Mimi kwa uelewa wangu Wakala wa Chama cha Siasa kwenye Uchaguzi ni mtu anayeteuliwa na chama chake na kuwasilisha jina lake Tume kwa ajili ya kusimamia maslahi ya chama chake na mgombea wake wakati wa kupiga Kura, kuhesabu Kura na Kujumlisha. Wakala anayeteuliwa kwa kazi hii anakula kiapo cha kutekeleza majukumu yake chini ya Msimamizi au Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.
Wakala ni mtu muhimu sana wakati wa Uchaguzi, Mgombea anapoteua Wakala atakayesimamia maslahi yake anakua amejiridhisha kabisa kuwa ameteua mtu makini mwenye Sifa zote zikiwemo za za Uteuzi kutoka kwenye Chama chake na kuwa na Kibali cha uteuzi, amekula kiapo cha kutunza Siri, Umri pia ni muhimu awe na miaka 18 na kuendelea pia Awe na Akili Timamu.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 57 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa na Kifungu cha 58 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kwa pamoja na kanuni ya 48 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 na kanuni ya 42 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015 kila Chama cha Siasa chenye mgombea wa nafasi yoyote kinaweza kuteua Wakala wake kwa kila kituo cha kupigia Kura.
Inashauriwa wakala awe ni mkazi wa eneo la kituo anachokisimamia hii inamsaidia wakala kushiriki pia katika Uchaguzi wa ngazi zote tatu za udiwani, ubunge na kiti cha Rais.
MAJUKUMU YA WAKALA, Wakala ana jukumu la Kutambua Wapiga Kura ndio maana anatakiwa awe mkazi wa eneo analolisimamia, Wakala anamwalikisha na kulinda maslahi ya mgombea au wagombea katika kituo na pia Wakala anashirikiana na Msimamizi wa Kituo na Msimamizi Msaidizi wa Kituo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinazohusu upigaji Kura zinafuatwa katika Kituo.
Sote tunakubaliana kuwa Mawakala wa vyama Vya Siasa lazima wawe ni watu Makini na wenye akili Timamu wanaoweza kutekeleza kikamilifu jukumu Kuangalia mchakato mzima wa kpiga Kura, kuhesabu Kura, kujumlisha na kutangazwa matokeo ya Uchaguzi;
Wakala makini anatakiwa Kuwepo katika kituo wakati wa kufungua na kufunga kiyuo pia awepo muda wote wa upigaji wa kura na kuhesabu Kura.
Wakala anao wajibu wa Kuuliza au kutaka maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Kituo juu ya jambo linaloweza kutokea kituoni, katika hili anatakiwa azingatie sheria na kuepuka kutumia lugha za kuudhi, vurugu, nguvu au jambo lolote linaloweza kuzuia au kuvuruga utaratibu unaoendelea kituoni. Mawakala wengi wamekuwa wakichemka hapa wamekuwa wakifanya vurugu vituoni na matokeo yao ni kutolewa nje na kuishia kulalamika. Mwanzo nimesema mgombea au chama kinatakiwa kilete Mawakala makini wenye uwezo wa kuhakikisha maslahi ya vyama vyao yanalindwa na kusimamiwa kwa mujibu wa Sheria.
Wakala au Mgombea Kuridhika au kutoridhika katika Kituo cha kupigia kura.
Ukisoma Kanuni ya 59 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 na kanuni ya 53 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, Wakala au Mgombea atajaza fomu zifuatazo:
Fomu Na. 14 : hii ni Fomu ya Malalamiko au Ridhaa ya Wakala wa Upigaji Kura. Fomu hii hujazwa na Wakala kabla ya kuanza na baada ya kukamilika upigaji kura kuonyesha kuridhika au kutokuridhika na mwenendo wa upigaji kura.
Fomu Na 16: Hii ni fomu ya Malalamiko au Ridhaa ya Mgombea au Wakala. Fomu hii hujazwa na wakala katika hatua za uhesabuji wa kura kuonyesha kuridhika au kutoridhika na utaratibu wa kuhesabu Kura.
Hizi Fomu ni muhimu sana zijazwe, Mawakala wengi wanakimbilia kulalamika kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hawajazi hizi fomu, kwa hiyo hoja zao zinakosa nguvu kisheria na hata wakienda mahakamani wanapoulizwa kama wamejaza hizo fomu au wakiombwa copy ya hizo fomu wanaishia kutoa macho.
Chonde chonde Vyama vya Siasa na Wagombea chagueni Mawakala wenye uwezo wa kutetea Maslahi yenu kwa mujibu wa Sheria na sio kupigana vituoni.
Mungu Ibariki Tanzania.