YANAYOSABABISHA HALI NGUMU MITAANI NI HAYA.
Waraka wa BASHIR YAKUB +255784482959.
1. Kuziba kwa mianya ya wizi bandarini. Kama tunasema bandari pekee ikitumika vizur inaweza kuilisha Tanzania nzima halafu hapohapo ikawa mapato yake ya zaidi ya 70% yanaingia mifukoni mwa watu, unategemea nini tena hiyo ya 70% ikizuiwa kuingia mifukoni mwa hao watu. Ni bila shaka athari zake zitaonekana maishani mwetu.
Hawa watu waliokuwa wanachezea hii 70% ambalo ni pato kubwa kabisa wana makampuni, wameajiri maelfu ya watu , wana familia,ndugu na marafiki ambao wamekuwa wakiogelea kwenye hii 70% nk, nk. Hawa maelfu walioajiriwa nao wanazo familia, wanazo biashara ndogo ambazo nazo wameajiri watu. Cheni ni ndefu kuliko niliyotaja na kwa ufupi unakuta imemgusa kila raia. Sasa hali ya uchumi inabakije vilevile baada ya hii 70% kuminywa. Katu haiwezekani lazima tuhisi(feel) maumivu.
Isipokuwa swali litakuwa Kama pesa hiyo imetoka mikononi mwa wachache na kuwa mali ya taifa kwann serikali isiirudishe mitaani ikaonekana tena kwa njia halali. Jibu litakuwa ni kwamba matokeo ya serikali kuingiza hela mtaani hayawezi kuonekana haraka. Yanaonekana baadae kupitia manufaa ya miradi.
Hela ya ubadhirifu bandarini ilikuwa ni hela nyingi mno kuwa kwenye mzunguko na kuondoka kwake ghafla hakuwezi kutuacha salama. Huu ni ukweli na lazima tuukubali.
2. Pesa ya wauza unga. Mzunguko wa hela ya unga mtaani unakadiriwa kufikia hadi tirioni 2 kwa mwaka. Pesa hii inaondokaje ghafla mtaani halafu tukabaki vilevile. Haiwezekani lazima tuhisi kupungukiwa na kitu.
Sehemu unakoziba mzunguko wa tirioni 2 katu hapawezi kubaki Kama awali. Ni patakuwa na mabadiliko tu.
3. Pesa iliyotokana na matumizi mabaya katika taasisi za serikali na ufisadi. Pesa ya rushwa, posho za hovyo, matumizi yasiyo na tija hakuna tena. Mzunguko wa pesa hii sio wa kubeza. Ulikuwa mkubwa na ulisisimua mitaani. Mameneja, wakurugenxi na viongozi wengine wa serikali walikuwa hawaulizi mara mbili katika kununua majumba ya bilioni 2 na zaidi, kujenga mahoteli, mabar na viwanja vingine vya starehe kwa pesa ambayo haitokani na mshahara.
Walikuwa hawaulizi mara mbili kuhonga magari ya milioni 30, 20 nk. Walikuwa hawaulizi Mara mbili kutoa mamilioni ya mitaji ya kuanzisha biashara kwa familia zao na wapendwa wao. Yote hii ni pesa kwenye mzunguko.
Ilikuwa ni kawaida kwa taasisi ya serikali kushikilia hata kumbi nne katika hoteli tofauti tofauti kwa kipindi cha miezi hata minne huku wakizilipia kila siku. Wamefanya mikutano au hawakufanya wanalipia tu.
Ndio maana hoteli nyingi zimefunga kumbi na waajiriwa katika kumbi hizo wamepunguzwa. Hii yote ilikuwa ni hela kwenye mzunguko. Unategemeaje kukatwa kwake ghafla kutuache kama tulivyokuwa awali. Haiwezekani jamani.
JAMBO MOJA KUBWA: Ni kwamba karibia 60% ya pesa iliyokuwa inasisimua na kuchamgamsha mitaa yetu ilikuwa ni pesa haramu/chafu. Kuondoka kwake ghafla hakuwezi kutuacha vilevile kama tulivyokuwa. Ilikuwa ni lazima tuone na kuhisi unyonge katika vipato vyetu baada ya kuondoka pesa hii.
Ila kitu kimoja ni kuwa uchumi una mazoea. Kama tulivyokuwa tumezoea kuishi kwa pesa haramu siku zinakuja ambapo tutazoea kuishi kwa pesa ambayo vyanzo vyake ni halali na hapo tutaacha kulalamika.
Lakini pia siku zinakuja ambapo manufaa makubwa ya kurudisha pesa hii mikononi mwa umma yataonekana na kila mmoja atafaidi tofauti na pesa haramu ambayo wachache ndio hufaidi.
Kwa haraka hatua zinazochukuliwa ni muhimu mno kuliko tunacholalamikia sasa.