nivoj.sued
JF-Expert Member
- Jul 14, 2009
- 221
- 190
Wadau wa elimu inayotolewa kupitia Vyuo vya Maafisa Tabibu nchini, yaani Clinical Training Officers (COTCs), wamemtaka Rais Magufuli, kuingilia kati kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ili kuhakikisha yafuatayo yanatekelezwa mara moja:
1. Vyuo vya COTCs vianze mara moja kuandaa prospectus zake ili wanafunzi wasiwe wanasoma bila kujua miongozo muhimu ya kitaaluma inayowahusu.
2. Wizara ifute mara moja utaratibu wa kuendesha mitihani ya COTCs, ambapo kwa sasa uko centralised, ukiwa chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Mafunzo. Utaratibu huu ni onevu kwa wanafunzi, na unawaburuza wakuu wa vyuo. Hakuna uwianisho wa ratiba za vyuo na ratiba za mitihani inayoendeshwa na Wizara. Waathirika ni wanafunzi.
3. Mitaala husika itamke bayana kwamba zitakuwepo wiki mbili maalum kwa ajili ya mitihani ya marudio vyuoni. Kwa sasa, ratiba za mitihani ya marudio zinakwenda sambamba na ratiba za masomo ya kawaida. Hivyo, wanafunzi wenye mitihani ya marudio wanalazimika kuacha masomo yanayoendelea ili wakafanya mitihani ya marudio. Wakimaliza, tayari wenzao wanakuwa wamekwisha waacha mabli. Katika mazingira haya, wengi watapoteza masomo yao hivi karibuni, maana hakuna uhakika kwamba muda wa kutosha kufanya masomo yote utapatikana.
4. Baadhi ya walimu wa COTCs hawana mafunzo yoyote ya ualimu. Kwa hiyo, inawawia vigumu kutengeneza utaratibu mwafaka wa ufundishaji ili kuwasaidia wanafunzi kukabiliana na shinikizo la muda. Kunahitajika "in-service training on classroom process." Vinginevyo, COTCs zitageuka kuwa tembo mweupe.
5. Usimamizi wa COTCs uimarishwe. Kwa sasa kitengo cha udhibiti cha NACTE (Compliance unit) kinashindwa kufanya kazi kwa kuwa, vitendea kazi muhimu vinapaswa kuandaliwa na Wizara ya Afya. Kwa mfano Wizara inawajibika kuandaa Kanuni za Mitihani, na Mitaala. NACTE wanatoa mwongozo, wanasubiri Mitaala na Kanuni za Mitihani ili waanze compliance audit. Vitu hivi vsipokuja ndani ya muda NACTE hawana la kufanya. Sababu ni moja: NACTE iko chini ya Wizara ya Elimu, wakati COTCs ziko chini ya Wizara ya Afya. Kwa maoni yangu, suluhishi ni kuanzishwa kwa "EWURA" ya Elimu, yaani "Tanzania Academic Qualifications Regulatory Authority (TAQRA).
6. Kanuni za mitihani katika vyuo vya COTCs ziandaliwe haraka na kusambazwa kwa wadau. Kanuni hizi sio nyaraka za siri, kama ambavyo wahusika Wizarani wanavyojaribu kuonyesha.
7. Mitaala kwa ajili ya vyuo vya COTCs iwekwe wazi na kusambazwa kwa wadau bila gharama za malipo kama NACTE wanavyofanya sasa hivi. Katika ulimwengu huu wa E-governance, mitaala sio nyaraka zinazopaswa kufichwa kabatini ili kuwalazimisha wadau waje kuzinunua.
8. Kwa uzorotefu ulioonekana, katika ngazi ya vyuo na Wizara, wakati wa kushughulikia mgogoro wa kitaaluma KIbaha na Mtwara, ni maoni ya mwandishi kwamba:
(a) Mkurugenzi wa Mafunzo, Otillia Gowelle, apangiwe kazi nyingine.
(b) Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, apangiwe kazi nyingine.
(c) Mkuu wa Chuo cha COTC Mtwara na Afisa Taaluma wake wapangiwe majukumu mengine.
(d) Mkuu wa Chuo cha COTC Kibaha na Afisa Taaluma wake wapangiwe majukumu mengine.
Mapendekezo haya, yanatokana na sintofahamu inayosimuliwa kwa kirefu hapa chini. Soma kama unao muda wa kutosha.
Tangu miaka ya 1930, serikali ya Tanzania iliweka utaratibu wa kupunguza upungufu wa madaktari bingwa nchini. Kwa mujibu wa utaratibu huu, kuna ngazi tatu za wataalam wa huduma za afya.
Ngazi hizo ni Clinical Assistant (CA), Clinical Officer (CO) na Assistant Medical Officer (AMO). Takwimu za kiserikali za mwaka 14 zinaonyesha kwamba Tanzania kuna Clinical Assistants 1,216 Clinical Officers 6,164 na Assistant Medical Officers 1,737. Wataalam hawa wanaandaliwa kupitia Vyuo vya Maafisa Tabibu, au Clinical Training Officers (COTCs) kwa kimombo. Miongoni mwa COTCs zilizopo nchini ni pamoja na hizi:
Kibaha COTC, Kilosa COTC, Lindi COTC, Mafinga COTC, Mtwara COTC, Mbeya Assistant Medical Officers Training Centre (AMOTC), Kigoma Clinical Assistant Training Centre (CATC), Masasi CATC, Maswa CATC, Musoma CATC, Songea CATC, Sumbawanga CATC, Mpanda CATC, Nzega Nurses Training Centre (NTC), Nachingwea NTC, na Kibondo NTC.
Kuna vyuo kama hivi chini ya Wizara nyingine pia. Kwa mfano, Chuo cha Usafirishaji (NIIT) kiko chini ya Wizara ya Usafiri, Mawasiliano na Uchukuzi; wakati chuo cha Fedha (IFM) kiko chini ya Wizara ya Fedha.
Hapa ninataka kuongelea tatizo la kiuuendeshaji katika vyuo vya Maafisa Tabibu (COTCs). Nimealazimika kufanya hivyo kufuatia matukio mawili yanayofanana, moja likiwa limetokea KIbaha COTC, na jingine Mtwara COTC.
Hivi karibuni, Wanafunzi sita wanaosomea Chuo cha Maafisa Tabibu Kibaha wameamriwa na Wizara ya Afya kurudia mwaka katika mazingira tata. Wanafunzi hao ni: Husin Kabaju, na Nicas Cosmas, Paul Yohana, Jonathan Charles, Iilene Deogratias, na Anna Hhayri.
Mbali na wanafunzi hawa sita wa Kibaha COTC kuna wanafunzi kumi na nne wanaosomea Chuo cha Maafisa Tabibu Mtwara ambao wamekumbwa na mkasa ule ule. Hawa ni: Ramadhan Said, 8. Abel Frank, Rehema Nkya, Adamson Adam, Rajab M. Rajab, Esther Elisha, Shaaban Malinda, Ng'oha KIngamkono, Shabani Mhina, Wilson Sylvester, Hamis Juma, Deusdedit Galikano, Waiswa Peter, na Abubakar Musa.
Kwa mujibu wa barua ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo, Dk. Otilia F. Gowelle, yenye kumbukumbu namba JB.87/327/01/121, iliyoandikwa tarehe 06 Juni 2016, maagizo yafuatayo yametolewa kwa wanafunzi na vyuo husika:
“Ombi la wanafunzi hao haliwezi kukubalika kwa sababu hawakuweza kusoma masomo ya muhula wa kwanza wa mwaka wa tatu na kufanya mitihani ya muhula huu kulingana na mtaala unavyoelekeza.
“Hivyo, [wanafunzi hawa] wanatakiwa [kwenda nyumbani na baadaye] kurudi vyuoni ifikapo mwezi Septemba-Oktoba 2016 muhula wa masomo kwa mwaka wa tatu utakapoanza.”
Kadhalika, kupitia barua hii, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Dk. Gowelle, alitoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa baadhi ya vyuo vya Wizara kuwawaruhusu wanafunzi waliotoka Mtwara kwenye mitihani ya marudio kuendelee na masomo ya mwaka wa tatu.
Kuhusu jambo hili, Dk. Gowelle, alisema yafuatayo: “Vyuo vilivyoweza” [kuwaruhusu wanafunzi husika] “kuendelea na masomo muhula wa pili wa mwaka wa tatu” [vitakuwa] “ni vile ambavyo walikuwa wakisoma na kufanya mitihani, sambamba na kurudia mitihani ya marudio.”
Baada ya kupokea majibu ya Wizara, wanafunzi wa Chuo cha Kibaha walijibu kupitia barua yao ya tarehe 15 Juni 2016. Barua nyingine yenye maudhui sawa na barua hii iliandikwa kwenda kwa Mkuu wa Chuo cha Kibaha pia. Kupitia barua zao mbili, wanafunzi hawa walitoa ufafanuzi ufuatao kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara:
“Katika semester ya kwanza tulikuwa tumekwisha soma ‘module’ zote. Pia tulikuwa tumekwisha anza kufanya mitihani ya CAT-I. Tulibakiza CAT-II kwa baadhi ya ‘module.’ Hivyo, kwanza, tunaomba kuruhusiwa kufanya mitihani hii ya ndani ya semester ya kwanza.
“Tuko tayari kujiandaa kwa ajili ya mitihani ya semester ya kwanza na kufanya mitihani hiyo ndani ya mwezi wa saba hadi mwezi wa nane. Tukifanikiwa katika hili tutakwenda nyumbani, na tutakuwa katika nafasi ya kurudi chuoni mwezi wa kumi kwa ajili ya kujiandaa kwa ajili ya mitihani ya NTA Level 6, kukamilisha field, na rotation za wodini.
“Hivyo, tunaomba kuruhusiwa kufanya mtihani wa kumaliza NTA Level 6 mwezi wa pili mwaka 2017 kama ‘first sitting’ wakati wenzetu watakapokuwa wanafanya mitihani ya marudio.”
Kwa ajili ya kumthibitishia Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara, Dk. Gowelle, kwamba wao hawana tofauti na “vyuo vilivyoweza” kuwaruhusu wanafunzi husika “kuendelea na masomo muhula wa pili wa mwaka wa tatu,” waliambatanisha fomu zenye sahihi za mahudhurio yao ya darasani pamoja na fomu zenye sahihi za mahudhurio ya walimu darasani.
Kwa njia hii wanafunzi wakathibitishia Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara, Dk. Gowelle, kuwa hata chuoni kwao Kibaha “walikuwa wakisoma na kufanya mitihani, sambamba na kurudia mitihani ya marudio” kama walivyokuwa wakifanya wanafunzi wa vyuo vingine walioruhusiwa kuendelea na mwaka wa tatu.
Mpaka habari hii inaandikwa Wizara haijasema lolote kuhusu maombi ya wanafunzi hawa. Lakini, mwandishi amezipitia nakala za mitaala husika na fomu za mahudhurio ya wanafunzi na kujiridhisha kwamba, hakuna kifungu cha kikanuni kinachohalalisha maamuzi ya Wizara dhidi ya wanafunzi hawa. Mitaala husika imeambatanishwa hapa kwa faida ya wasomaji.
Nimetimiza wajibu wangu basi.