JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 667
- 1,075
Kustaafu hali ya mtu kujiondoa kwenye nafasi yake ya kazi au kutoka kwenye maisha ya kufanya kazi. Mtu anaweza pia kustaafu nusu kwa kupunguza masaa ya kazi au mzigo wa kazi. Kwa Tanzania umri wa lazima kustaafu ni miaka 60.
Ikiwa umeajiriwa basi ni wazi kuwa wewe ni mstaafu mtarajiwa, haijalishi kuwa utastaafu ndani ya miaka 10 au hata 20 ijayo ni vyema ukajipanga mapema jinsi ya kukabiliana na swala hilo.
Fanya yafuatayo ili kujitengenezea maisha salama yasiyo na msongo wa mawazo baada ya kustaafu.
Jiandae kisaikolojia
Kustaafu ni kipindi tofauti sana na kipindi ulichokuwa kwenye ajira. Kipindi hiki utakutana na mtindo mpya wa maisha tofauti na ule uliouzoea.
Andaa fikra zako kutambua kuwa wakati wa kufaidi mambo mbalimbali kama vile mshahara, ofisi, gari ya kampuni au hata nyumba ya taasisi kutokana na kazi yako sasa umefikia mwisho.
Weka akiba
Ikiwa kazi yako ndiyo uliyokuwa unaitegemea kama chanzo chako cha kipato, basi tafakari juu ya maisha bila kazi hiyo. Hakikisha unaweka akiba ya kutosha itakayokuwezesha kumudu matumizi yako mbalimbali baada ya kustaafu.
Unaweza kuweka akiba ya pesa au ya vitu ambavyo vinaweza kubadilishwa kuwa pesa kama vile ardhi, mifugo au majengo.
Lipa madeni
Kumbuka baada ya kustaafu kiwango chako cha kipato kitapungua; hivyo ni muhimu kulipa madeni kabla ya kustaafu ili usije ukahangaishwa na madeni wakati wa kustaafu.
Ondoa matumizi yasiyo ya lazima
Baada ya kustaafu kiwango chako cha mapato kitapungua, hivyo ni muhimu kutazama upya matumizi yako. Hakikisha matumizi yote ambayo hayana umuhimu au ulazima unayaepuka.
Tafuta chanzo kingine cha pesa
Kwa kuwa ulikuwa unategemea kazi yako kama chanzo chako cha kipato, ni muhimu sana kutafuta chanzo kingine cha kipato. Usisubiri hadi ustaafu ndipo upate chanzo kingine bali anza kutafuta chanzo hicho kabla hujastaafu ili ujijengee uzoefu.
Jiunge kwenye bima ya afya
Mara baada ya kustaafu utahitaji huduma za afya hasa kutokana na matatizo mbalimbali ya uzeeni. Unapokuwa umejiunga na bima ya afya utaweza kupata matibabu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.