Baadhi ya wanachama wa JamiiForums wamedokeza kudai kwamba huduma ya Pacemaker haipo Muhimbili. Aidha, madai hayo yanabainisha kwamba wagonjwa wamekuwa wakiahidiwa kuletwa kwa huduma hiyo lakini mpaka sasa haijawekwa na kuna taarifa kuwa baadhi wamepoteza maisha kutokana na kukosa huduma hiyo.
- Tunachokijua
- Pacemaker ni kifaa kidogo ambacho huwekwa (kilichopandikizwa) kwenye kifua ili kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo. Kifaa hicho husaidia kutengeneza umeme wa moyo pamoja na kuongozaa mapigo yake. Kuweka pacemaker kwenye kifua kunahitaji utaratibu wa upasuaji.
Aidha kuhusu madai yaliyotolewa na mdau, JamiiForums imefanya mawasiliano na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Anna Nkinda amesema:
“Si kweli Pacemaker hazikuwepo kwa muda wa miezi miwili, kilichotokea ni kuwa zilipungua kidogo lakini wakati huo zilikuwa zimeagizwa kutoka nje, hospitali yetu ni kubwa hatuwezi kukaa bila Pacemaker.
“Kilichotokea wakati zimepungua ndani ya wiki mbili wale wenye uhitaji wa dharura ambao hawawezi kusubiri ndio wakawa wanalazimika kupatiwa huduma, tayari Pacemaker zimeshaingia na zimeanza kutumika kuanzia jana, leo zoezi linaendelea.
“Taasisi yetu ni ya Serikali hatuwezi kuishiwa kabisa, ikitoke zinaelekea kuisha tunashirikiana na taasisi na hospitali mbalimbali Nchini ambapo tunaweza kuchukua kutoka kwa wenzetu wa Tanzania au Afrika Mashariki.
“Mfano wiki ya Februari 6-12 tuliweka Pacemaker tatu, wiki ya 13-19 hatukuwa na mgonjwa wa dharura aliyehitaji Pacemaker.
“Jana waliwekewa Pacemaker wagonjwa watatu na leo wagonjwa watano, kwa kuwa zimeshakuja madaktari wameshaanza kupiga simu kwa wale waliokuwa wakihitaji.
“Madai kuwa kuna watu wamefariki kwa kukosa Pacemaker hospitalini kwetu si za kweli, hata hizo habari kuwa kuna mgonjwa amefariki leo (Februari 24, 2023) kwa kuikosa huduma hiyo hazina ukweli.”