Iringa: Uchunguzi waonesha watoto hunyweshwa Pombe ili walale

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,591
8,820
Wakati Serikali ikipambana na tatizo la utapiamlo sugu ‘udumavu’ katika mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, imebainika kuwa wazazi wamekuwa wakiwanywesha watoto pombe za kienyeji kama sehemu ya kuwatuliza ili waendelee na shughuli zao.

Iringa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa udumavu nchini, ikiwa na asilimia 47.1 ikitanguliwa na Rukwa, yenye asilimia 47.9 na Njombe inayoongoza nchini kwa asilimia 53.7.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya vijiji vya Manispaa ya Iringa, umebaini watoto hao hunyweshwa pombe aina ya ulanzi ‘mkangafu na mdindifu’, wanzuki na pombe za kupika na mahindi maarufu komoni. Mbali na hilo, pia wazazi hushindwa kuwapa mlo bora kwa wakati, kwa sababu muda huwalazimisha kulala kwa kuwapa pombe hizo na kuishia kupata utapiamlo.

Hata hivyo, lishe duni ndiyo sababu kubwa ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano na inakadiriwa kugharimu Serikali asilimia 2.6 ya pato la Taifa kila mwaka.

Akilizungumzia hilo, Mkuu wa mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema suala hilo lipo, ila wamekuwa wakichukua hatua, ikiwamo kutoa elimu. “Wajawazito wanakunywa na watoto wakizaliwa wanaanza kupewa pombe, lakini hatua zimekuwa zikichukuliwa.

Tunakemea unywaji pombe uliokithiri kwa kuwashiriksha wanawake na wanaume, hali hiyo ninakiri ipo na haitaisha kwa muda mfupi na sisi viongozi hatutachoka, tutaendelea kutoa elimu zaidi,” alisema Dendego.

Hali halisi ilivyo

Novemba 10, majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha Semtema Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa, mwandishi alishuhudia watoto watatu wanamfuata mama yao katika shughuli zake za uuzaji wa pombe za kienyeji.

‘Mama tuna njaa’ anasema mmoja wa watoto hao anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano, aliyeongozana na dada yake makadirio miaka 7 na mdogo wao miaka mitatu.

‘Nendeni mkale makande yapo jikoni nilifunika na ndoo,’ anasikika mama huyo anayeonyesha ametumia pia kilevi anachouza. Baada ya muda wa dakika tano anawaita na kuwapa pombe ya ulanzi kwenye sado za vipimo vya nusu lita, kila mtoto ya kwake.

Jambo la ajabu ni kuwa wale wawili wakubwa walikunywa haraka na kumaliza pombe yote, wakati mdogo wao akinywa taratibu lakini aliimaliza na walipokuwa wanaondoka alikuwa anayumba na dada yake akambeba wakaondoka eneo lile.

Mama wa watoto hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Monica, alipoulizwa kama ni sahihi kuwapa watoto pombe, alisema: “Nimekuzwa, nimelea wadogo zangu kwa pombe na watoto wetu wanakunywa, hakuna jambo la ajabu ni utamaduni wetu.

“Jeshi la Polisi na uongozi wa mkoa hawapaswi kulifumbia macho suala hili, watoto wanapokunywa hawali, wanalala na njaa na inawaathiri sana,” alisema Schola Mgombelwa, mkazi wa eneo hilo.

Athari za kiafya

Ofisa lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Walbert Mgeni alisema kitaalamu pombe huingilia ukuaji wa ubongo wa mtoto, hivyo badala ya kukua jinsi unavyotakiwa ukuaji wake unaingiliwa na kusababisha udumavu na utapiamlo.

“Hii huathiri michakato ya kifiziolojia katika mwili wa mtoto, hasa mfumo wa umeng’enyaji chakula, anaweza kupata magonjwa ya moyo,” alisema Mgeni.

Naye Ofisa lishe mwandamizi TFNC, Dorice Katana alishauri: “Mtoto anatakiwa apewe vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi, kundi la pili vyenye asili ya wanyama na jamii ya kunde, maziwa, mbogamboga, mafuta, asali na apate angalau milo mitatu,” alisema Katana.

Kwa upande wa daktari mbobezi wa upasuaji wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Zaitun Bokhari alisema, “Mtoto mdogo kunyweshwa pombe ina madhara makubwa, haijalishi ni za kienyeji au za kisasa. Ubongo wake unakuwa bado haujakomaa, na ni rahisi kuharibu ini au figo”.

Mikakati ya Serikali

Dendego alisema wana shughuli nyingi za kutokomeza hali ya udumavu katika mkoa, tangu tumboni mwa mama kwa maana wengi hawali vizuri, hawapati mahitaji muhimu, kwa hiyo mtoto anaweza kuzaliwa vizuri lakini zile siku 1,000 za ukuaji wake akaharibika.

“Tuna programu ya lishe mashuleni na katika vituo vya kutolea huduma za afya, kubwa ni kupata virutubisho, Serikali inashirikiana na wadau kutoa elimu ya umuhimu wa lishe kwa kinamama. “Wajue namna ya kuandaa chakula cha mtoto, kinapaswa kiwe na nini na ni mchanganyiko upi unatengeneza chakula bora,” alisema Dendego.

Akilizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis alisema tatizo la udumavu kwenye maeneo yanayopatikana chakula kwa wingi, kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, kilichopo mkoani Iringa kimepata kibali cha kufanya tafiti za hali duni ya lishe, ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la udumavu linaloikabili manispaa hiyo,” alisema Mwanaidi.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom