Kilio ukata wiki ya tatu bungeni
www.ippmedia.com/sw/habari/kilio-ukata-wiki-ya-tatu-bungeni
Hata hivyo, wakati hali ikionekana kuwa kero kwa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi kulazimika kuwazuia wabunge wake kuibua na kuachangia kwa kuiunga mkono hoja hiyo na nyingine zenye kufanana nayo, ilifichuka kuwa hali ya Bunge kifedha ni mbaya.
Aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, ameweka wazi kuwa hali ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NOAT) ambayo yeye ndiye mkuu wake, nayo si nzuri kifedha.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ndiyo iliyofichua ukata unaolikabili Bunge wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi Waziri Mkuu wiki juzi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia anasema kuwa katika mwaka huu wa fedha (2016/17), Mfuko wa Bunge (Fungu 42) uliidhinishiwa jumla ya Sh. bilioni 99.066 na hadi kufikia Machi 31, ulikuwa umepokea Sh. bilioni 77.479 (Sh. bilioni 59.929 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh. bilioni 17.479 kwa ajili ya mishahara).
”Hata hivyo, pamoja na kupokea fedha hizo, bado kunaonekana kuna changamoto kubwa ya kutolewa fedha kwa wakati kwa fungu husika na hivyo kuathiri utekelrezaji wa baadhi ya majukumu ya Mfuko wa Bunge,” anasema Ghasia.
Anasema hadi sasa mfuko huo una bakaa ya bajeti ya matumizi mengineyo ya kiasi cha Sh. bilioni 8.338 kulingana na bajeti iliyoidhinishwa, lakini bakaa hiyo haitoshi kutekeleza shughuli zilizobaki katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.
Anasema kamati yake imebaini mfuko una upungufu wa Sh. bilioni 21.196 ambao utaathiri utekelezaji wa shughuli za Bunge kwa kipindi cha robo ya nne, changamoto Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wataitua kwa kulipatia Bunge kiasi hicho cha fedha.
Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), anasema kamati yake imethibitisha kuwapo kwa changamoto ya mgawo wa fedha kutoka Hazina kutoendana na ratiba ya shughuli za ofisi hivyo, Ofisi ya Bunge imejikuta ikiingia katika madeni ya kiasi cha Sh. bilioni 5.7 huku Spika Job Ndugai akikiri kuwa hali ni mbaya na imefikia kipindi wanachelewa kulipa mishahara na posho za wabunge.
Wakati wabunge wakilia ukata, CAG Assad naye ameweka wazi kwamba ofisi yake imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati kutokana na kutopewa fedha na serikali.
Prof. Assad aliwaambia waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge mjini hapa wiki iliyopita kuwa
hadi Oktoba mwaka jana, alikuwa hajapewa hata senti moja kwa ajili ya ukaguzi.
Kutokana na changamoto hiyo, Prof. Assad alisema anashindwa kufanya kazi kwa kufikia kiwango cha kitaifa na kimataifa cha ukaguzi kama inavyotakiwa licha ya kuwa na watumishi wenye ari ya kufanya kazi kwa muda mrefu.
Pia, Prof. Assad aliwaambia waaandishi wa habari mjini hapa Machi 14, kuwa anashindwa kukaa ofisini kwa utulivu kutokana na madeni makubwa ya makandarasi ambao wanajenga majengo yetu.
UTATA WA WAZIRI MPANGO
Fungu la NOAT lilikuwa miongoni mwa mafungu manne yaliyoibua mjadala mzito bungeni wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka jana baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kubaini kuwa kiwango cha fedha kilichopangwa kwa ajili ya ofisi hiyo kilikuwa pungufu kwa asilimia 60 kulinganishwa na makadirio yake kwa mwaka huu wa fedha.
Mafungu mengine yaliyolalamikiwa kwa kiasi kikubwa na watunga sheria hao ni ya Mfuko wa Bunge, Mahakama na Maji.
Wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka huu wa fedha, Naibu Waziri Kivuli wa wizara hiyo aliliambia Bunge kuwa walibaini bajeti ya NOAT ilikuwa imefyekwa kwa asilimia 60 ikilinganishwa na makadirio ya ofisi hiyo.
Alisema ofisi hiyo iliomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 68.839 ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi, lakini serikali ilitengea Sh. bilioni 32.3. Kati ya fedha hizo zilizotengwa na serikali, Sh. bilioni 28.3 ni za matumizi ya kawaida na Sh. bilioni nne ni za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Silinde ambaye alilazimika kusoma bajeti ya upinzani kutokana na kutokuwapo bungeni kwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, alifichua kuwa mafungu ya Mahakama, Bunge na Maji yalikuwa yamefyekwa kulinganishwa na mwaka wa fedha 2015/16 na pia huku akimshukia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kwa madai ya kupanga bajeti bila kuzingatiwa uhalisia na umuhimu wa mafungu husika.
Hata hivyo, katika kile ambacho baadhi ya wabunge wamekuwa wakikiita 'ubishi', Dk. Mpango alikaa kuongeza mafungu hayo, uamuzi ambao madhara yake yanaonekana sasa.
Wakati Dk. Mpango alikataa kuyaongeza fedha mafungu hayo, Waziri Mkuu anasema serikali italiongeza Bunge zaidi ya Sh. bilioni 21 ambazo kimsingi ndicho kiasi cha fedha ambacho Waziri Mpango alikataa kukiongeza katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya serikali mwaka jana.