SoC02 Inaanza na wewe - Afya ya Akili

Stories of Change - 2022 Competition

Nyakabwegula

New Member
Feb 7, 2019
1
1
Lipo shinikizo la kijamii kwamba mwanadamu anayeweza kukubalika na kuaminika ni yule aliye na ‘akili timamu’. Kwasababu hiyo kila mmoja hupenda kujitazama kuwa yu timamu pengine dhidi ya, au kuliko wengine wote wanaomzunguka. Huona kuwa changamoto za kiakili hazimhusu yeye; ni matatizo ya wengine. Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonyesha ya kwamba, ingawa kiasili mwanadamu alipaswa kuwa na utimamu usioyumba, lakini mabadiliko ya kimaisha ambayo yameleta ushindani katika kila kitu, yamechochea matumizi ya akili yaliyopita kiasi na hivyo kuathiri afya ya akili za wanadamu karibu wote hasa wa kizazi hiki. Kwasababu hii, tafiti nyingi zinadai ya kwamba kila mwanadamu ni kichaa kwa namna moja au nyingine.

Katika Tanzania, uelewa wa wanajamii juu ya masuala yahusuyo afya ya akili bado uko chini sana. Yapo matukio mengi ambayo, pengine hayatazamwi kwa kina, lakini yanaonyesha kuwa mzizi wake upo katika afya duni ya kiakili. Linapozungumzwa suala la afya ya akili katika jamii, fikra za wengi huwaelekea vichaa ama walioko hospitalini au wanaoranda mitaani. Ingawa fikra hizo zina ukweli, lakini ni ukweli wa upande mmoja.

Pamoja na jamii kuonekana kukubali kuwa kushughulisha akili kupita kiasi, hasa kutumia muda mwingi ‘kujisomea mambo magumu’, kwaweza kuathiri utimamu wa akili, zipo imani kuwa wagonjwa wa akili huwa hivyo kwa kurogwa. Huenda katika hili kuna ukweli, lakini hakuna ushahidi wa kitaalamu na hivyo kufanya dai hili kuwa mtazamo tu katika jamii.

Hata hivyo, ipo haja ya jamii kuongeza uelewa na umuhimu wa kushirikiana na kushirikishana. Mabadiliko ya kimtazamo yanahitajika. Hatua ya kwanza katika kuibadilisha jamii ni kuisaidia kutambua ya kwamba, yeyote anaweza kupatwa na changamoto ya afya ya akili. Kila mmoja anapaswa kuijali afya ya akili ya mwingine.

Kutajwa au kujitaja kwamba una changamoto ya afya ya akili, ni aibu kwenye jamii kwa mtazamo uliopo sasa. Bila kujua, hiki kinachoonekana kuwa ni aibu kinaongeza matatizo zaidi. Ni shinikizo zaidi kwa wanaopitia changamoto za kiakili na ni lango la madhara makubwa ambayo yangeweza kuepukwa shinikizo hilo lisingekuwepo. Kuna haja ya kujenga jamii inayowakubali, kuwajali, kuwaheshimu na kuwa tayari kuwasaidia wanaopitia changamoto hizi. Na hii inafaa ianzie katika ngazi ya familia kwenda nje kwenye jamii kwa upana wake.

Lazima ionekane kwamba, kuwa na changamoto katika afya ya akili kunakubalika mbele jamii, na kwamba ni ubinadamu kwa mtu kutokuwa sawa wakati fulani. Ikiwa miili yetu inaweza kuchoka au kuchoshwa, vivyo hivyo kwa akili zetu.

Tunahitaji jamii ambayo ni kimbilio la wanaojisikia kutokuwa sawa katika akili zao, tofauti na ilivyo sasa, wenye changamoto kuona ni salama kwao kuikimbia jamii.

Ni tamanio la kila mwanadamu kuishi maisha ya furaha yasiyo na maumivu ya aina yoyote. Kwa bahati mbaya, hilo haliwezekani. Maisha yana changamoto na mapito mengi ambayo hutuacha na makovu yanayopona na yaliyo magumu kupona. Hakuna mwanadamu ambaye hapitii maumivu; ni viwango tu na uwezo wa kuhimili ndivyo hutofautiana kati ya mtu na mtu.

Yapo maumivu yaletwayo na kushindwa kufikia matarajio yetu au ya wanaotutazama, matukio ya kikatili au ya kutisha, dhana ya kukataliwa, maumbile yetu kutoturidhisha au mabadiliko ya kimaumbile yanayosababisha tujisikie kupoteza mvuto wa kimwonekano mbele ya jamii, na mengine mengi.

Twaweza kujaribu kukabiliana na changamoto hizi kwa kujikokota kujaribu kusimama tena baada ya kuanguka, lakini yawezekana tusiweze kwa jitihada zetu. Yawezekana mapito tuliyopitia yametufanya tuone hatuwezi tena. Huenda tumekuwa watu wa hasira sana na kuona tunaweza kudhuru wengine na hata kujidhuru. Pengine tunasononeka sana kiasi kwamba hatuoni tena thamani ya maisha.

Inapofika hatua hiyo, jibu huwa ni moja tu, tunahitaji kusaidiwa. Lakini vipi kama tunaona tunahitaji msaada na hakuna pa kupata msaada huo. Mbele, nyuma, kulia na kushoto kumejaa watu walio tayari kuhukumu kuliko kusaidia? Jamii isiyojali ni hatari zaidi kuliko tatizo lenyewe.

Watanzania wengi wamepoteza maisha kwa kukosa ujasiri wa kumshirikisha japo rafiki. Waliothubutu nao hawakusaidiwa njia za kukabiliana nalo. Na hii ni kwasababu wengi katika jamii hawana uelewa wa tatizo na wapi msaada unaweza kupatikana. Wapo wataalamu wa kisaikolojia ambao wanaweza kuwa msaada mkubwa. Bahati mbaya, huduma zao ni ghali sana kiasi kwamba, inaonekana ni anasa kwenda kupata msaada wao. Badala ya kuwa msaada, viwango wanavyotoza vimekuwa tatizo jingine juu ya tatizo.

Mwaka 2018 kulikuwa na matukio ya kusikitisha ambapo, jijini Mwanza, kijana wa miaka 25, mhitimu wa shahada ya kwanza ya sayansi ya kompyuta, alikatisha Maisha yake kwa kupanda na kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya jengo la kibiashara, Rock City Mall. Sababu ya yeye kufanya hivyo ni ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha, iliyomfanya, kwa mujibu wa ujumbe aliouacha, ajione kuwa ni maskini asiye na chochote wala yeyote wa kumsaidia.

Mwaka huohuo wa 2018, kijana mwingine wa miaka 24, mwanachuo wa chuo cha Mtakatifu Agustino kampasi ya Mbeya, alijinyonga mara baada ya timu ya Liverpool, aliyokuwa akiishabikia, kupoteza mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya timu ya Real Madrid ya Hispania. Inadaiwa kwamba, kijana huyo ambaye amekuwa akicheza sana michezo ya kubashiri, aliweka kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa sehemu kubwa ya ada ya masomo yake. Matarajio yake kukwama na kwasababu hiyo kupoteza kiasi hicho cha fedha, ilikuwa ni kihama kwake.

Mwaka 2022, mkoani Lindi, mwanamume wa umri wa miaka 59, mkazi wa Dar Es Salaam, alijinyonga kutokana na kutingwa na madeni. Na mwaka huohuo wa 2022 jijini Arusha, kijana wa miaka 17 alijiua kwa kujipiga risasi kwasababu zinazohusianishwa na kifo cha baba yake nchini Marekani. Vilevile kuna matukio ya kikatili hasa ya kuua wenza kwasababu za wivu wa kimapenzi, ambayo ni mengi sana na yanaripotiwa mara kwa mara kutoka pande tofauti za nchi.

Tujiulize, je kulikuwa na sikio lililokuwa tayari kuwasikiliza ndugu hawa kabla ya kufikia kufanya maamuzi waliyochukua? Ni kiasi gani tunaguswa na maumivu ya watu wetu wa karibu na kwa kiasi gani tunawaonyesha utayari wetu wa kuwasikiliza bila ya kuwahukumu au kuwapaka aibu kwa kuwatangaza? Leo twasoma habari za wengine, kesho ni ama sisi au ndugu zetu wa karibu. Je, tunashiriki kujenga mazingira ya kutuinua pindi tutapoanguka? Ujenzi wa jamii rafiki kwa changamoto za afya ya akili ni jukumu la kila mmoja, mmoja-mmoja, likianza na wewe. Tujielimishe na kwa elimu hiyo tuielimishe jamii nzima. Inawezekana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom