SoC02 Jenga uchumi imara kwa maisha bora

Stories of Change - 2022 Competition

Mrema David

Member
Jul 19, 2022
5
3
Uchumi ni mali iliyopatikana kutokana na mali za nchi au watu. Vitu viwili vikubwa vinavyoweza kumsaidia mtu kufikia malengo yake kiuchumi na kimaisha ni Nidhamu binafsi na Nidhamu ya maisha; lakini huwezi kutengeneza nidhamu ya maisha bila ya kuwa na nidhamu binafsi.

Nidhamu binafsi ni uwezo wa kujitambua, na kujua unapaswa kufanya nini, wapi, kwa wakati gani na kwa madhumuni gani. Nidhamu ya maisha ni uwezo wa kutambua mazingira yanayokuzunguka na mahitaji yake, na kuishi kulingana na mahitaji hayo pasipo kupoteza thamani ya mtu binafsi au thamani ya mazingira.

UJASIRIAMALI NA FURSA​

Ujasiriamali ni hali ya uwekezaji mtaji katika biashara. Ujasiriamali ni kuona fursa na kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuitumia fursa hiyo.

Fursa ni nafasi inayoweza kutumika kwa ajili ya kutimiza lengo fulani kwa manufaa ya aliyeiona na kuitumia nafasi hiyo. Fursa inaweza ikajitokeza kama changamoto au katika hali nyinginezo.

Ili uweze kufanikiwa kiuchumi kuna wakati ni lazima uone matatizo ya jamii kama fursa ambazo unawajibika kuzitafutia ufumbuzi. Sio kila changamoto unapaswa kuichukia, au kuikimbia; Geuza changamoto kuwa fursa, wekeza katika fursa, jijengee uwezo wa kujiajiri.

MCHANGO WA MIRADI YA KIFAMILIA KATIKA UCHUMI WA DUNIA​

Mradi wa kifamilia ni kitu pekee kinachoweza kuondoa sonona ya kiuchumi. Ulichonacho nyumbani ni akili na maarifa ya wazazi na/au walezi ulionao juu ya miradi ya kifamilia. Kaa nao, uliza maswali, weka jitihada ya kushiriki. Kwa ufupi, huwezi kuwa mzalishaji mzuri mahali popote kama hukuwahi kuwa mzalishaji mzuri katika familia.

Hapa kuna mifano hai kama vile Bakhresa, na Mohamed Dewji; ambao mafanikio yao yamejengwa katika miradi ya familia na kurithishana ujuzi mbalimbali mpaka kuwa matajiri wakubwa na wenye ushawishi hapa Tanzania na nje ya Tanzania.

MCHANGO WA UTANDAWAZI KATIKA KUKUZA UCHUMI​

Utandawazi ni mfumo wa uhusiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari unayofanya mataifa kuwasiliana kwa urahisi.

Mahali Dunia ilipofikia huwezi kujitenga na mitandao. Mitandao inasaidia kielimu, kiimani, kibiashara, kupata habari, na kadhalika. Utandawazi kupitia mitandao ya kijamii umeunganisha watu tofauti na maudhui tofauti. Nidhamu binafsi inamsaidia mtu kuchuja na kuchanganua, na kufuata yale yenye tija kwa maisha ya sasa na ya baadaye.

Moja kati ya maudhui makubwa ya kiuchumi yaliyosababishwa na kukua na kuenea kwa utandawazi kwa sasa, ni biashara mitandaoni. Kwa sasa mtu mwenye biashara au mradi fulani anaweza kuwafikia watu wengi kwa kutangaza bidhaa zake kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Instagram, n.k, bila kusahau “programu” mbalimbali zinazotengenezwa kwa madhumuni ya kufanya biashara.

Kadhalika katika mitandao hiyo kuna fursa mbalimbali za ajira kwa ajili ya watu mbalimbali. Hii ni faida ya mabadiliko kutoka mifumo ya analojia kwenda mifumo ya kidijitali, ili kuendana na kasi ya Dunia ya sasa.

UWEKEZAJI​

Uwekezaji ni hali ya kutumia fedha au mali katika biashara kwa lengo la kuzalisha zaidi. Kila mtu ana eneo lake la shauku, eneo linalomfanya afurahi, eneo lake la ufanisi, na vitu anavyovichukia.

Mtu anapokuwa na shauku katika eneo fulani:

Anaweka bidii katika eneo hilo, anakuwa na uvumilivu katika eneo hilo, anakuwa na ubunifu katika eneo hilo.

Kila mtu ana eneo linalomfanya afurahie:

Usipofurahia unachofanya, inakuathiri kimwili na kiakili. Mtu asiyefurahia anachofanya mara nyingi huwa na visingizio, na madhara yake ni kukosa ubunifu na kutoweka muda mwingi katika eneo hilo.

Kila mtu ana eneo lake la ufanisi:

Mtu anakuwa na ufanisi na jambo fulani kutokana na kujifunza katika eneo hilo au kuwa na kipaji katika eneo hilo. Ufanisi huathiriwa na shauku; hivyo ili kufanikiwa, ni muhimu haya mawili kwenda pamoja.

Kila mtu ana vitu anavyovichukia:

Ukichukia uchafu, utafanya usafi; ukichukia umaskini, utafanya kila njia kukuza kipato chako. Unapochukia changamoto fulani, ni vema kuzigeuza kuwa fursa zitakazokusaidia kukua na kusaidia jamii inayokuzunguka.

MAARIFA SABA YANAYOKUPA UWEZO WA KUFANIKIWA KIUCHUMI​

Uwezo wa kupata wazo la uzalishaji:

Wazo ndilo linatengeneza fedha, kampuni, kiwanda, biashara, na kutoa mwelekeo au kuchora ramani ya kile kinachoonekana kwenye ndoto yako.

Uwezo wa kuzishinda changamoto zinazojitokeza:

Kwenye wazo na utekelezaji wa wazo, kuna changamoto mbalimbali mfano, kukatishwa tamaa, kupingwa, tena na watu wa karibu. Ni lazima mtu kusimama imara kupigania wazo lako na ndoto yako na kuhakikisha vinatimia.

Uwezo wa kuona fursa katika mazingira yaliyokuzunguka:

Ili mtu ufanikiwe kiuchumi lazima uwe na jicho makini kuona fursa ndani ya mazingira yako na kuzichangamkia. Katika kuchangamkia fursa hizo, hakikisha unazitengenezea uwiano mzuri na wazo lililopo kichwani mwako na utekelezaji wake.

Uwezo wa kutafuta fursa nje ya mazingira yako:

Mafanikio ya kiuchumi yanahitaji kupanua wigo wa mawazo. Fursa hazipo ndani pekee; simama, fungua mlango, toka nje, jenga nguvu yako na huko pia.

Uwezo wa kujua mahitaji ya kufanikisha ndoto yako:

Ukitaka kuwa mkulima ni muhimu kufahamu mahitaji ya kukupelekea kuanza kulima, mfano eneo la kufanyia kilimo (kiwanja/shamba), jembe na/au plau, mbegu, mfumo wa maji, n.k. Hivyo katika kufanikisha wazo, ni lazima kujua mahitaji ya kulitekeleza pamoja na upatikanaji wake

Uwezo wa kusimamia mipango yako na kujitathmini:

Mipango yoyote endelevu inahitaji nidhamu kubwa katika usimamizi, na tathmini. Wazo linahitaji tathmini, utekelezaji pia unahitaji tathmini. Unapoanzisha mradi na kukutana na changamoto au kukwama, ili kusonga mbele ni lazima kufanya tathmini kujua kwa nini umekwama. Tengeneza tathmini binafsi na watu waliokuzunguka, ili kujua namna nzuri ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika safari yako ya mafanikio.

Uwezo wa kuthubutu kufanya wakati wengine wanaogopa:

Ili kufanikiwa kiuchumi ni lazima kushinda hofu. Hofu ni adui wa maendeleo. Usiwe mwoga kuchukua hatua, kuanza, na kufanya maamuzi ya kimaendeleo.

MAKOSA YA KIUCHUMI YANAYOPASWA KUEPUKWA​

Kutaka kuhurumiwa na watu.

Kushindwa kugundua uthamani wa vitu ulivyonavyo, kikiwamo kipawa.

Kutafuta suluhisho la muda mfupi katika matatizo yanayohitaji suluhisho la muda mrefu.

Kukosa mkakati, umakini wa kutafakari, na kujitambua.

HITIMISHO​

Uimara katika uchumi unatusaidia katika mapambano dhidi ya “umaskini”. Uchumi bora unakuja pale ambapo watu wote watafuata kanuni muhimu za maisha ambazo ni kuweka bidii katika eneo linalomuingizia mtu kipato, pamoja na nidhamu. Kuwekeza katika mambo haya mawili kunapelekea kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla; hivyo kujenga Taifa imara na lenye uwezo wa kujitegemea katika hali mbalimbali.
 

Attachments

  • JENGA UCHUMI IMARA KWA MAISHA BORA-DAUDI G. MREMA.pdf
    140 KB · Views: 8

Similar Discussions

Back
Top Bottom