Je, mambo yako hayaendi? Tegua mtego!

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
26,965
65,052
JE MAMBO YAKO HAYAENDI? TEGUA MTEGO!

Anaandika, Robert Heriel
Yule Shahidi!

Mambo haya ni bure, wala sitakuchukulia chochote Kama faida. Nimeyaandika haya kama kumbukumbu Kwa hao watakaona yatawafaa, tena isihesabike maneno haya ni kifungo kwa yeyote bali yawe ufunguo Kwa hao waliofungwa, yawape Uhuru wa kweli wale wautafutao huo.
Tena Mimi Taikon, ndiye Shahidi wa maneno haya, nimeyapima na sasa ninayatolea hesabu kadiri ya nafasi niliyoipata.

Maishà yangu yamesimama, hayaendi, yameganda Kama barafu wakati wa kuanguka Kwa theluji.
Muda umenikimbia na kuniacha hata sijui iwapi njia yakupita, hata Ile njia niliyoipanga ningali Niko na muda imenipotea katika fikara zangu.

Ndoto zangu zimeniamsha usingizini, hata sikumbuki nilichokuwa nakiota.
Labda nitoke nje kuangalia Nyota za angani, nione vile zinavyong'aa labda nitazikumbuka zile ndoto nilizokuwa naziota ningali ni kijana Mdogo.

Lakini Nyota zipo juu Sana nami nipo chini Sana, Kama zilivyo mbali hizo Nyota ndivyo zilivyombali ndoto zangu. Tena Kama vile Nyota zisivyohesabika ndivyo na ndoto zangu nilizoziota zilivyonyingi hata nisweze kuzikumbuka.

Kama nisipolala basi sitaweza Kuota ndoto, na Kama nisipoamka basi hazitakuwa ndoto Bali zitakuwa ni kweli halisi. Basi ni akheri nisiamke ili ndoto zangu usingizini zibaki kuwa kweli, Kwa maana Aamkaye ndiye mwenye kujua alikuwa anaota lakini sio alalaye.

Hayo yote niliyaona katika maisha ya mwanadamu. Mwenye ndoto ndiye Yule alalaye, na asiyelala kamwe hawezi Kuota ndoto. Huo nao ni mtego katika maisha ya binadamu.

Tena wapo waotao wakiwa usingizini wasijue wanaota ndoto, nao wapo wanaoota na kujua wapo ndotoni. Hivyo ndivyo maisha ya binadamu yalivyo. Maisha ya binadamu yapo usingizini.

Wengine wanaishi wakidhani hawaishi hivyo huota ndoto ya maisha Fulani wasijue maisha wanayoyaishi muda ule ndio ndoto yenyewe. Kile walichokisahau walipokuwa usingizini, katika fikra zao ndicho wanachokiishi hivi leo. Hayo nayo ni sehemu ya maajabu ya Mungu.

Kama kila ndoto ilivyo na maana yake, ndivyo na kila Jambo Lina njia yake.
Na Kama kila ndoto ilivyo na mafumbo yake yanayohitaji kufumbuliwa ili maana ya ndoto hiyo iwe dhahiri ndivyo katika kila Jambo kwenye njia yake kuna mitego ambayo inatakiwa iteguliwe ili Mtu aweze kupita katika njia hiyo na kulifanikisha Jambo hilo. Hiyo nayo ni hekima kwao wenye ufahamu.

Katika njia kuna ramani, na ramani haimfai mtu bila ya msoma Ramani, Kama mtu hajui kusoma ramani basi ramani haimfai kitu. Wapo wanaopotea njia wangali wanayoramani, na wapo wanaopatia njia bila ya ramani. Huo nao ni mtego waliotegwa wanadamu ili wasipate maana halisi ya maisha, tena washindwe kubashiri.

Lakini asiye na ramani apatiapo njia basi yupo mwenyeji aliyemuonyesha hiyo njia.
Kwa maana mwenyeji hahitaji ramani kupatia njia isipokuwa Mgeni. Basi hivyo ndivyo maisha yalivyo.

Ikiwa mambo yako hayaendi basi Rudi kitandani ukalale ili katika ndoto mambo yako yaende. Kwa maana wote ambao mambo yao yanaenda basi hata katika ndoto mambo Yao huenda.
Lakini yupo mtu asemaye, tazama Mimi nikilala sioti ndoto yoyote, nalala Kama Mtu.
Ikiwa ni hivyo basi huo nao ni mtego unaopaswa kuteguliwa.

Lakini wapo waotao ndoto bila ya kuzikumbuka kutokana na ubongo wao kushindwa kurekodi matukio yaliyokuwa yanaendelea katika maisha ya nafsini ndio huko ndotoni. Mwili unapokuwa umechoka Sana kutokana na kazi nyingi Sana basi ubongo hushindwa kurekodi kumbukumbu za ndoto Kwa usahihi.

Lakini pia Matumizi ya madawa yanayoharibu ufanisi wa ubongo huweza kumfanya mtu asikumbuke Jambo lolote. Unywaji wa pombe kupitiliza, kulala chumba kisicho na hewa ya kutosha Hali iñayopelekea upumuaji kuwa duni na kufanya ubongo kupata hewa WA oksijeni isiyotosha huweza kumfanya mtu kupagawa usingizini.
Bado hujanipata??

Mambo yako yataenda ikiwa unanguvu ya kuyafanya yaende.
Ikiwa utakuwa na uwezo wa kuona na kuitegua mitego iliyokatika njia yako.
Ikiwa utakuwa na kumbukumbu za ndoto zako.

Nguvu unayo?
Unamacho ya kuona mitego katika njia yako?
Je unauwezo wa kufumbua mafumbo katika ndoto zako?

Ndoto ulizoziota ungali mdogo zimetimia! Ndoto za kuishi maisha mazuri, kuwa na Mke Mzuri na watoto wazuri!
Vipi sasa umekwama?
Uliziota ndoto zile ukiwa umelala, umeamka ukiwa mtu mzima ukaona kumbe ulikuwa usingizini. Au bado unataka ndoto zako ziwe kweli?

TEGUA MITEGO
1. Ikumbuke ndoto uliyoiota kisha fumbua mafumbo ya ndoto hiyo.

2. Kuwa na macho yenye kuona mitego,

3. Tambua njia uliyokuwa ni sahihi uendelee kutumia macho kuiona mitego kisha itegue. Kumbuka sio kila mtego ni wakutegua mingine yakuruka na kuachana nayo.

4. Hakikisha Una power ya kutosha itakayokuwezesha kumaliza mwendo wako.

5. Kuwa na Ramani ya kukuongoza katika njia yako.

6. Kama huna ramani, basi kuwa na Mwenyeji wa kukuongoza katika njia yako.
Kila unakopita hakikisha unaweka Alama na kumbukumbu ili baadaye iwe ramani Kwa utakaotaka waje kwako/wawe Kama wewe.

7. Hakikisha ukiota ujue unaota ndoto hata kama hujui mwisho wa ndoto hiyo.
Kuwa na mtazamo/Imani kuwa mwisho utakuwa mzuri na wewe ndiye utaibuka mshindi.

8. Usirukie rukie njia utakazokutana nazo huko mbeleni, huo nao ni mtego.
Ukiwa umelala ndotoni hakikisha hauoti ndoto zilizojichanganya changanya.

9. Usimuambie mtu ndoto yako hata Kama hujui maana yake. Jitahidi kutafuta maana yake mwenyewe.

Basi hayo yatakutosha Kwa leo.
Na ikiwa hujanielewa basi usihofu Kwa maana maandiko hayo sio jela ya kukufunga wewe bali ni ufunguo wa kukufungua katika maisha yako.

Ndimi Taikon, kutoka Nyota ya Tibeli, yenye mbawa mbili.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa Sasa Arusha.
 
Back
Top Bottom