Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene akiagiza uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ufanyike kabla ya Machi 25, halmashauri hiyo imesema haijapata taarifa rasmi.
Machi 11, Simbachawene akiwa Arusha aliagiza uchaguzi huo kufanyika kwa kuzingatia kifungu cha 13(1) cha Kanuni za Kudumu za Jiji.
Pia, Simbachawene alitaja sifa za wapiga kura kuwa lazima wawe madiwani wote wa halmashauri za Jiji la Dar es Salaam za Ilala, Temeke na Kinondoni, wabunge wa kuchaguliwa na viti maalumu ambao mchakato wa kuwapata ulianzia kwenye mamlaka za halmashauri hizo.
Katika mkutano huo na wanahabari, Simbachawene alisisitiza vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kukubali matokeo ili kutosimamisha maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya Simbachawene kutaja tarehe hiyo, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Wilson Kabwe alisema hadi sasa hawajapata taarifa rasmi ndiyo maana wanashindwa kuitisha kikao cha baraza la madiwani, kitakachokuwa na ajenda moja ya kumchagua meya na naibu wake.
Uchaguzi huo, umeahirishwa mara tatu kwa sababu mbalimbali, ikiwamo mvutano kati ya vyama vya CCM na Ukawa, hasa uhalali wa wajumbe wa kupiga kura na kuwapa muda mameya wa manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke kuteua wajumbe bila kujali itikadi watakaoingia kwenye halmashauri hiyo.