Jifunze kitu katika simulizi hii

Mtuache

JF-Expert Member
Mar 12, 2021
256
656
Mwanaume mmoja alikuwa anampenda sana mkewe. Walikuwa wamejaaliwa watoto watatu waliokuwa wachangamfu na walifurahia sana maisha.

Yule mwanaume alikuwa analipwa mshahara wa wastani ambao usingetosha kukidhi kumpendezesha mkewe na kutunza familia. Kutokana na changamoto za kipato kidogo alijiongeza na kununua kagari kadogo aina ya IST(mtanisamehe wale wenye ndoto ya kununua IST) ili akaendeshe kama taxi jioni baada ya kutoka ofisini ili kuongeza kipato chake.

Kiukweli huu mpango ulienda vizuri na maisha yakawa bora na mazuri ijapokuwa alichoka sana na pia alikosa muda wa kutosha na familia yake. Hatahivyo, alijitia moyo kuwa haiwezekani mtu akala keki yake na bado ikawepo yaani, ukiwa na muda huna pesa na ukiwa na pesa huna muda ~ hivyo kila mtu huchagua anachotaka kuwa nacho.

Kila siku jioni jamaa alimpatia mkewe maokoto ya kwenye teksi kama shilingi 25,000 isipokuwa siku ya Jumapili aliyokuwa anaswali na kupumzika. Hii ilikuwa kwaajili ya gharama za chakula na matumizi ya nyumbani. Pale nyumbani palikuwa na amani furaha na utulivu. Kutokana na jinsi jamaa alivyompenda yule mkewe na watoto hakutaka kuuliza matumizi ya ile pesa. Kodi ya nyumba ada na matibabu alitoa kwenye mshahara wake wa ofisini.

Kwa ghafla siku moja mkewe akaugua na alihitajika kufanyiwa operesheni ya haraka. Na yule mwanaume hakuwa na tabia ya kujiwekea akiba. Alitaabika na kuhuzunika sana kwani dakitari alimweleza kuwa mkewe asipofanyiwa upasuaji kwa haraka ili kutatua tatizo linalomsibu atafariki dunia. Jamaa akajiongeza akamjulisha mkewe kuwa anaenda kuuza ile gari yake IST kwa haraka hata kama ni kwa hasara ili apate fedha za kumtibu mkewe. Basi mama watoto akamshukuru sana kwa jinsi anavyompenda na kumwambia hakika akipona atampenda zaidi na kuwajali watoto.

Yule mwanaume akarudi nyumbani akihuzunika kuwa hatakuwa na gari ya kutengenezea pesa jioni baada ya kazi hivyo atakosa pesa na uchumi wa familia yake na ubora wa maisha utashuka. Hatahivyo, akapiga moyo konde kuwa ni heri mkewe atibiwe kuliko kuwa na hiyo gari.

Wakati akitafuta madalali wanaoweza kuuza ile gari kwa haraka au wateja akawa anapiga magoti chumbani na kusali sana usiku kucha. Alikuwa anapiga magoti kwenye mfumbati wa kitanda na kuegemea godoro upande wa miguuni. Mara akagumdua kuwa ule upande wa miguuni mwa godoro kulikuwa kugumu kugumu na kuna uzito usiokuwa wa kawaida. Ndipo alipoamua kufunua shuka na kulitoa lile godoro.

Alipolichunguza lile godoro kuu kuu akakuta limekatwa na ndani yake kuna fedha iliyofichwa inayofikia shilingi milioni nne na nusu (TZS 4,500,000). Yule mwanaume akashangilia kwa furaha kuu huku akiwa amepigwa na butwaa. Mbona mwenzangu anajua ana kitita kinachotosha matibabu na kuzidi na hasemi yuko tayari niuze gari inayotusaidia kutengeneza pesa? Kwakweli hakupata majibu wala hakumuuliza wala kumueleza yeyote.

Akaichukua ile pesa akalipa matibabu ya mkewe yote, akanunua godoro kubwa jipya la Tanform 6×6 unene wa nchi sita na mashuka mapya. Akachukua lile godoro kuu kuu walilokuwa wanalilalia 'benki' ya mama watoto na kuwaita watoto wake wote watatu wakalilowanisha kwa mafuta ya taa na kisha wakalichoma moto kwa pamoja. Akawaambia nimenunua godoro jipya ili mama yenu akirudi alale mahali pasafi na pazuri.

Kwa neema za Mungu mama akatibiwa akapona vizuri na kurusiwa kurudi nyumbani. Aliporudi nyumbani akakuta mumewe amenunua godoro jipya na mashuka mapya mazuri sana. Akauliza, "Mume wangu godoro la zamani liko wapi?". Mumewe akamjibu, "Aisee lilikuwa na kunguni na wadudu wa aina nyingi, sikuwa naweza kulala usiku wakati hukuwepo. Tulilimwagia mafuta ya taa mimi na watoto tukalichoma moto". Watoto wakamwambia mama yao, "ni kweli mama! Tulilichoma moto lile godoro tukiwa na baba, ule moto ulikuwa kama wa jehanamu." Stori ikaishia hapo. Japokuwa mama alipona kabisa, huu ni mwaka wa sita bado ule mshono wa oparesheni huwa unauma 😂😂😂😂.
 
Wanawake wajinga hawakuwaga na ubinafsi sana. Chake ni chake ila cha mwanaume ni chao wote.
 
Ingawa umeelezea kama hadithi fulani! Ila kiukweli hawa ndugu zetu linapikuja suala la fedha, huwa wabinafsi sana.
 
Back
Top Bottom