SoC04 Jamii isiyoinyooshea kidole serikali, jamii yenye ari ya uwajibikaji

Tanzania Tuitakayo competition threads

mailimoja77

Member
May 18, 2016
21
8
Imekuwa ni desturi ya jamii ya watanzania kuinyooshea kidole na kuilaumu serikali katika kila changamoto inayotukumba, iwe matatizo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, na mazingira. Tunapotazamia malengo ya muda mrefu kuanzia Miaka 5 - 25 kufikia Tanzania tuitakayo, wajibu binafsi na uwajibikaji katika ngazi ya familia ndio suluhu ya kufikia Tanzania yenye changamoto chache kulinganisha na hali tuliyonayo kwasasa ambapo tunakumbwa na changamoto kadha wa kadha mathalani utendaji mbovu kwa baadhi ya watumishi wa umma na taasisi binafsi, changamoto kwenye sekta ya afya, sekta ya elimu, uhaba wa maji safi mijini na vijijini, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Changamoto na matatizo mengi tuliyonayo nchini ni matokeo ya watu kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Kama ulimbukeni huu wa kuilaumu serikali hautokoma basi maendeleo endelevu tutaendelea kushuhudia kwenye nchi za wenzetu tu. Iwapo kila mtu atashindwa kujimilikisha hii nchi na kuiona ni yake na kuwa tayari kuwajibika katika eneo lake basi tutaendelea kuwa na taifa lenye choyo, chuki, ubinafsi, lawama, visingizio, maadili ya hovyo, na changamoto nyingi zisizo za msingi.
Mfano;
Watu wanajenga kwenye mabonde na mkondo wa maji, maafa ya mafuriko yakijitokeza lawama kwa serikali.

Mimba za utotoni kwa wanafunzi na ulawiti kwa watoto lawama zinaenda kwa serikali.

Uchafu wa miji huku baadhi ya watu wakiwa na tabia ya kufungulia chemba za choo pindi mvua zikinyeesha ambapo huleta milipuko ya magonjwa kama kipindupindu ni wajibu binafsi kuepukana na hili ila kidole cha lawama kinaelekezwa serikalini.

Hata uharibifu wa mazingira kwa kuchoma mkaa, kukata miti kiholela, kulima na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji na kusababisha ukosefu wa huduma ya maji lawama zinaiendea serikali wakati tatizo limeanzia ngazi ya chini yaani mtu binafsi.

Utendaji mbovu wa watumishi wa umma na taasisi binafsi ni changamoto iliyozalishwa toka kwenye familia na jamii zisizo na weledi matokeo yake wametuzalishia watendaji n watumishi wa hovyo hovyo.

Hivyo basi kushindwa kuwajibika ngazi binafsi na ngazi ya familia huchochea kuwa na matatizo ambayo hayaleti mantiki kuilaumu serikali ambayo inawatendaji na viongozi toka kwenye jamii zetu hizi hizi, tunachokiona serikalini yanaakisi kinachoendelea kwenye familia zetu na jamii zetu, watu wanakwepa wajibu wao kisha kubaki kupiga domo la lawama na visingizio.

Uwajibikaji ni msingi Muhimu wa maendeleo katika maeneo yote ya maisha na ni hatua ya makusudi kuzingatia kuhakikisha kila mtu anatimiza majukumu yake katika nafasi aliyopo.

Mtu akiwajibika binafsi hupunguza au kuondoa kabisa nafsi lalamishi, majungu, unafiki na migogoro huongeza uzalendo na kupunguza ubinafsi.

Serikali na mipango yake endelevu ya maendeleo ni bure kama hapatokuwa na raia wa kukubaliana na mipango hiyo kwa maana ushiriki hai wa wananchi hufanya utekelezaji wa malengo ya kimaendeleo kufanikiwa kwa wepesi.

Ni rai yangu tutazamie sasa kuandaa kizazi chenye ari ya wajibikaji kuanza sisi wenyewe kuwa wazalendo wa nchi na wawajibilkaji katika maeneo yetu kila mmoja, kuanzia ngazi ya uwajibikaji binafsi, familia na hata jamii kuelekea taifa lenye uwazi na uzalendo, hii itapelekea kuwa na kizazi kipya chenye hamasa ya uwajibikaji na uzalendo ambacho kitafanikisha kuwa na Tanzania tuitakayo isiyo na kunyoosheana vidole vya lawama.

ZIFUATAZO NI BAADHI YA HOJA ZINAZOKAZIA SUALA LA UAJIBIKAJI NGAZI YA MTU BINAFSI NA NGAZI YA FAMILIA KATIKA KULETA TIJA KWENYE MAENDELEO YA TAIFA KUIFIKIA TANZANIA TUITAKAYO.

Muandishi John Gagarini (17.06.2012);
aliandika na kumnukuu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Bw. Ahmed Kipozi alipokuwa katika mdahalo wa Utawala Bora na Uwajibikaji wa Viongozi Kwa Wananchi kwenye kata ya Msata wilayani humo. Bw. Kipozi alipendekeza suala la uwajibikaji lianzie ngazi ya familia ili kujenga taifa lenye uwajibikaji na uadilifu kuepukana na viongozi wabadhirifu wa mali za umma.

"Uadilifu unaleta uwajibikaji, hivyo ni vyema jamii zikajenga utamaduni wa kuwajibika na si kuilaumu tu viongozi kwani usipowajibika kwenye familia ndivyo utaratibu utakaouendeleza sehemu za utendaji wa kazi na katika kuendeleza malengo ya maendeleo" Bw. Kipozi.

www.mwananchi.co.tz (23.10.2019 ikaboreshwa 17.03.2021); Iliandika makala kuhusu changamoto ya kusambaza maji safi na salama Iliandika;

"Utafiti juu ya usambazaji wa maji vijijini uliofanyika kwenye nchi 13 zinazoendelea umeonesha; serikali za nchi kushindwa kupeleka madaraka kwa wananchi, miradi ya maji hupangwa kutoka juu kwenda chini, badala ya kuanzia chini kwenda juu... Nchi ya Rwanda kwa upande wake imefanikiwa kutunga sheria ya kuvuna maji ya mvua, hii imesaidia kupiga hatua kubwa katika zoezi zima la kusambaza maji safi na salama" imezungumza makala hiyo.

Huu ni mfano mzuri wa uwajibikaji, ushirikishwaji na uwezeshaji. kila mtu nchini Rwanda anawajibu kuyavuna maji, serikali imewashirikisha wananchi kwa kutunga sheria ya kuvuna maji ya mvua na inawawezesha katika njia za kuyavuna.
Makala hii ikaonesha umuhimu wa uwajibikaji tokea ngazi ya chini yaani wajibu binafsi, wajibu ngazi ya familia, wajibu ngazi ya jamii kisha taifa.

www.dw.com (30.01.2024) Imeandikwa na Hawa Biloga. Ripoti mpya iitwayo Kielelezo Cha Mtazamo wa Ufisadi inasema;

"Kulingana na ripoti mpya ya shirika la kimataifa la kufuatilia masuala ya ufisadi la Transparency, nchi za Denmark, Finland, New Zealand na Norway ndizo nchi zilizo na ufisadi mdogo zaidi duniani" Inasema ripoti hiyo. (Nchi hizi ni moja ya nchi zenye uchumi mzuri duniani)

"Mataifa yaliyo kisini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania yamepata kiwango cha chini zaidi..." Inasema ripoti hiyo. (Na nchi hizi pia ni moja ya nchi zenye uchumi wa chini duniani)

Hivyo basi, hiki ni Kielelezo tosha kuwa Kuna uhusiano kati ya maendeleo endelevu na uwajibikaji.

Hitimisho.
1719781266161.jpeg


(PICHA NIMEANDAA MWENYEWE)

Kama picha iliyoambatanishwa inavyoonesha,
Unapoinyooshea serikali kidole kuilaumu basi Kidole kimoja (1) kitaielekea serikali lakini vidole vitatu (3) vinakurudia mwenyewe ikiwa na maana kwamba, unawajibu mkubwa zaidi kutatua changamoto kuliko yeyote. Na Kidole kimoja (1) kilichobaki (dole gumba) kinaangalia chini, hii inamaanisha kwamba; kama pande zote mbili yaani Serikali na Mtu binafsi zisipotambua wajibu wao basi kila kitu kitashuka chini au kitakufa na hakuna kitakachoendelea mbele.

Hivyo Basi, kuelekea Tanzania Tuitakayo, Tuache lawama na Kila mtu asimamie Wajibu wake katika nafasi aliyopo tutaifiia Tanzania Tuitakayoyenye maisha bora kwa kila mtu.
 
Back
Top Bottom