa linaweza kunufaika na urithi huu wa lakini bado hakuna juhudi zilizofanywa na Serikali kutaka kumrejesha. Sehemu ya masalia hayo kwa kipindi cha sasa ni mjusi mkubwa anayeoneshwa katika Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Naturkunde Berlin, Ujerumani. Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya mjusi huyo ni masalia halisi kutoka Tendaguru Tanzania na asilimia 40 ni malighafi za kibunifu kwa ajili ya kupata umbo halisi la mjusi.

Katika hotuba ya bajeti kwa mwaka 2021/22 Serikali iliahidi kuwa itaanzisha mazungumzo kupitia Makumbusho ya Taifa na Makumbusho ya Naturkunde ya jiji la Berlin, Ujerumani, ili kuweka mazingira wezeshi ya kuanzisha mjadala kati ya nchi ya Ujerumani na Tanzania ili kurejesha au kunufaika na masalio hayo. Lakini katika hotuba ya mwaka huu Serikali ipo kimya hadi sasa ni wazi hakuna hatua za uhakika zilizochukuliwa.

Serikali inataja hatua za kujenga masanamu ya mijusi kama njia kutangaza na kuvutia utalii, hii ni dhahaka sana kwa taifa letu. Sanamu linaweza kuacha kumbukumbu tu lakini haliwezi kuwa kivutio kwa watu. Wakati Ujerumani inanufaika na Mjusi halisi, sisi tunaitaka kujitangaza kwa kuweka masamu ya mijusi.

ACT Wazalendo tunarudia kuitaka Serikali kuweka wazi hatua zilizofikiwa katika kumrejesha mjusi huyo na namna ambayo tunaweza kupata gawio la manufaa ya kipindi chote ambacho Ujerumani imekuwa ikinufaika kutokana na mjusi huyu. Aidha, tunaitaka Serikali kushughulikia suala hili kwa kutumia mwakilishi wetu (Balozi), badala ya kutumia idara ya Makumbusho.

6. Udhibiti wa janga la moto katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro
Matukio ya ajali za moto katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro imekuwa ikizua hofu ya kupoteza watalii, hali ya afya ya wananchi wanaozunguka eneo hilo na Serikali kwa ujumla. Tumeshuhudia ndani ya miaka mitatu kutokea ajali ya moto mara mbili; Ulitokea Novemba 11, 2020 na Oktoba 21, 2022.
Serikali kupitia Mamlaka ya hifadhi ya Taifa (TANAPA) ina wajibu wa kudhibiti matukio ya moto kwenye maeneo ya hifadhi. Isichukulie kwa mzaha matukio haya ya moto ya mara kwa mara kwenye Mlima Kilimanjaro. Viongozi wabuni njia za kudhibiti majanga ya moto yasitokee na si kuanza kuhangaika wakati majanga yanapotokea kwani madhara ni makubwa.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ichukue hatua za tahadhari ili kudhibiti majanga ya moto katika Mlima Kilimanjaro usiwe unatokea hususani katika kipindi cha kiangazi. Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) wawe wanafanya uchomaji wa mapema (Earlier buning). Huu ni uchomaji wa makusudi ambao unafanyika kabla nyasi hazijakauka sana. Uchomaji huu unaandaliwa mipaka ya kuchoma kwa kuandaa njia ya kuzuia moto (fire block).


Imetolewa na;
Ndg. Juliana Donald Mwakan’gwali
Twitter: @Julianamwakan’gali
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii
ACT Wazalendo.
04 Juni 2023.
 
Back
Top Bottom