"Katiba ya nchi ni msingi na chimbuko la sheria zote nchini pamoja na uwezo wenyewe wa kutunga na kuendesha utawala kwa mujibu wa sheria. Katiba hugawa nguvu za dola kwa vyombo vikuu vitatu - yaani vyombo vya utungaji sheria, vyombo vya utendaji na vyombo vya utoaji haki.
Mgawanyo wa nguvu za dola kati ya vyombo vilivyotajwa na kutokuingiliana katika madaraka ya vyombo hivyo ni msingi mojawapo wa utawala wa demokrasia ya kiliberali. Walakini, muhimu zaidi kuliko vifungu vya katiba ambavyo ni wazi, ni itikadi inayo halalisha utawala na matumizi ya madaraka kwa upande wa tabaka-tawala dhidi ya matabaka-tawaliwa.
Tangu Tanzania ipate uhuru wake kumetungwa katiba nne (au tano) mpya na marekebisho mengi ya mara kwa mara. Katiba ya kwanza kabisa ilikuwa Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961. Umuhimu wa Katiba ya 1961 ni kwamba ilikuwa kama njia ya kutoa uhuru kwa Tanganyika. Kwa wananchi na viongozi wao katiba hii haikuwa kama muafaka wa siasa kati ya watawala wa ndani na watawaliwa bali ilikuwa hitimisho la mapambano ya kitaifa dhidi ya ukoloni.
Kwa kweli, katiba yenyewe ilitungwa na wataalamu wa ofisi ya koloni huko Uingereza na katiba iliwekwa kama nyongeza (
schedule) ya Sheria ya Uhuru wa Tanganyika iliyopitishwa na Bunge la Uingereza.
Ushirikishwaji wa wananchi katika Utungaji wa Katiba: Tukiangalia historia ya utungaji katiba katika nchi yetu, hatujawa na tabia wala utamaduni wa kuhusisha na kushirikisha wananchi kwa jumla yao katika mijadala ya katiba.
Katika nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, kama nilivyoonyesha, katiba ilikuwa na nafasi tofauti. Katiba imekuwa kama ramani ya kurekodi ugawaji wa nguvu na hasa kuweka ukiritimba wa nguvu za dola mikononi mwa chombo cha utendaji chini ya rais, kwa upande mmoja, na kuweka ukiritimba wa mambo ya kisiasa mikononi mwa chama kimoja, kwa upande mwingine.
Kama msomi na kama mwananchi, ningependa kusisitiza kwamba kuna haja kubwa na nyakati hizi ni nafasi nzuri ya kihistoria kuangalia na kutafakari upya hoja ya kutunga katiba mpya.
Kazi kama hii haina budi ifanyike bila jazba na bila ushindani wa kisiasa, bali kwa kuweka matakwa ya taifa mbele ya ubinafsi na maslahi ya chama chochote kile. "
Profesa Shivji