LGE2024 JamiiForums kwa kushirikiana na Star TV inafanya mjadala kuhusu Tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
677
1,098
Fuatilia mubashara mjadala wa Tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaofanywa na JamiiForums kwa Kushirikiana na Start TV.


Kupata taarifa na matukio yote kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ingia hapa: LGE2024 - Special Thread: Mijadala ya Mikoa yote Tanzania Bara inayoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

Washiriki kwenye mjadala huu ni;
1. Prof. Kitila Mkumbo -Mbunge wa Ubungo na Waziri wa Mipango na Uwekezaji - CCM.

2. Isihaka Mchinjita - Makamu Mwenyekiti Act Wazalendo - Bara.

3. Peter Madeleka - Wakili wa Kujitegemea

4. Bonface Jacob - Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani.

====

Kwanini uchaguzi huu unaonekana machoni pa wengi CCM imepora uchaguzi?

Kitila Mkumbo:
Katika hatua zote vyama vyote vilirishiriki katika mchakato mzima, malalamiko yanaweza yakawepo lakini muhimu ni kwamba utaratibu wa kisheria ambao unahusu uchaguzi husika uwe umezingatiwa. Na baada ya matokeo kutangazwa upo utaratibu wa kisheria ambao walalamikaji wanaweza kuchua hatua kwenda kujaribu kutafuta haki katika hatua nyingine.

Kama CCM kauli yenu ni ipi kuhusu watu waliiouwa kipindi cha uchaguzi, je mnatambua ni nani aliyetekeleza mauaji haya ya kinyama ya wagombea upande wa upinzani?

Kitila
: Kauli ya CCM inapotokea mauaji tunasikitishwa na tunalaani mauaji hayo na tunataka vyombo husika kufanya uchunguzi na hatua zichukuliwe kwa wahusika

Kitila: Tanzania inahitaji zaidi uwepo wa CCM kuliko kitu chochote kwani kinaendelea kufanya miradi mbalimbali mikubwa na wananchi wanapaswa kuendelea kuiamini CCM iendelee kukaa madarakani.

Kama chama mlisema hamjaririka na mchakato wa uchaguzi, unahisi ni kwanini?

Isihaka
: Uchaguzi huu ulikuwa ni uchafuzi, kulikuwa na zoezi la dola kukabili wananchi na kupoka mamlaka ya wananchi ya kuamua nani awe kiongozi wao. Kati mchakato huu wa uchaguzi tulishuhudia kwenda kinyume na maamuzi ya bunge ya kutaka uchaguzi huu usimamiwe na tume ya uchaguzi, kwenye kinyume na vyama vya siasa katika mjadala waliofanya ambapo kupitia kikosi kazi ilikubalika katika mambo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ni mifumo ya uchaguzi na moja ya uchaguzi huo ni uchaguzi wa serikali za mitaa, kulikuwa na mabadiliko ya sheria yalioysema tume huru isimamie uchaguzi lakini kupitia bunge waliamua kutotunga sheria hiyo na baadaye OR TAMISEMI wakawa wasimamizi wa uchaguzi huu.

Boniyai: Zoezi la uandikishaji kulikuwa na changamoto nyingi mpaka marehemu kuandikishwa, uandikishwaji wa wanafunzi wenye umri mdogo mpaka shule ya msingi, watu ambao hawapo kwenye maeneo hayo, uenguaji wa wagombea kwa uonevu

Kama wakili unahisi ni wapi ambapo makosa ya kisheria yalifanyika katika uchaguzi huu huenda imechangia kwa namna fulani kuharibu uchaguzi huu wa serikali za mitaa?

Madeleka
: Kosa kubwa sana ambalo tumekuwa tukifanya miaka yote ni kutokuupa uchaguzi wa serikali za mitaa misingi ya kikatiba. Katiba ya JMT inataja uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na mchakato wake. Udhaifu huu wa kukosa misingi ya kikatiba ndio inayopelekea kutungwa kwa sheria ambazo kimsingi hazilengi katika kuhakikisha nchi yetu inaendesha zoezi ya uchaguzi kidemokrasia. Unapokuwa huna misingi ya kikatiba unatoa mwanya kwa wabunge kutunga sheria wanazojua wao na mwisho wa siku watu wanakuja kuhalalisha maovu ambayo yanakuja kufanyika katika uchaguzi.

Madeleka: Nikichukua uzoefu wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, naogopa sana kuona Tanzania inaingia katika uchaguzi mkuu wa 2025 tukiwa na mifumo ya Kikatiba, ya Sheria na Kiuchaguzi hihii. Uchaguzi wa Mwaka huu umegharimu roho za watu, umegharimu Damu za watu, umewafanya watu wengine Leo wabaki na vilema vya maisha vya kudumu, umesababisha Watoto wasiokuwa na hatua wabakie yatima. Sasa kama tutakuwa tunataka 99.01% iongezeke kwa kuongeza idadi ya damu inayopaswa kumwagika 2025 sidhani tutakuwa tuna akili timamu. Wito wangu kama Mtetezi wa haki za Binadamu tubadilishe mifumo ya uchaguzi, kwasababu hii mifumo iliyopo tunapata madhara wote, tuache ubinafsi tufikirie kizazi kinachokuja

Katika uchaguzi huu ni wapi ambapo unaona kumeenda vibaya kiasi kwamba imewafanya mshindwe kwa kiwango kikubwa katika uchaguzi huu? Ni wapi vyama vya upinzani mlikosea?

Boniyai: Niweke jambo sawa kwanza, CHADEMA hatujashindwa, hakukuwa na ushindani! Ushindi wa CCM unakusa mambo 3; Uhalali wa kisiasa, mbili ni ushdini ambao hauna uhalali wa kisheria pamoja na moral authority.

Boniyai: CHADEMA hatujashindwa uchaguzi wa serikali za mitaa kwasababu hakukua na ushindani. Sisi tulizuiwa kuingia kwenye ulingo wa ushindani, kwahiyo huwezi kutuambia tumeshindwa na aliyebakia mwenyewe ulingoni amejitangazia kushinda Uchaguzi kwa kujifurahisha. Sisi hatuwezi kusema kwamba CCM wameshinda na CHADEMA wameshindwa kwakuwa hapakuwa na ushindani na mazingira ya ushindani hayakuwepo.

Je, upi ni msimamo wenu, mnautambua au hamuutambui uchaguzi huu?

Boniyai:
Kama mwenyekiti wa Pwani, hatuna mgombea wowote aliyeshinda, tulitaka mvua inyeshe watanzania waone panapovuja, na watanzania wameona.

CCM kiliungua wagombea karibu wote wa CHADEMA na hata kule ambako walibaki mlitumia mitutu ya bunduki kuwaondoa, kwanini yamefanyika hayo?

Kitila
: Upinzani hawakujiandaa, 75% ya vitongoji CCM ilikuwa mgombea pekee hata kabla ya mchakato wa kuenguliwa kuanza. Tatizo lililoko hapa ni maandalizi, hoja hapa ni kwamba hawakujiandaa. Kuna kanuni za uchaguzi lazima uzingatie, upande wa CCM watu walikuwa trained vizuri.

Katika mazingira kama hayo (ambayo watu wanakamatwa na kura feki zikiwa zimepigwa kwa mgombea wa CCM) mnapata wapi uhalali wa kushangilia kwa kishingo 98.01%?

Kitila
: Kwenye tuhuma kama hizo zipo taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa ambako huko zitaenda kujibiwa na hatua kuchukuliwa.

Kwa yote yaliyotokea chama chako kimechukua hatua gani kuhakikisha kinapambana na kile mnachokiita Uchafuzi?

Isihaka
: Chama chetu hakitambui uchaguzi huu kama uchaguzi halali, na tunataka uchaguzi urudiwe. Tumewataka watanzia watoe ushirikiano hasa kwa maeneo ambayo tulikuwa tunawasihi wananchi wasitoe ushirikiano kwa viongozi viongozi haramu ambao ni mawakala wa uchaguzi haramu, pia tumewaandikia barua vyama vingine vya upinzani ili tukutane kwa pamoja na tutafute mustakabali mpya wa uchaguzi nchini.

Mmesema kwamba hamtambui uchaguzi huu, je wale walioshinda nao vilevile hamtambui ushindi wao?

Isihaka: Uchaguzi unapoharibika mchakato mzima unakuwa umeharibika. Tunamaintain status-quo kwa maana ya hali iliyopo, na sisi tutakwenda mahakamani kwa maeneo yote ambayo watu wetu walienguliwa. Tunachokitaka ni wanachi wasitoe ushirikiano kwa wote ambao hawakushinda uchaguzi huu.

Mazingira ya uchaguzi yaliyoshuhudiwa yakiwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, sheria pamoja na demokrasia kukandamizwa, yanatoa taswira gani kwenye uwekezaji ndani na nje ya taifa letu?

Kitila
: Hoja ya msingi hawa hawakujiandaa, walikuwa na migorogoro kibao kati yao

Katika uchaguzi huu ni kasoro gani ambazo ulishuhudia ambazo ukitazama unaona wenzenu wa upinzani waliona?

Kitila: Katika baadhi ya maeneo idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa wachache kuliko wale waliojiandikisha, hivyo kuna kazi ya ziada inatakiwa kufanywa kwenye kuhamasisha, pia wananchi walikuwa wanapata changamoto ya kupata kupata majina yao, hivyo kwenye teknolojia kuna haja ya vyombo vinavyoshughulikia uchaguzi kuweka mazingira mazuri ya teknolojia.

Madeleka: Kuhusu vyama kujiandaa na uchaguzi na uhalali wa zoezi zima la uchaguzi, hivi ni vitu viwili tofauti. Uchaguzi unakuwa halali kwasababu michakato yote ilizingatia sheria.

Katika mazingira ambapo CCM imetangazwa kushinda kwa 99% wapinzani wanapaswa kufanya nini kuhakikisha sauti za wananchi zinaendelea kusikika hata nje ya uchaguzi?

Isihaka: Katika mazingira ya namna hii wajibu wa upinzani unaongezeka; kusimama na kuwasemea wananchi juu ya changamoto za taifa lao.

Unadhani nini kinawazuia upinzani kuitoa CCM madarani ambayo mnasema kuwa CCM imechoka na inaelekea kutoka madarakani?

Isihaka: Ni matumizi ya nguvu za dola kuua utumishi wa umma, ambapo watumishi wa umma wamegeuka kuwa chawa wa taifa lao wanageuka kutumikia CCM matokeo yake nchi inazidi kwa vibaya

Taarifa ya CCM kushinda kwa 99% ni kielelezo Cha juu kuwa CCM ni dhaifu sana, yaani kimekuwa dhaifu kiasi ambacho kinaogopa maoni ya Wananchi, kinaogopa Watanzania wakiuliza juu ya wanavyokiona Chama Cha Mapinduzi watasema nini? Kwahiyo baadaye wanakuja kuibuka na haya majibu ambayo hata wenyewe hawawezi kuyaamini na inahitaji kuwa mwendawazimu uyakubali kwamba baada ya ukuaji wa Demokrasia katika kipindi chote hichi leo CCM au kuna chama kingine kinaweza kushinda kwa 99% mahali popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

PIA SOMA
- LGE2024 - JamiiForums na StarTV kuwahoji wanasheria kuhusu Hali ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa leo Novemba 23, 2024
 
Nnachojua watumishi wote wa uma walipewa maelekezo maalumu toka uandikishaji mpaka upigaji !! Elewa neno ipigaji.

Walimu mathalani na wote waliosimamia walipewa target kwakila kituo wawe wamefikisha kura idadi fulani ambayo ni almost not less than 95% kwa kila kituo.

Kimsingi wanatupeleka kwenye civil disorder tujiandae kwa machafuko kama vyombo vya usalama havitalitetea taifa dhidi ya ccm.
 
Fuatilia mubashara mjadala wa Tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaofanywa na JamiiForums kwa Kushirikiana na Start TV.


Kupata taarifa na matukio yote kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ingia hapa:

-
 

Attachments

  • 5891204-aeb7d1d0d93f0573adbcbe9287bbfca7.mp4
    29.9 MB
  • 5890513-6210cd34d68240f1725651f41e222ed7.mp4
    19.4 MB
  • 5890193-242c46d8611c5927d2bae1d81e6b1414.mp4
    66.1 MB
Back
Top Bottom