SoC02 Elimu ya juu kwa maendeleo ya Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

NAIMA MAVURA

New Member
Sep 9, 2022
1
1
ELIMU YA JUU TANZANIA​

Elimu ni ujuzi, uelewa na maarifa kuhusu jambo au mambo Fulani. Elimu hupatikana sio tu kwa kufundisha bali hata kwa kujadiliana na kuuliza maswali. Elimu ni ufunguo wa mafanikio ikiwa na maana ya kuwa ni wajibu wa kila mtu kuipata bila kuzingatia hali ya Maisha, jinsia, kabila, umri, rangi na dini. Elimu yaweza kuwa iliyo rasmi. Elimu rasmi ni elimu ambayo hutolewa pale ambapo mtu huingia darasani na kufundishwa mfano elimu ya awali, msingi, upili na elimu ya juu.

Elimu ya juu ni elimu ambayo hutolewa vyuoni baada ya kumaliza elimu ya upili hujumuisha elimu, utafiti, huduma za kijamii na mawasiliano. Elimu ya juu kama ngazi ya elimu nyingine ina faida kama zifuatazo;

Kuongezeka kwa uwezo wa kuajiriwa; Wanafunzi waliohitimu elimu ya juu wenye shahada ya kwanza hupata kazi kirahisi kuliko wale wenye stashahada hivyo kumhakishia mtu ufaulu wa Maisha akipata ajira kirahisi. Mtu hubobea katika sekta kama vile udaktari, urubani, ualimu hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kupandisha uchumi.

Vilevile huboresha uwezo wa mawasiliano; kwa maana elimu ya juu mtu huipata si kwa njia ya kufundishwa pekee bali hata kwa utafiti, majadiliano, kuwasilisha mbele ya wanafunzi wengine na wakufunzi, kutumia vifaa vya teknolojia kama vile projekta na tarakilishi. Hivyo humpa mwanafunzi uwezo mkubwa wa kuongea mbele ya watu kwa kuzingatia cheo na umri na kuweza kufikia malengo kama vile kuwa raisi, mbunge, Waziri ambayo itampasa kuongea mbele za watu.

Pia huongeza kujiamini na kujitambua nafasi yake katika jamii; tunaamini kuwa mwanafunzi wa elimu ya juu anauwezo mkubwa kiakili hivyo huweza kufikiria mambo yanayomzunguka, kwa elimu aipatayo anaweza kufanya utafiti na kupata suluhisho hivyo kuielimisha jamiii yake kuhusu suala linalokabili jamii husika bila kutetereka na hivyo kukubalika katika jamii.

Inakuza uvumbuzi kupitia utafiti mbalimbali zinazofanyika vyuoni; tafiti hizo zinakuza na kuchochea ubunifu wa vifaa haswa sayansi na teknolojia na suluhisho kwa matatizo mbalimbali katika jamii katika Nyanja kama vile afya. Wanafunzi vyuoni hubuni vifaa mbalimbali vinavyo rahisisha utendajii kazi katika sekta tofauti kama vile jembe linalotumia umeme wa jua, lilogundulika na wanafunzi wa vyuoni.

Kila chenye umuhimu kwenye jamii hakikosi kasoro, elimu ya juu ina changamoto mbalimbali zinazowakumba wanafunzi, wakufunzi na wadau wote wa elimu changamoto hizo ni kama zifuatazo;

Hakuna taasisi maalumu ya kuwapima wanafunzi; mkufunzi ndiye muamuzi wa ufaulu wa mwanafunzi inategemea na matakwa yake akiamua huyu afaulu basi atafaulu au asifaulu. Mfano kama mapendekezo yake yapo katika pesa basi atahakikisha yule mwenye pesa ndiye atakayefaulu na yule asiye na pesa hatofaulu hivyo kukwamisha maendeleo ya wanafunzi, pia hata mwenye uwezo wa kumpa rushwa ya ngono anaweza kufanya vizuri akiwa hastahili kufaulu hivyo kuwanyima haki ya msingi wanafunzi wengine wanaostahili na kupelekea kupata watu wasio na ujuzi katika sekta husika.

Hakuna mtaala unaowaongoza wakufunzi katika ufundishaji; kila mkufunzi hufundisha mada kwa ujuzi wake na uelewa wake, hakuna muongozo maalumu uliowekwa kwamba mkufunzi anatakiwa kufundisha sehemu Fulani mpaka Fulani hivyo kupelekea wanafunzi wawili wa vyuo tofauti kuwa na uelewa tofauti kuhusu mada Fulani hivyo kuleta mchanganyo katika uwasilishaji wa maarifa yao.

Tafiti mbalimbali hazitiliwi maanani na serikali kama umahiri na uzamifu; katika nchi yetu mtu anayethaminiwa ni yule mwenye shahada ya kwanza na ndiye atakayepata kazi kirahisi, ila yule mwenye uzamifu huonekana kuwa ana elimu ya ziada. Hivyo kushindwa kupata ajira kwa hofu ya waajiri kushindwa kuwalipa mshahara.

Kutokuthaminiwa kwa watoa elimu (wakufunzi na wadhahiri); idadi ya wakufunzi na wadhahiri nchini ni ndogo kwakuwa thamani yao haipewi kipaumbele. Wakufunzi na wadhahiri wanafanya kazi kwa wito lakini malipo yao ni madogo na hayalingani na kazi kubwa waifanyao, hivyo kuwakatisha tamaa kuendelea na kazi nzito ya ufundishaji na kuamua kutafuta ajira nyingine itakayo mthamini.

Kila tatizo lina ufumbuzi wake, yafuatayo ni mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha elimu ya juu;

Kutenga taasisi maalumu au tume ambayo itawapima wanafunzi ili kutokupendelea wala kuwaonea wanafunzi wanayostahili; Serikali yatakiwa kuweka taasisi ambayo itampima mwanafunzi kwa njia yoyote ili kumpa ufaulu wake au kufeli kwake na sio mkufunzi kuamua ili kuondoa upendeleo wa aina yoyote ambao utaonekana kujitokeza, hivyo itapelekea kupata wafanya kazi wenye ufanisi, maarifa na ueledi katika kazi zao.

Kuweka taasisi maalumu vyuoni itakayozuia na kupambana na rushwa ya aina yoyote; taasisi hiyo inatakiwa kuhakikisha hakuna rushwa itayotolewa wala kupokelewa kwa mwanafunzi na mkufunzi wake na kama ikitokea hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote wawili ipate kua fundisho kwa wanafunzi na wakufunzi wengine na kwa kufanya hivyo tutapata wanafunzi bora watakaoiongoza jamii katika njia sahihi na inayotakiwa.

Serikali inatakiwa kutenga bajeti maalumu na yakutosha kwa ajili ya elimu ya juu; mfuko utakaotengwa utatumika katika kuwalipa wakufunzi, wadhahiri, ununuzi wa vifaa vya kufundishia kama vile projekta, tarakilishi, vishkwambi na kujenga vyuo vingine nchini ili iendane sambamba na idadi ya wanafunzi na kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye ufaulu mzuri anapata chuo na kuendeleza masomo yake ili aweze kufikia malengo yake.

Kwa kuhitimisha, serikali ya Tanzania inapaswa kushirikiana bega kwa bega na taasisi ya elimu ya juu Tanzania ili kuhakikisha elimu bora inatolewa nchini kwa maendeleo ya taifa letu la sasa na hata la vizazi vijavyo.

Naima Mavura.

Feza girls secondary school. 0715418188.
 
Back
Top Bottom