Mystery
JF-Expert Member
- Mar 8, 2012
- 15,843
- 31,049
Huu ukiwa ni mwaka wa 4 mfululizo shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) limeendelea kumwalika Rais Magufuli kwenye sherehe zao na kumfanya kuwa ndiye mgeni rasmi kwenye sherehe hizo
Hata hivyo Rais Magufuli katika mialiko yote hiyo amekuwa akipiga danadana dai lao kuu vyama vya wafanyakazi la kuwaongezea kima cha chini kutokana na ugumu wa maisha wanayokabiliana nayo
Tumeshuhudia katika sherehe zilizoisha hivi majuzi, Rais Magufuli akilihamisha Baraza lake la mawaziri na kulipeleka pale Mbeya na kufanya kampeni ya nguvu kwa chama chake cha CCM
Tumeshuhudia pia convoy ya misafara yake ikiwa na magari yasiyopungua 100, huku ikitafuna pesa za walipa kodi wa nchi hii kuyahudumia katika mafuta na posho wanazolipwa hao watumishi ambazo ni mamilioni ya shilingi za kitanzania
Sisi wafanyakazi wa nchi hii tunapomwalika kiongozi yeyote kwenye sherehe hizo tunategemea kiongozi huyo ajisikie uchungu na madhila yanayowapata wafanyakazi wanyonge wa nchi hii na wala siyo kusikia kiongozi huyo akijinadi kuwa tunatekekeza miradi mikubwa ya reli ya standard gauge, mradi wa kuzalisha umeme kutoka mto Rufiji na ununuzi wa madege ya mabombedier.
Tujiulize swali moja hivi nchi za wenzetu ambazo miundobinu yao ni ya hali ya juu sana kulinganisha na ya kwetu, hivi nao waliwapigisha "mark time" bila kuwaongeza mishahara wafanyakazi wao kipindi hicho cha ujenzi wa hiyo miundo mbinu yao??
Nakumbuka katika awamu iliyopita ya uongozi wa TUCTA chini ya Katibu Mkuu wake Nicholas Mgaya waliwahi kumwambia Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete, kuwa iwapo hutakuja kwenye sherehe zetu bila kuzingatia kilio cha wafanyakazi, basi ni vyama tukamweka mgeni rasmi mtu yeyote yule ambaye tunafahamu atapigania maslahi ya wafanyakazi wanyonge wa nchi hii
Imethibitika dhahiri kuwa Rais Magufuli hajali kabisa mateso wanayopata wafanyakazi wanyonge wa nchi hii
Ndipo hapo sasa nawauliza viongozi wa TUCTA kuwa kuna haja gani ya kuendelea kumwalika Rais Magufuli katika sherehe za Mei Mosi, wakati mkijua hayupo tayari kuwapunguzia machungu wanayopata wafanyakazi wanyonge wa nchi hii??
Sherehe za Mei Mosi ni zenu shirikisho la vyama vya wafanyakazi, kwa hiyo mna hiyari ya kumchagua mtu yeyote ambaye mnaamini kauli zake zitaleta "impact" katika maisha ya wafanyakazi
Ninachopendekeza kwenu viongozi wa TUCTA msimpe tena mwaliko Rais Magufuli kwenye sherehe hizo, mpaka pale atakapokuwa tayari kuongeza mishahara ya kima cha chini
Kama aliweza kufanya hivyo Katibu Mkuu aliyepita Nicolas Mgaya kwa Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete, ni kitu gani kinawashinda nyinyi viongozi wa sasa wa TUCTA kumtilia ngumu Rais Magufuli kuja kwenye sherehe zenu akiwa mgeni rasmi??