Hii ndiyo Njia yako ya uhakika ya kutokea

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,912
3,389
Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu hapa duniani huwa ana njia yake ya uhakika ya kutokea, njia ambayo inamfikisha kwenye mafanikio makubwa.

Lakini wengi wamekuwa hawafanikiwi kwa sababu wakifika kwenye njia hiyo, wanabadili njia au kuacha safari kabisa.

Yaani ni sawa na mtu anayetafuta mlango, halafu anapoupata na kukuta umefungwa, anaondoka na kwenda kutafuta mlango mwingine.

Matokeo yake ni mtu kujikuta akihangaika na mambo mengi bila ya kupiga hatua zozote kubwa.



Rafiki, njia ya uhakika kwako kutoka na kufanikiwa ni pale unapokutana na ugumu kwenye kitu chochote ulichochagua kufanya. Pale penye ugumu ndipo penye hazina kubwa ukiweza kuvuka ugumu huo.

Lakini kama tunavyojua, watu wengi wanapokutana na ugumu huwa wanakimbia na kuachana na kitu hicho. Wengi wanaanza kitu na kukifurahia mwanzoni kwa sababu ni rahisi. Lakini wanapoanza kukutana na ugumu, wanaona hawawezi kuendelea tena. Hivyo wanaacha na kwenda kuanza kitu kingine.

Hivyo ndivyo unavyokuta watu wamefanya vitu kumi ndani ya miaka 5 na hawajafanikiwa kwenye kitu hata kimoja. Kama wangekusanya nguvu zote kwenye kitu kimoja, lazima wangefika mbali.

Iko hivi rafiki, pale unapokutana na ugumu ndipo penye fursa kubwa. Ugumu unaashiria fursa kubwa kwa sababu kuu mbili;

Moja ni wewe mwenyewe kuweza kutoka nje ya mazoea yako. Mambo yanapokuwa rahisi ni kwa sababu ya mazoea unayokuwa nayo. Unapotoka nje ya mazoea yako ndiyo mambo yanaanza kuonekana magumu. Huwezi kufanikiwa kwa kufanya kwa mazoea, ni lazima utoke nje ya mazoea. Hivyo unapokutana na magumu usikimbie, jua unatoka nje ya mazoea na hapo ndipo penye mafanikio.

Mbili ni kuweza kuvuka pale ambapo wengine huwa wanaishia. Kwa kuwa wengi wakikutana na ugumu huwa wanaacha, wewe ukiendelea unakuwa tofauti kabisa na hao wengine. Kwa kuendelea licha ya ugumu kunakufanya uwe mbele ya wengine na kuvuka ushindani ambao unabaki chini. Hilo linakupa fursa kubwa ya wewe kufanikiwa zaidi.

SOMA; Sababu Mbili Kwa Nini Mafanikio Ni Magumu Sana Kwa Zama Hizi.

Unapokutana na ugumu kwenye jambo lolote lile, huwa unaanza kufikiria kuacha na kubadili kile unachofanya. Lakini kwa namna ulivyojifunza hapa, kamwe usifanye hivyo. Badala yake tafuta njia ya kuvuka kila ugumu unaokutana nao na kuweza kupata matokeo makubwa na mazuri.

Upande wa pili wa kila ugumu kuna fursa kubwa na nzuri kwako kupata mafanikio unayoyataka. Hivyo kila unapokutana na ugumu, usikimbie, badala yake jua umefika kwenye njia ya uhakika kwako kutoka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekufafanulia kwa kina jinsi ya kukabiliana na magumu unayokutana nayo kwenye safari yako na kuyageuza sababu ya wewe kufanikiwa. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho na kwenda kufanyia kazi ili mafanikio yawe ya uhakika kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom