UFAFANUZI KUHUSU UHUSIANO WA FAO LA KUJITOA NA UWEKEZAJI WA MIFUKO KWENYE VIWANDA
_______________________
1.0. FAO LA KUJITOA
Kumekuwa na minong’ono na hofu kwamba mapendekezo ya marekebisho ya Sheria za Mifuko yanalenga kuondoa fao la kujitoa ili kuwezesha utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya jamii kuwekeza katika viwanda. Fao la kujitoa katika mifuko ya Hifadhi ya jamii ilifutwa kupitia Sheria Na. 5 ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii mwaka 2012. Pamoja na mambo mengine Sheria hii ilifuta utaratibu wa wanachama kujitoa na kuchukua michango yao katika Mfuko wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko ya Pensheni wa (PPF). Hata hivyo utekelezaji wa marekebisho hayo ulisitishwa Oktoba 2012 mpaka pale utaratibu mbadala wa fao hilo utakapoandaliwa. Tangu wakati huo mpaka sasa jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili. Jitihada hizo ni pamoja na kufanya tathimini ya mifuko yote ili kujiridhisha endapo itamudu kutoa fao mbadala kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi wa wananchi.
Aidha, maelekezo ya Serikali kuhusu ushiriki wa Mifuko katika viwanda yalitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli wakati wa uzinduzi wa Bunge la 19 la Jamhuri ya Muungano. Maelekezo haya yalitiliwa tena msisitizo na Mhe. Rais wakati wa uzinduzi wa majengo ya Mifuko ya PPF na NSSF Jijini Arusha mnamo tarehe 11 Mei, 2012.
Hivyo, si kweli kwamba jitihada za Serikali kutafuta ufumbuuzi wa fao la kujitoa zinalenga kuwezesha utekelezaji wa mifuko kuwekeza katika sekta ya viwanda. Ni muhimu pia kutambua kwamba mfumo wa hifadhi ya jamii unalenga kuwalinda Wafanyakazi dhidi ya majanga yatokanayo na umasikini wakati wa uzee, kwa kuhakikisha wastaafu wanapata mafao bora. Madhara yatokanayo na fao la kujitoa ni makubwa ikiwa ni pamoja na mwanachama anaejitoa kukosa sifa za kupata pensheni pale anapostaafu na hivyo kwenda kinyume na malengo ya kuwepo kwa hifadhi ya jamii. Uzoefu unaonyesha kwamba wanachama wanaojitoa mara nyingi hurudi serikalini kuomba kulipwa pensheni.
2.0. UWEKEZAJI KATIKA VIWANDA
Kwa mujibu wa Miongozo ya Uwekezaji yam wa 2012 kama ilivyofanyiwa mapitio, mifuko inaweza kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwepo eneo la viwanda. Mifuko imekuwa ikiwekeza katika viwanda kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia Mikopo (syndicated loans) ambapo Mifuko inaweza kutoa mikopo kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za fedha. Mifano ya ushiriki wa Mifuko katika uwekezaji wa namna hii ni katika viwanda vya Kagera Sugar, TANESCO, 21st Century na Tanzania Pharmaceuticals Industries ambapo Mifuko ilitoa mikopo ya moja kwa moja ikishirikiana na Taasisi nyingine za fedha. Mifuko pia inaweza kuwekeza kupitia Hati Fungani (Corporate Bond) kama walivyofanya kwa Benki ya Barclays; Kampuni ALAF na TBL.
Mifuko imekuwa ikiwekeza kuwekeza kwenye viwanda katika mfumo wa majengo. Kwa mujibu wa miongozo ya uwekezaji, Mifuko inaruhusiwa kuwekeza katika eneo hili hadi asilimia 30 ya rasilimali zake.
Hivyo, suala la uwekezaji katika viwanda si suala geni na wala halina uhusiano na mapendekezo ya kuondoa fao la kujitoa.
Pamoja na mambo mengine inaainisha mambo makuu manne ya kuzingatia ili kuhakikisha kwa uwekezaji unaofanywa na mifuko unakuwa na tija wa wanachama na kuleta uendelevu wa mifuko. Mambo hayo ni:
i. Usalama wa michango (Safety). Uwekezaji ni lazima kuhakikisha kwamba kila shilingi inayowekezwa kwenye miradi inakuwa salama na inabaki kama shilingi.
ii. Kuzalisha (Yield). Kila kiasi cha fedha kinachowekezwa ni lazima kizae na kutengeneza faida.
iii. Ukwasi au uwepo wa fedha tasilimu kila wakati (Liquidity); ni lazima Mifuko inapowekeza kuhakikisha kwamba inabakiza fedha za kutosha kulipa mafao kadiri yanavyoiva na mahitaji mengine.
iv. Kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali (Diversification). Mifuko inazuiwa kuwekeza katika eneo moja badala yake inapaswa kuwekeza kwenye vitega uchumi mbalimbali ili kujikinga na athari (Risk Management).
v. Kuwekeza kwenye maeneo yenye tija kwenye jamii inayo zunguka Mradi (Social economic utility). Msingi huu unatilia mkazo kuwekeza maeno ambayo yanaboresha maisha ya jamii iliyokaribu na eneo la Mradi. Vile vile huweza kusaidia uchumi wa nchi kwa ujumla
1.0 FAIDA ZAKE
Uwekezaji wa Mifuko ya hifadhi ya jamii katika viwanda juu una faida zifuatazo:
(i) Kuiwezesha Mifuko kulipa mafao kwa wanachama wake kwa mujibu wa sheria
(ii) Uwekezaji katika viwanda utasaidia kukua kwa Sekta ya viwanda na hivyo kuongeza ajira na hatimaye kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla
(iii) Kuwekeza kwa njia ya hati fungani au hisa kutawezesha Mifuko kuuza hati hizo katika soko la mitaji pale watakapohitaji fedha taslimu kwaajili ya kulipa mafao;
(iv) Kukuza Soko la Mitaji na hivyo kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa gharama nafuu;