- Ada za shule, kodi za nyumba, ufahari wa kutunza kwenye sherehe ndiyo chanzo cha masahibu
- Mwanamke mmoja anaweza kujiunga Vicoba saba
- Wengi hawakopi kwa ajili ya biashara
- Wengine wanakopa kwa siri, waume zao hawajui hadi siku ya kuzolewa vyombo vya dhamana
KUMEKUWA na wingu zito kuhusu mikopo wanayokopa wanawake, hususan wake za watu katika miji mikubwa nchini kutoka kwenye Vicoba na taasisi mbalimbali za kifedha vikitajwa kuwa ni chanzo kikuu cha migogoro ya kifamilia na magonjwa ya msongo wa mawazo, kama Kiharusi na Shinikizo la Juu la Damu.
Mbali na magonjwa hayo yasiyokuwa ya kuambukiza na mambo ya kifamilia, yapo madai kwamba, wakopaji wengi wamepoteza vitu, ndoa na wengine kufikishwa mahakamani kwa kukosa uaminifu wa kirejesha fedha. Neno kubwa linalowahangaisha wakopaji wa kwenye Vicoba na taasisi za fedha miaka ya karibuni ni MAREJESHO.
VICOBA NI NINI?
Vicoba ni taasisi ndogo za kukopesha kwa wana vikundi waliyoungana kwa idadi fulani. Vicoba ni kifupi cha Kiingereza, Village Community Bank.
Hivyo, Vicoba ni utaratibu wa kuweka na kukopa kwa watu waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Utaratibu huu ulianza nchini miaka ishirini na moja iliyopita na umeonesha mafanikio makubwa kwa baadhi ya wanavikundi wake kuweza kukopeshana, kusaidiana katika matatizo mbalimbali, kuanzisha miradi ya pamoja ya kiuchumi. Lakini pia, Vicoba imekuwa mwiba kwa wanakikundi ambao siyo waaminifu.
Madhumuni ya mwanzilishi wa Vicoba ilikuwa ni kuunganisha nguvu na rasilimali za wanachama ili kuondoa umaskini na kuleta maendeleo kwa kuchangia mifuko ya jamii, kuendesha mfuko wa kuweka na kukopa, kushiriki katika mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara, uongozi na uanzishaji wa shughuli mbalimbali za pamoja za maendeleo.
Kawaida wana Vicoba humaliza mzunguko wao baada ya miezi kumi na mbili (12) na kufanya tathmini ikiwemo kugawana makusanyo na faida na kisha kuvunja kikundi ili kuanza mzunguko mwingine mpya.
Gharama za uendeshaji wa Vicoba ni ndogo kwani hakuna ofisi, mara nyingi wana kikundi huchagua mahali pa kukutana kwa muda usiyozidi saa moja. Maeneo mengi ya kukutana huwa baa au pia nyumbani kwa mmoja wa wanavikundi.
Mfumo wa Vicoba ni mzuri hasa kwa dhana ya kuanza kidogo ili kuwa na kitu kikubwa baadaye. Licha ya kujihusisha na kuweka na kukopa, wanakikundi husaidiana katika matatizo mbalimbali, kama vile misiba, ugonjwa na matatizo mengine ya kijamii. Wakati mwingine hata sherehe.
Lakini kuna Vicoba vinavyomilikiwa na mtu mmoja mwenye fedha zake, akiweka waalimu wa kutafuta wanachama na kuwafundisha kisha kuweka akiba kwa kiwango fulani halafu kukopesha.
Mtanzania George Sevetta, mzaliwa wa Lupembe, Njombe ndiye anatajwa kuwa mwanzilishi wa Vicoba nchini mwaka 2000 akiita ni Benki za Jumuiya Vijijini au Village Community Bank. Alianzia maeneo ya Kisarawe mkoani Pwani na Ukonga, Dar es Salaam na baadaye wengi kuyatumia mawazo yake hayo na kuenea kote Tanzania.
TAASISI ZA FEDHA NI NINI?
Inawezekana hata Vicoba pia ikawa ni taasisi ya kukopesha fedha. Lakini zipo taasisi ambazo siyo Vicoba, zikijipa majina mengine na zinamilikiwa na mtu mmoja au wawili ambapo, masharti yao ya mikopo ni pamoja na ahadi ya kubebewa vyombo mkopaji akishindwa kurejesha fedha alizokopa.
WAKOPAJI WAKUBWA WA VICOBA
Wanawake, hususan wake za watu, ndiyo kundi kubwa linalotajwa kujiunga kwenye Vicoba, licha ya wanaume wachache nao kuwepo kwa misingi ya kujiongezea kipato.
Hata hivyo, uchunguzi wa mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, wanawake wengi wamekuwa wakijifunga kwenye mikopo ya Vicoba kwa kuchukua fedha nje na maelezo ya kwenye makaratasi ya kujieleza.
Sera za Vicoba karibu vyote vilivyotapakaa nchi nzima, zinamtaka mkopaji kujaza fomu yenye maelezo kamili, hasa kipengere cha SABABU za mkopo ambapo kipaumbele kikubwa ni kukuza biashara ambayo tayari ipo au kuanzisha mpya yenye uchambuzi unaokubalika.
SIFA ZA MKOPAJI VICOBA
Inapofika muda wa mwanakikundi kutaka mkopo, hutakiwa kuonesha mahali anapoishi kwa wakati huo, samani alizonazo na wadhamini wasiyopungua wawili. Ikibidi mmoja ambaye ni mwanachama wa siku nyingi na awe ameshachukua mkopo na kulipa bila usumbufu wowote.
Lakini ni baada ya mwanakikundi huyo kuweka akiba ya fedha kwa kiwango kilichokubalika kisera.
Aidha, baadhi ya Vicoba hutaka wanakikundi kuwasilisha barua kutoka ofisi ya Serikali ya Mtaa, ikiwa na muhuri, saini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, picha ya mkopaji, namba za Kitambulisho cha Taifa (Nida) au Kitambulisho cha Mpiga Kura ili kuonesha kuwa, mhitaji huyo anatambulika rasmi hivyo, hatasumbua kwenye marejesho. Vicoba vingine havihitaji.
Uchunguzi wa hivi karibuni umebaini kwamba, sababu nyingi zinazojazwa kwenye fomu za mwanakikundi mkopaji ni za kumridhisha mtoa mkopo, hasa ya KUENDELEZA BIASHARA ili aweze kutoa kwa urahisi akiamini pesa zake zitarudi kwa kuwa zinakwenda kuzalisha.
CHANZO CHA MAHANGAIKO
Hata hivyo, imegundulika kuwa, mwezi mmoja baada ya mwanakikundi kupewa mkopo, ukakasi kwenye MAREJESHO huanza kutamalaki kwani wengi waliyochukua mikopo huzitumbukiza fedha hizo kwenye matumizi ya kutoa tu bila kuingiza (siyo biashara).
Uchunguzi unaonesha kuwa, katika kila wakopaji 20, 15 hawana biashara hata ya genge la kuuza nyanya, achilia mbali maduka ya kuuza nguo, saluni za kike, kusafirisha bidhaa, kama wanavyojaza kwenye makaratasi ya kuombea mkopo.
Aidha, imebainika kuwa, pesa nyingi za mikopo ya Vicoba na taasisi nyingine za kifedha, zinatumika kwenye ada za wanafunzi mashuleni (hasa shule binafsi), kodi za nyumba huku baadhi ya wanawake wakitajwa kuwa hufanya fahari kwa manunuzi ya vitu vya kutuza kwenye sherehe mbalimbali, zikiwemo Kitchen Party, Baby Shower na kumtoa mtoto nje mchanga maarufu kama 40.
Baada ya matumizi hayo, imebainika kuwa, marejesho hushindwa kufanyika kwa usahihi kama makubaliano ya kwenye mikataba inavyosema na ndipo mwanakikundi huweza kukacha vikao vya marejesho na ufuatiliaji wa makarani na maafisa wa Vicoba au taasisi za mikopo huanza hapo mpaka kufikia hatua ya samani za ndani kuchukuliwa kama masharti yanavyotaka.
MWANAMKE MMOJA KUSHIRIKI VICOBA SABA
Mama Baraka, mkazi wa Mtaa wa Songea, Ilala jijini Dar es Salaam, alikiri kuwepo kwa mtifuano kwenye marejesho ya mikopo kwenye Vicoba na taasisi nyingine za fedha.
"Ukweli ni huu nitakaokwambia mimi. Ni kweli wanawake wangi tunakopa kwenye Vicoba na taasisi nyingine za fedha. Ila matumizi ya zile fedha ndiyo tatizo. Mfano mimi nina Vicoba saba. Kisa cha kuwa na Vicoba vyote hivyo ni kutafuta pesa za kulipa madeni sehemu nyingine.
"Niliingia Vicoba ya kwanza mwaka jana, nilipewa mkopo wa shilingi laki tano (500,000). Nikafanyia sherehe ya harusi ya mdogo wangu ambaye alitakiwa kuolewa kabla ya Ramadhan ya mwaka jana haijaanza.
"Sasa kivumbi kikawa kwenye marejesho. Sina biashara yoyote, nategemea 'kodi ya meza' kutoka kwa mzee. Na kila wiki lazima nirejeshe pesa. Ilibidi pesa ninazopata niweke akiba Vicoba nyingine ya pili, nikakopa ili kurejesha mkopo wa Vicoba ya kwanza. Mchezo ukawa huo, nakopa Vicoba hii nalipa Vicoba ile," anasema mama Baraka.
Mwandishi:"Umesema una mume, kwa nini usimshirikishe pale ulipoona umebanwa na wakopeshaji mpaka kutishia kuchukua vitu nyumbani?"
Mama Baraka: "Sikumwambia mume wangu kama nilichukua mkopo. Sikupenda ajue kwa sababu hakubaliani na mikopo yenye masharti ya kubebeana vitu nyumbani. Na ndiyo maana najikuta naingia Vicoba vingi ili nilipe madeni maana wanaodai ukipitisha marejesho muda mrefu wanakufuata nyumbani kuzoa vitu. Sasa fikiria, mume hajui halafu ghafla anaona gari linakuja kuchukua vitu. Pana ndoa hapo kweli?"
Aidha, mama Baraka aliendelea kudai kuwa, wanawake wenzake wengi ambao wapo kwenye ndoa, wamejiunga kwa siri kwenye Vicoba na taasisi za fedha bila waume zao kutambua mpaka ikitokea siku maafisa wamefika nyumbani kuchukua vitu ndipo siri hufichuka.
Amesema kuwa, ana ushahidi wa dada wa mumewe (hakumtaja jina), mkazi wa Kawe, Dar es Salaam, aliachika kwa talaka baada ya mumewe kukuta sebule nyeupe, akiambiwa kwamba, Vicoba wamechukua samani zote na kuacha picha za ukutani tu.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi umegundua kuwa, wanawake wengi wanaochukua mikopo Vicoba, taasisi za fedha, wamekuwa wakitaabika kwa 'ubize' wa siku nzima za siku saba za wiki wakihudhuria vikao mbalimbali kwa Vicoba mbalimbali ili kutunza uwakilishi wao na pia kutunza siri kwa waume zao wasijulikane wapo Vicoba kwa vile matumizi ya pesa zao, hazikupita 'meza kuu' (kwa waume).
Baadhi ya wanawake wako bize kiasi cha kukosa muda wa kuangalia familia kutokana na muda mwingi kushughulikia mambo ya Vicoba na taasisi za fedha 'wakikimbizana' na tarehe za marejesho.
Wanawake wengi waliyoongea na mwandishi wetu walikiri kutaabishwa na mikopo ya Vicoba na taasisi za fedha wakisema kuwa, wamekuwa wakijikuta wanatoka majumbani asubuhi ya mapema na kurudi jioni kama wafanyakazi waliyoajiriwa.
Baadhi yao, wamekuwa wakipanda daladala wakiwa na watoto wachanga kana kwamba wanakwenda Kliniki, lakini kumbe wanahudhuria vikao vya Vicoba ambavyo vingi hufanyika Jumanne, Jumatano, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Ugumu wa marejesho unapozidi kiasi cha kutishia mambo kujulikana kwa waume zao, ndipo wengi hupatwa na msongo wa mawazo (stress) mpaka kufikia hatua wengine kupata kiharusi na presha kwa vile maswali mengi kutoka kwa wanaume ni wapi pesa za mkopo zilikwenda? Maswali haya huambatana na ugomvi wa wivu wa mapenzi.
Lakini imegundulika pia baadhi ya wanandoa (mke na mume), wamekuwa wakishirikiana kukopa Vicoba na taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kulipia ada za shule, kodi za nyumba, michango ya harusi na mambo mengine yanayofanana na hayo huku, jina la mke likisimama mbele ya mkopo husika.
MAMBO YA KUBORESHA NI HAYA
Julieth Mwaimu, yeye ni mwalimu wa Vicoba Afya, yenye makao makuu yake, Mbagala, Dar, alikiri uwepo wa wateja ambao, hawana kipato, kama vile biashara, ndiyo maana kwenye marejesho kunaibuka matumizi ya nguvu ikiwemo kuchukua vitu.
"Mtu anakopa hela lakini hana kipato chochote, anategemea mumewe akitoa hela ya matumizi, abanebane ndiyo apate hela ya marejesho. Sasa wakati mwingine mumewe kipato kinagoma. Ndipo taharuki huanzia hapo."
Kuhusu wakopaji wengi kudanganya kwenye makaratasi madhumuni ya mkopo, Julieth alisema:
"Ni kweli, baadhi ya Vicoba, hata hawataki kujua mwanakikundi anapeleka wapi pesa anazokopa. Matokeo yake ndiyo hayo, kuwindana. Lakini Vicoba yangu mimi hapana. Tunataka kujua matumizi ya pesa ili ikibidi tutoe ushahuri au elimu kwa mkopaji.
"Tumekuwa tukiwashauri wakopaji kubadilisha biashara kulingana na maeneo. Na kweli wamefanikiwa hata kurejesha mikopo bila usumbufu wowote. Vicoba yangu haina historia ya kuchukua samani za mwanakikundi kwa vile nawasimamia vilivyo."
Aidha, Julieth aliwashauri wamiliki wengine wa Vicoba kubadili muundo wa kukopesha ili kupunguza kama siyo kuondoa kabisa matatizo.
"Kwanza; mwanakikundi awe na biashara yenze kuzingatia maeneo na mazingira yanayoendana na biashara. Pili; kumfuatilia mwanakikundi kwenye biashara yake kila mara ili kuangalia maendeleo na kushauri ikibidi. Tatu; biashara ya kumkopesha mtu iwe hai. Siyo mtu akope pesa kwa ajili ya kwenda kuanzisha biashara mahali ambapo mazingira hayakubali.
"Nne; hili bado nalifikiria tu. Wenye Vicoba tuwe na mawasiliano ya kimtandao. Mtu akikopa kwangu, na kwao wenzangu wajue kwamba amekopa. Wasumbufu wengi ni wale wenye Vicoba zaidi ya viwili."
Suzan Jonas, mkazi wa Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam, yeye alisema kuwa ana Vicoba vitatu, akiweka wazi kwamba, ugumu wa marejesho ya Vicoba, wa kulaumiwa ni wamiliki wenyewe kwani riba imekuwa kubwa, muda wa marejesho ni mfupi na kiwango cha chini cha mkopo ni kidogo sana.
"Mkopo wa kwanza unaniambia nichukue shilingi laki tano. Muda wa kurejesha miezi mitatu. Riba asilimia ishirini. Nini kitatokea?" alihoji mwanamke huyo.
DAKTARI ATIA NENO
Kuhusu baadhi ya wanawake kupatwa na magonjwa yatokanayo na msongo wa mawazo, daktari mmoja wa Dr. Chale Clinic iliyopo, Mbezi Kwamsuguru, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Dk. Chale, alikiri kuwepo kwa wagonjwa wa Kiharusi na Shinikizo la Juu la Damu ambao historia zao zinaonesha kuwa, chanzo kikubwa ni msongo unaochangiwa na madeni kutoka kwenye taasisi zinazokopesha fedha.
"Unajua iko hivi, mtu yeyote aliyepata magonjwa hasa haya yasiyoambukiza, kama kiharasi au shinikizo la juu la damu, kitaalamu, lazima umuulize historia ya maisha yake. Kazi anayofanya, hali ya uchumi nyumbani hata migogoro ya ndoa.
"Sasa wengi, hasa wenye matatizo ya presha, ukiwauliza wanataja madeni. Mama mmoja aliniambia anadaiwa milioni tano kwenye Vicoba na taasisi mbili za fedha," alisema daktari huyo na kuongeza kuwa, hakuna kitu kinawapa mawazo watu wengi duniani kama madeni.