Hili la kutumbua majipu hadi taasisi za dini limekaa vyema

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
MWALIMU Julius Nyerere aliwahi kutumia hafla aliyokaribishwa na mashehe kusisitiza kwamba serikali haina dini (japo wananchi wataendelea kuwa na dini zao).

Kwamba ni kauli aliyoitoa kwa walengwa, ili kama kuna kiongozi wa dini alikuwa anafikiria vinginevyo aelewe msimamo wa serikali na pia alitaka hilo asilisemee pembeni. Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alifanya kitu kinachofanana na hicho. Kusema mbele ya mashehe, wakati wa Baraza la Idd bila shaka wakiwemo wanaolalamikiwa kuhusu kunufaika na mali za Waislamu kwa maslahi binafsi, kwamba serikali yake itarejesha mali za dini zote zilizoingia kwenye mikono isiyohusika.

Kama alivyofafanua Rais Magufuli, hizi ni mali ambazo kimsingi ziliwalenga waumini, lakini baadaye wajanja wachache wakaingia ubia na wawekezaji kwa kurubuniwa au wakaziuza kwa maslahi binafsi. Mimi (mwandishi) ninazijua pia baadhi ya mali za Waislamu ambazo ama zilitolewa wakfu au zilipatikana kupitia mgongo wa Uislamu, lakini mwisho wa siku wajanja wachache wakazifanya zao binafsi.

Rais alisema: “Ninafahamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini nyingine katika kuwarubuni na kuingia ubia. Mali hizo baadaye huwa zinapotea kabisa.” Halafu baada ya kusema hayo, akaongea kile ambacho kimekuwa kikifumbiwa macho muda mrefu: “Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia mali hizi zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda wawekezaji, lakini wanachokiahidi hawatekelezi. Haiwezekani.”

Ukweli ni kwamba kilichowahi kumpeleka Shehe Ponda Issa Ponda jela wakati fulani na kukaribia kuvunja amani ni hicho cha kudai mali za Waislamu. Na kosa alilofanya Ponda na wafuasi wake ni kuamua kushika sheria mkononi badala ya kufuata mkondo wa sheria. Na ninashukuru kwamba Rais ameliona hilo na sasa anawataka Waislamu kutumia wanasheria kuzirejesha mali zao, badala ya kutumia ‘msuli’ ambao ni hatari kwa amani.

Lakini tatizo ninaloliona ni kwamba, ukiondoa Shehe Mkuu, Abubakar Zubeir ambaye amekuwa akiguswa na mali za Waislamu kupokonywa, baadhi ya ‘majipu’ yanayolalamikiwa kuhusika na kuuza mali za Waislamu kwa maslahi binafsi yalikuwemo pia kwenye baraza hilo la Iddi! Ni kwa msingi huo ninashauri, serikali isaidie kuyatumbua majipu hayo bila hata ya ganzi ili kuleta heshima katika mali za dini ambazo zimekuwa kama hazina mwenyewe.

Kwa sisi tulio ndani ya Uislamu, tunajua kwamba migogoro mingi katika majumba ya ibada imekuwa ikitokana na baadhi ya waumini, hususani vijana, kuamua kuhoji mali za Waislamu ambazo zinatumiwa kwa maslahi binafsi au kuuzwa. Lakini kwa bahati mbaya sana, wabadhirifu wa mali hizo, baadhi yao wakiwa viongozi wa kidini, wamekuwa wakionekana mbele ya macho ya polisi kama malaika, na wale wanaodai mali za Waislamu ambao ndio wanasimamia haki kuonekana kama wakorofi, watu wa vurugu.

Hali hiyo, bila shaka imechangia kuwafanya watu kama Ponda na kundi lake kuamua kuchukua sheria mkononi katika baadhi ya maeneo. Na kwa kweli, hali ya kushindwa kusimamia ipasavyo mali za Waislamu na kusimamia haki kwa ujumla wake imekuwa ikichangia Bakwata kukosa umaarufu miongoni mwa Waislamu.

Mimi ninampongeza sana Rais Magufuli kwa hili na kwa kweli, kama atalisimamia ipasavyo kwa maana ya kuhakikisha haki inatendeka na bila kumuonea mtu, atathibitisha kile alichokisema wakati wa kampeni kwamba atakuwa rais wa wote, akitetea maslahi ya watazania wote bila kubagua itikadi zao za kisiasa wala dini. Huu ndio uongozi uliotukuka.

Ingawa mimi binafsi ninamuunga mkono Shehe Mkuu, Zubeir kwamba amekuwa akipigania umoja wa Waislamu na kutaka kuibadili Bakwata, lakini nimalizie kwa kumshauri Rais pia kuchukua ushauri uliowahi kutolewa wakati fulani bungeni na Mbunge wa sasa wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Zitto aliitaka serikali kufuatilia lawama za muda mrefu za Waislamu kuhusu Bakwata na kutaka zichunguzwe ili kupatiwa ufumbuzi. Kwamba serikali inapotaka kuongea na Waislamu inawaita Bakwata ambao kuna sehemu nyingi hawaungwi mkono na Waislamu wote tofauti na ilivyo kwa vyombo kama Baraza la Maaskofu.

Mimi ninamshauri Rais aongee pia na makundi mengine ya Waislamu, wakiwemo watu kama Ponda kujua uanaharakati wao unalenga nini hasa badala ya kupuuzwa. Ninaamini kwa utaratibu huu aliotangaza rais, na kama ataweza kuongea na makundi ‘yaliyoasi’ kutoka Bakwata, atasaidia sana kurejesha umoja uliopotea ndani ya Uislamu na hivyo kusaidia pia kujenga amani ya nchi yetu.
 
Back
Top Bottom