Hotuba ya mapendekezo Ya mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,689
55,662
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2016/17

UTANGULIZI

1.Mheshimiwa Spika,naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17.

2.Mheshimiwa Spika,naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema na hivyo kuweza kukutana ili kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17.

3.Mheshimiwa Spika,napenda kutumia nafasi hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, na Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu, kwa uongozi wao mahiri katika kusimamia uwajibikaji na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi

kwa kasi kubwa zaidi. Katika kipindi kifupi tumeona mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato, kuanza kutolewa kwa elimu msingi bila malipo, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo na kuongezeka kwa uwajibikaji kwa watumishi wa umma. Ni imani yetu na ya kila Mtanzania kuwa chini ya uongozi wao, uchumi wa Taifa utaimarika na kukua kwa kasi zaidi kutokana na usimamizi madhubuti katika utekelezaji wa Mipango, Programu, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mikakati mbalimbali ya maendeleo.

4. Mheshimiwa Spika,napenda kuishukuru kwa dhati kabisa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kwa ushirikiano wao. Maelekezo na ushauri mzuri waliotupatia wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 umetusaidia katika kuandaa hotuba hii na kuboresha hatua za maandalizi ya Mpango wenyewe.

5.Mheshimiwa Spika,kipekee nimshukuru Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb), na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Servacius Beda Likwelile kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku.

6.Mheshimiwa Spika,Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 ninayowasilisha leo katika Bunge lako Tukufu yatatumika kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17.

7.Mheshimiwa Spika,Mapendekezo ya

Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamezingatia: malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Miaka 15 (2011/12 – 2025/26); taarifa ya awali ya maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wakati akizindua Bunge la 11 yenye msisitizo wa ujenzi wa uchumi wa viwanda; na Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa mwaka

2015. Aidha, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamezingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; makubaliano ya kikanda na Kimataifa ikiwemo: Dira ya Afrika 2063, Mpango kazi wa Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (2008); Sera ya Viwanda ya Afrika Mashariki pamoja na mkakati wa utekelezaji wake; Mwelekeo wa viwanda wa SADC (2013 – 2018) na Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda ya SADC (2015 – 2063).

TATHMINI YA MWENENDO WA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII

(a) Mwenendo wa Uchumi

8. Mheshimiwa Spika, Pato halisi la Taifalilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 mwaka 2014 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.3 mwaka 2013. Licha ya kupungua kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa, Tanzania imeendelea kuwa na kiwango cha juu cha ukuaji kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2013 na 2014. Ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki mwaka 2014 ni kama ifuatavyo:- Rwanda (asilimia 7.0), Kenya (asilimia 5.3), Uganda (asilimia 4.9) na Burundi (asilimia 4.7).

9. Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa beiumeendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja, ambapo uliongezeka kutoka asilimia 4.0 Januari 2015 hadi asilimia 6.8 Desemba 2015;viwango vya ribavinaonesha kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kupata mikopo na uwekezaji nchini ambapo tofauti kati ya riba za amana za mwaka mmoja na riba za mikopo ya mwaka mmoja iliendelea kupungua kutoka asilimia 3.43 Januari 2015 hadi asilimia 3.22 Oktoba 2015; nathamani ya mauzo njeya bidhaa na huduma iliongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 8,610.0 Oktoba 2014 hadi Dola milioni 9,406.1 Oktoba 2015 sawa na ongezeko la asilimia 9.2. Aidha,thamani ya Shilingiya Tanzania dhidi ya dola ya Kimarekani iliendelea kupungua kutoka wastani wa shilingi 1,745.6 Januari 2015 hadi shilingi 2,177.1 Oktoba 2015.

(b) Kiwango cha Umaskini

10. Mheshimiwa Spika,Tafiti za Mapato na Matumizi katika Kaya, zinaonesha kuwa, kiwango chaumaskinimijini na vijijini kimepungua, mwenendo ambao unaashiria kuwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa asilimia 6.5 kwa mwaka iliyofikiwa kwa kipindi cha muongo mmoja na nusu uliopita imeanza kuwanufaisha wananchi. Umaskini ulipungua kutoka asilimia 39

(1992) hadi asilimia 34.4 (2007), sawa na asilimia

4.6 kwa kipindi cha miaka 15. Vile vile, Umaskini katika kipindi cha miaka 5 ya karibuni ulipungua kwa asilimia 6.2 kutoka asilimia 34.4 (2007) hadi asilimia 28.2 (2012). Katika kutatua tatizo la umaskini, Serikali itaelekeza nguvu zaidi katika sekta ya viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

(c) Utekelezaji wa Bajeti

11. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2014/15,bajeti ya Serikaliilikuwa shilingi bilioni 19,853.3 ambapo bajeti ya maendeleo ilikuwa shilingi bilioni 6,473 sawa na asilimia 32.6 ya bajeti yote. Utekelezaji wa bajeti ulifikia asilimia 86.6 ya lengo kutokana na kupungua kwa mapato ya ndani, misaada na mikopo. Mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 9,938.4 sawa na asilimia 87.8 ya makadirio. Matumizi yalikuwa shilingi bilioni 17,189.7 sawa na asilimia 87 ya makadirio ya bajeti ambapo matumizi ya maendeleo yalikuwa shilingi bilioni 3,261.7 sawa na asilimia 51 ya makadirio ya bajeti ya maendeleo. Aidha, katika mwaka 2015/16, fedha za maendeleo zilizotolewa hadi Desemba 2015 zilifikia shilingi bilioni 1,845.57, sawa na asilimia 31.2 ya bajeti ya maendeleo.Deni la Taifalilifikia dola za kimarekani milioni 19,221.4 Oktoba 2015, ikilinganishwa na dola milioni 18,643.8 Oktoba 2014. Ongezeko hilo lilichangiwa kwa kiwango kikubwa na malimbikizo ya riba ya deni. Deni la Taifa linatokana na mikopo ya masharti nafuu ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya nishati, maji, barabara, madaraja, reli na viwanja vya ndege.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa

12. Mheshimiwa Spika,mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya Matokeo Makubwa Sasa ni pamoja na: kupata hatimiliki za mashamba makubwa 4 ya Bagamoyo, Kitengule, Lukulilo na Mkulazi; ukarabati wa maghala 30 na ujenzi wa skimu 19 zenye jumla ya hekta 9,709 na hivyo kuwanufaisha wananchi 69,681; kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara katika shule 167 sawa na asilimia 63.25; kuongezeka kwa ufaulu wa shule za msingi na sekondari kutoka asilimia 31 na 43 mwaka 2012 hadi asilimia 57 na 70 mwaka 2014 kwa mtiririko huo; kuunganisha umeme kwa wateja wapya 8,078 kupitia mradi wa usambazaji wa umeme vijijini awamu ya pili ambapo hadi Juni 2015, wateja waliounganishiwa umeme chini ya miradi ya REA na TANESCO wamefikia 241,401; kupungua kwa muda wa meli kukaa bandarini kwa ajili ya kupakia na kupakua mizigo kutoka siku 7.0 hadi 2.9; uchukuzi wa mizigo kwa njia ya reli umeongezeka kwa asilimia 42 kwa mwezi; kukamilika kwa ujenzi wa miradi ya maji 975 yenye jumla ya vituo 24,129 vya kuchotea maji katika halmashauri 148 ambavyo vimenufaisha wananchi milioni 5.75; na kuanzishwa Jumuiya za Watumia Maji 1,802 ambapo Jumuiya 875 zimesajiliwa na kutoa huduma za maji vijijini kwa ufanisi.

Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati

Miundombinu

13. Mheshimiwa Spika,hatua iliyofikiwa kwarelini kukamilika kwa ukarabati wa mgodi wa kokoto wa Tura - Tabora na mtambo wa kuzalisha kokoto wa Kongolo – Mbeya kwa ajili ya matumizi ya njia za reli; kwa upande wabarabarani kukamilika kwa ujenzi wa km 542.6 za barabara kuu ikilinganishwa na lengo la km 560.3 kwa kiwango cha lami; kukamilika kwa ukarabati wa km 102.09 za barabara kuu chini ya lengo la km 131.5 kwa kiwango cha lami; kukamilika asilimia 100 kwa ujenzi wabomba la gesikutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542); kukamilika kwa

ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo; kukamilika kwa vituo vya kupokelea gesi vya Somanga – Fungu na Kinyerezi; kukamilika kwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi I; kukamilika kwa asilimia 90 ya ujenzi wa gati labandari ya Itungi(Ziwa Nyasa); kukamilika kwa

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano(km 7,560) na kusambazwa katika mikoa 24 Tanzania Bara na kuendelea na kazi ya kuunganisha Zanzibar katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi; na kuboresha upatikanaji wahuduma za majisafi vijijini kufikia wananchi 21,783,062 sawa na asilimia 68.8.

Kilimo

14. Mheshimiwa Spika,shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kuzalisha na kusambaza miche bora ya kahawa 1,014,671 katika wilaya za Moshi, Mbinga, Bukoba, Mbozi na Tarime; kukamilika kwa tafiti na kuidhinishwa kwa aina mpya 65 za mbegu za mazao ya chakula kutoka vituo vya utafiti vya umma na binafsi na kukamilika kwa ukarabati wa minada ya upili ya Pugu (Ilala), Lumecha (Songea), Kirumi (Butiama) na Nyamatala (Misungwi) na ununuzi wa mitamba 75 kwa ajili ya mashamba ya Ngerengere na

Mabuki; na kukamilika kwa skimu 19 za umwagiliaji mpunga zenye hekta 9,709 kati ya skimu 39 zenye hekta 21,738.

Viwanda

15. Mheshimiwa Spika,hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanda cha Viuadudu Kibaha, Pwani; kulipa fidia ya shilingi bilioni 7 katika Eneo Maalum la Uwekezaji Bagamoyo ambapo fidia iliyolipwa hadi sasa ni shilingi bilioni 26.64 kati ya shilingi bilioni 47.5 zinazopaswa kulipwa; ulipaji wa fidia ya shilingi bilioni 53 katika Kituo cha Biashara na Uwekezaji Kurasini, na hivyo kukamilisha fidia iliyokadiriwa kulipwa mwaka 2013 ya shilingi bilioni 94.1; na kukamilika kwa ukarabati wa barabara ya Itoni - Mkiu – Liganga na Mchuchuma kwa kiwango cha changarawe.

Maendeleo ya Rasilimali Watu

16. Mheshimiwa Spika,wanafunzi 159 wamepata mafunzo katika fani za mafuta na gesi kwa ngazi mbalimbali ndani na nje ya nchi; kupatiwa mafunzo walimu wa sekondari 5,868 wa masomo ya Sayansi, Hisabati, Biolojia na Lugha; na kupeleka fedha kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kiasi cha shilingi bilioni 135.8 katika nusu ya mwaka 2015/16 ambapo shilingi bilioni 134.7

zimetolewa kwa wanafunzi 119,073;Taasisi ya Mifupa Muhimbili:kukamilika kwa ujenzi wa jengo la ghorofa 7 litakalokuwa na sehemu za kutolea huduma pamoja na malazi kwa wagonjwa;Hospitali ya Rufaa kanda ya kati Singida:kuendelea na ujenzi wa hospitali;Hospitali ya Bugando:kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la tiba ya mionzi;Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili– Kampasi ya Mloganzila:kuendelea na ujenzi wa ghorofa ya 9 ya jengo la hospitali ya kufundishia;

Hospitali ya Kisasa ya Benjamin Mkapa Dodoma:kukamilika kwa ujenzi wa hospitali kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na tiba ya magonjwa, pamoja na tafiti na mafunzo kwa wanafunzi wa afya wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Utalii

17. Mheshimiwa Spika,Serikali iliendelea na usanifu wa ujenzi wa Utalii House awamu ya pili eneo la ubalozi wa zamani wa Marekani na kuboreshwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato ya utalii, uwindaji na upigaji picha. Aidha, idadi ya watalii kutoka nje imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi 1,140,156 mwaka 2014; na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Kimarekani bilioni 1.86 mwaka 2013 hadi bilioni 2.01 mwaka 2014.

Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

18. Mheshimiwa Spika,Serikali imekamilisha ujenzi wa vituo vya utoaji huduma za pamoja mipakani vya Sirari/Isebania, Holili/Taveta, Mtukula/Mutukula (Tanzania na Uganda), Rusumo (Tanzania na Rwanda) na Horohoro/Lungalunga (Tanzania na Kenya), ambavyo vimeanza kutoa huduma. Vile vile, usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Tunduma/Nakonde (Tanzania na Zambia) umekamilika na ujenzi unatarajia kuanza Mei 2016 ambapo utagharamiwa naTradeMark East Africa. Aidha, ujenzi wa kituo cha Songwe/Kasumulu (Tanzania na Malawi) upo katika hatua ya kuanza usanifu wa kina. Vituo hivyo vinasaidia kupunguza usumbufu na muda wa kuhudumia mizigo mipakani, hivyo kurahisisha biashara kati ya nchi yetu na nchi jirani na kuongeza mapato ya Serikali.

USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI

19. Mheshimiwa Spika,Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili miradi 704 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 11.9 mwaka 2014 ikilinganishwa na miradi 885 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 88.2 mwaka 2013. Kupungua kwa idadi ya miradi kulitokana na uwekezaji mdogo katika sekta ya kilimo na ufugaji, utalii, majengo na biashara. Aidha, fursa za ajira zilizopatikana kutokana na miradi iliyosajiliwa mwaka 2014 zilikuwa 68,442 ikilinganishwa na fursa za ajira 202,487 mwaka 2013. Kati ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2014, miradi ya wageni ilikuwa 213, miradi ya wazalendo ilikuwa 323 na miradi ya ubia ilikuwa 168. Pamoja na kuwepo kwa uwekezaji kutoka nje, takwimu hizi zinaashiria ushiriki mkubwa wa sekta binafsi ya ndani katika uwekezaji katika miradi ya maendeleo.

CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI

20. Mheshimiwa Spika,changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango ni:-

(i)Upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo;

(ii)Taratibu ndefu na gharama kubwa za ununuzi wa umma;

(iii)Madeni, hususan ya wakandarasi wa ujenzi wa barabara;

(iv)Urasimu wa upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji na hati miliki;

(v)Upatikanaji wa fedha za kulipa fidia na mapungufu katika taarifa za tathmini ya fidia;

(vi)Bajeti ya maendeleo kutegemea kwa kiwango kikubwa misaada na mikopo kutoka nje;

(vii)Mchango mdogo wa sekta binafsi katika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;

(viii)Mazingira yasiyo wezeshi kwa uwekezaji na uendeshaji biashara; na

(ix)Uhaba wa miundombinu wezeshi (barabara, maji na umeme) ya kuwezesha utekelezaji wa miradi.

Hatua za kukabiliana na changamoto

21. Mheshimiwa Spika,hatua za kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na:-

(i)Kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa wakati, hususan fedha za miradi ya Matokeo Makubwa Sasa na miradi ya Kitaifa ya Kimkakati;

(ii)Kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi au uwekezaji wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma;

(iii)Kupanua ushirikishwaji wa jamii katika hatua zote za maandalizi ya Mpango ili kurahisisha utekelezaji;

(iv)Kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara ili kuchochea uwekezaji, hususan wa viwanda;

(v)Kuendelea kuimarisha miundombinu wezeshi katika maeneo ya mradi;

(vi)Kuweka mfumo wa utoaji taarifa mapema kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ili zitafutiwe ufumbuzi haraka; na

(vii)Kuweka mfumo wa kuharakisha utoaji wa hatimiliki za ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

MAENEO YA VIPAUMBELE 2016/17

22. Mheshimiwa Spika,baada ya kuzingatia maoni ya wadau pamoja na taarifa mbalimbali kama nilivyoainisha hapo awali, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 utakuwa na vipaumbele vifuatavyo:-

Viwanda

23. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2016/17, maeneo ya vipaumbele ni: viwanda ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake inapatikana nchini, hususan kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili nyingine; viwanda vya kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi nchini, kama vile nguo, viatu na mafuta ya kupikia; na viwanda vinavyotumia teknolojia ya kati na kuajiri watu wengi.

Miradi Mikubwa ya Kielelezo

24. Mheshimiwa Spika,Miradi Mikubwa ya Kielelezo (flagship projects), ili kuchochea ukuaji wa uchumi. Baadhi ya miradi hiyo ni: (i) uendelezaji wa maeneo maalum ya uwekezaji (SEZ) ya Bagamoyo, Mtwara, Kigoma na Kurasini; (ii) mji wa kilimo Mkulazi; (iii) kiwanda cha chuma cha Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma; (iv) ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango chastandard gauge; (v) kujenga msingi wa viwanda vya kuzalisha mitambo, nyenzo na malighafi za uzalishaji; (vi) kuimarisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo katika maziwa makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) ikiwa ni pamoja na ununuzi wa meli mpya, na kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya; (vii) kuanza maandalizi yatakayowezesha mradi wa ujenzi wa mtambo wa kusindika gesi kimiminika (Liquified Natural Gas- LNG plant) Lindi; na (viii) kusomesha vijana wengi, hususan, katika fani zitakazohitajika zaidi za mafuta na gesi, uhandisi, kemikali, tiba na afya.

Maeneo Wezeshi kwa Maendeleo ya Viwanda 25. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2016/17,maeneo wezeshi kwa maendeleo ya viwandani pamoja na: miundombinu ya nishati, reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, maji (kwa mahitaji ya viwanda) na mkongo wa Taifa wa mawasiliano. Aidha, itajumuisha kilimo (uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi) kwa kuwa ni nguzo ya msingi katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na malighafi za uzalishaji viwandani. Katika eneo hili, msisitizo utawekwa katika miradi iliyoanza kutekelezwa katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16.

Kufungamanisha Maendeleo ya Viwanda na Maendeleo ya Watu

26. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2016/17, Serikali itaweka msisitizo mkubwa katikakufungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu. Maeneo mahsusi yanayopendekezwa kutekelezwa ni pamoja na: kuhakikisha usalama wa chakula; afya ikiwemo kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa dawa kwa wananchi; kuimarisha elimu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu msingi bila malipo, kuimarisha ubora wa elimu kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa walimu walio kazini, kuongeza matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji, kuandaa mfumo endelevu wa ugharamiaji, na kuimarisha mifumo ya ithibati na udhibiti;

usimamizi na upatikanaji wa maji safi na huduma za majitaka, nishati ya uhakika, upatikanaji wa ajira, hifadhi ya jamii, usawa wa jinsia na watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maeneo Mengine

27. Mheshimiwa Spika,Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamebainisha maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa. Maeneo hayo ni pamoja na: utalii, misitu na wanyamapori; madini; hali ya hewa; ushirikiano wa kikanda na kimataifa; na utawala bora. Katika eneo hili msisitizo utawekwa katika kukamilisha miradi ambayo utekelezaji wake ulianza katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16).

UGHARAMIAJI WA MPANGO

28. Mheshimiwa Spika,Sekta binafsi itakuwa mtekelezaji mkuu wa Mpango huu. Serikali itakuwa na wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi ichangie kikamilifu katika utekelezaji wa Mpango. Aidha, katika bajeti ya maendeleo ya mwaka 2016/17, Serikali inakusudia kutenga kiasi cha shilingi bilioni 6,182.2 ili kutekeleza miradi ya maendeleo, ambapo fedha za ndani ni shilingi bilioni 4,810.1 sawa na asilimia 77.8 ya bajeti ya fedha za maendeleo. Vile vile, Serikali itawekeza mitaji katika benki za Uwekezaji Rasilimali (TIB) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuvutia fedha za mikopo ya masharti nafuu kutoka taasisi za fedha za ndani na nje kugharamia miradi ya maendeleo.

UFUATILIAJI, TATHMINI NA UTOAJI WA TAARIFA

29. Mheshimiwa Spika,Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 utazingatia mfumo na mwongozo utakaotumika katika ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo. Mfumo huo wa ufuatiliaji na tathmini utatekelezwa kwa kuweka malengo ya utekelezaji kwa kila sekta kwa mwaka na kuandaa mpango kazi wa mwaka. Utaratibu wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo utazingatia Mwongozo wa Mpango na Bajeti wa Mwaka 2016/17 na Mwongozo wa Uandaaji na Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management – Operational Manual) wa Mwaka 2015. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha idara za ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo ili miradi iliyoanzishwa iweze kuleta tija kwa Taifa.

30. Mheshimiwa Spika,Wizara ya Fedha na Mipango itafuatilia na kutathmini miradi ya Kitaifa ya kimkakati na mingine muhimu kwa ukuaji wa uchumi kwa kushirikiana na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali. Aidha, itachambua taarifa za ufuatiliaji na tathmini na kutoa mwelekeo wa maeneo ya kuboresha utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya Kimkakati na Matokeo Makubwa Sasa. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya Matokeo Makubwa Sasa utafanyika kwa kuzingatia mfumo huo.

VIHATARISHI VYA UTEKELEZAJI WA MPANGO

31. Mheshimiwa Spika,Vihatarishi mbalimbali vinaweza kujitokeza katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vihatarishi hivyo ni pamoja na: upatikanaji wa mikopo kwa wakati, riba kubwa, masharti magumu na utayari wa Washirika wa Maendeleo kutoa fedha za misaada kwa wakati; mfumuko wa bei unaotokana na kuongezeka kwa bei za chakula, nishati, vifaa vya ujenzi na vipuri katika soko la ndani na nje na hivyo kuongeza gharama za miradi; thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni hususan dola ya Kimarekani kuendelea kushuka na hivyo kusababisha gharama za uagizaji bidhaa na huduma za miradi kuwa kubwa. Vihatarishi vingine vya utekelezaji wa Mpango ni: uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zinaathiri uendelevu wa rasilimali asili na ikolojia; mahitaji ya nguvukazi yenye ujuzi; teknolojia; na ucheleweshwaji katika ununuzi wa umma.

32. Mheshimiwa Spika,Serikali kwa kushirikiana na wadau itakabiliana na vihatarishi kwa kuchukua hatua zifuatazo:- kupunguza utegemezi kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali na kuharakisha urasimishaji wa sekta isiyo rasmi; kuongeza kasi ya upatikanaji wa mikopo na misaada yenye masharti nafuu; kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara; kupunguza kiwango cha mikopo ya ndani kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi na kutoa fursa kwa sekta binafsi kukopa zaidi kwa ajili ya uwekezaji; na kuendelea kutoa elimu ya namna bora ya utekelezaji ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika miradi ya Maendeleo.

USHIRIKISHWAJI WA WADAU

33. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamezingatia maoni ya Wizara, Idara, na Taasisi za Serikali na Sekta binafsi. Masuala makuu ya maoni ya wadau yaliyojitokeza na kujadiliwa ni pamoja na: umuhimu wa kuandaa maeneo ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na kuendeleza viwanda vilivyopo; upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kutoka nje; na kuboresha miundombinu (maji, umeme na barabara) ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika viwanda nchini. Maoni na ushauri huo utazingatiwa wakati wa kuandaa Mpango wenyewe wa mwaka 2016/17.

RATIBA YA UTEKELEZAJI

34. Mheshimiwa Spika, baada ya kupata maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 utaandaliwa na kuwasilishwa Bungeni Juni, 2016 ambapo utekelezaji wake utaanza Julai, 2016 hadi Juni, 2017.

HITIMISHO

35.Mheshimiwa Spika,naomba nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 vinapatikana katika tovuti za Wizara ya Fedha na Mipangowww.mof.go.tznawww.mipango. go.tz.

36.Mheshimiwa Spika,baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu likae kama kamati ya Mipango na kujadili Mapendekezo niliyowasilisha, ili Serikali iweze kunufaika na ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Serikali itazingatia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na kuyafanyia kazi ipasavyo wakati wa maandalizi ya Mpango.

37.Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


Soma hapa MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17
 

Attachments

  • frame work.pdf
    324.5 KB · Views: 59
Nadhani hili lisiwe kwa Mabalozi! Wawakilishi watatusaidia ! Toka nyumba za Serikali ziuzwe watumishi wengine wamekuwa wakikaa nyumba za kupanga au Mahotelini hapa hapa nyumbani. Nadhani wakati wa mjadala waheshimwa wataliona hili.
Ni vizuri waraka na miongozo ya Serikali iwe wazi kwa Umma-hatua hii inasaidia usimamizi wa pamoja .Usiri kwenye uendeshaji wa Shughuli za Umma muda mwingine ndiyo chanzo cha matatizo mengine.



Mipangowww.mof.go.tznawww.mipango. go.tz.
6.3
Hatua za kudhibiti matumizi
m)
Kutumia fursa za mikopo ya nyumba (mortgage facility) katika upatikanaji wa majemgo ya balozi na wawakilishi walioko nje ya nchi badala ya utaratibu wa kupanga
pg.16

r)
Kuzingatia maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kwa Waraka Na.CAC.134/213/01/K/114 wa tarehe 26 Septemba 2012, kuhusu kudhibiti ununuzi
wa samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi;
 
DONT YELL ARGUE....!!!
Yote yamo humu humu kwa nini tu wavivu wa kusoma?
Soma kipengele cha 31
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…