The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 746
- 2,102
Mwanzilishi wa WikiLeaks Julian Assange
Mwanzilishi wa WikiLeaks Julian Assange kesho Jumatano (26 Juni, 2024) anatarajiwa kukiri kosa la kuvunja sheria za ujasusi za Marekani, katika makubaliano yatakayomaliza kifungo chake nchini Uingereza na kumruhusu kurudi nyumbani Australia.
Assange, mwenye umri wa miaka 52, amekubali kukiri kosa moja la jinai la kula njama ya kupata na kufichua hati za siri za ulinzi wa taifa za Marekani.
Anatarajiwa kuhukumiwa kifungo cha miezi 62 ambacho tayari ametumikia katika kikao cha kusikilizwa huko Saipan saa 3 asubuhi kwa saa za huko (saa 2300 GMT Jumanne). Kisiwa hicho kilichopo Pasifiki kilichaguliwa kutokana na Assange kukataa kusafiri hadi Marekani na badala yake kifanyike Saipan ambapo ni karibu na Australia.
Assange aliondoka gerezani Belmarsh nchini Uingereza Jumatatu kabla ya kupewa dhamana na Mahakama Kuu ya Uingereza na kupanda ndege mchana huo, WikiLeaks ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye jukwaa la kijamii la X.
Serikali ya Australia, inayoongozwa na Waziri Mkuu Anthony Albanese, imekuwa ikishinikiza kuachiliwa kwa Assange lakini ilikataa kutoa maoni juu ya kesi hiyo kwani bado inaendelea.
HISTORIA YA MASHTAKA
WikiLeaks mwaka 2010 ilitoa mamia ya maelfu ya hati za siri za kijeshi za Marekani kuhusu vita vya Washington huko Afghanistan na Iraq - uvujaji mkubwa zaidi wa aina yake katika historia ya kijeshi ya Marekani - pamoja na nyaraka nyingi za kidiplomasia.
Assange alishtakiwa wakati wa utawala wa Rais wa zamani Donald Trump kwa kuachilia kwa wingi hati za siri za Marekani, ambazo zilivuja na Chelsea Manning, mchambuzi wa zamani wa kijasusi wa jeshi la Marekani ambaye pia alishtakiwa chini ya Sheria ya Ujasusi.
Hazina hiyo ya zaidi ya hati 700,000 ilijumuisha nyaraka za kidiplomasia na akaunti za vita kama vile video ya 2007 ya helikopta ya Marekani ya Apache ikifyatua risasi kwa washukiwa waasi huko Iraq, na kuua watu kadhaa wakiwemo wafanyakazi wawili wa habari wa Reuters. Video hiyo ilitolewa mwaka 2010.
Mashtaka dhidi ya Assange yalizua ghadhabu miongoni mwa wafuasi wake wengi duniani ambao wamekuwa wakisema kwa muda mrefu kuwa Assange kama mchapishaji wa WikiLeaks hapaswi kushitakiwa kwa mashtaka yanayotumika kawaida dhidi ya wafanyakazi wa serikali ya shirikisho wanaoiba au kutoa taarifa.
Watetezi wengi wa uhuru wa vyombo vya habari wamekuwa wakisema kwamba kumshitaki Assange kwa jinai ni tishio kwa uhuru wa kujieleza.
"Makubaliano ya kukiri hatia yatazuia hali mbaya zaidi kwa uhuru wa vyombo vya habari, lakini makubaliano haya yanamaanisha kuwa Assange atakuwa ametumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa shughuli ambazo waandishi wa habari wanashughulikia kila siku," alisema Jameel Jaffer, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya uhuru wa vyombo vya habari ya Knight First Amendment Institute katika Chuo Kikuu cha Columbia.
SAFARI NDEFU
Assange alikamatwa kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mwaka 2010 kwa hati ya kukamatwa ya Ulaya baada ya mamlaka za Sweden kusema wanataka kumhoji kuhusu madai ya uhalifu wa kijinsia ambayo baadaye yaliondolewa. Alikimbilia kwenye ubalozi wa Ecuador, ambako alikaa kwa miaka saba, ili kuepuka kusafirishwa kwenda Sweden.
Alivutwa nje ya ubalozi huo mwaka 2019 na kufungwa kwa kukwepa dhamana. Amekuwa katika gereza la usalama wa juu la Belmarsh huko London tangu wakati huo, ambako kwa karibu miaka mitano amekuwa akipigania kusafirishwa kwenda Marekani.
Miaka hiyo mitano ya kifungo ni sawa na adhabu iliyotolewa kwa Reality Winner, mwanajeshi wa zamani wa Anga na mkandarasi wa kijasusi, ambaye alihukumiwa miezi 63 baada ya kuondoa nyaraka za siri na kuzipeleka kwa chombo cha habari.
Akiwa Belmarsh Assange alimuoa mpenzi wake Stella ambaye alizaa naye watoto wawili alipokuwa akijificha katika ubalozi wa Ecuador.
PIA, SOMA:
- Mwanzilishi wa Wikileaks Julian Assange aachiwa huru kutoka gereza la Belmarsh nchini Uingereza ambako amekaa kwa miaka 12
- Je, Julian Assange ni Shujaa au Msaliti?
- Wikileaks: Julian Assange aruhusiwa kufunga ndoa jela
- Mahakama ya Uingereza yahukumu Assange anaweza kurejeshwa nchini Marekani
- Snowden amuomba Trump amuachie Julian Assange kizuizini nchini United Kingdom kabla hajahukumiwa
- Julian Assange: Trump 'offered pardon for Russia denial'