Edo Kumwembe: Jonas Gerald Mkude, ni mwisho wa zama zake?

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
704
1,456
NIMEKUMBUKA miaka michache tu iliyopita, Simba walikuwa wanapigania maisha yao kwa Jonas Gerald Mkude. Wakati huo mkataba wake ulikuwa unakaribia kumalizika Simba na Yanga walikuwa wanahaha kumnasa Jonas. Simba walilazimika kutoa kiasi cha shilingi 80 milioni kuinasa saini yake kwa mkataba wa miaka miwili.

Maisha yamekwenda na yamebadilika ghafla kwa Mkude na Simba yenyewe. Ghafla Mkude si mali kitu kwa Simba. Kwanini? Ndani ya miaka miwili amekuwa akisotea benchi, huku hata yeye mwenyewe akishindwa kuonyesha hasira za kukaa benchi. Kuna viungo wawili tu wa chini ambao Simba imekuwa ikiwategemea kwa misimu miwili sasa. Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.

Jonas amekwenda chini ghafla. Asikudanganye mtu kuhusu umri. Nadhani wengi tulianza kuwafahamu kina Khalid Aucho kwa miaka mingi kabla ya Mkude. Jonas ameshindwa mwenyewe tu kwa sababu ambazo anazifahamu yeye mwenyewe.

Sababu nyingine zinadaiwa kufahamika zaidi kwa viongozi wa Simba. Kwamba Jonas ana matatizo binafsi katika nidhamu yake nje ya uwanja. Kwamba ana mambo mengi ya ajabu ambayo mwanasoka wa kulipwa hapaswi kuyafanya wakati akipambana kutetea ugali wake mezani. Hatuwezi kuhukumu lakini muda umehukumu.

Ndani ya uwanja Simba imemuacha Jonas kwa sababu tofauti. Wote wawili, Simba na yeye wamezama katika miaka ya karibuni. Simba imekwenda chini na imeruhusu watani zao Yanga watawale soka la Tanzania katika misimu hii miwili. Jonas naye amekwenda chini. Bahati mbaya kwake ni kwamba Simba walikuwa na uwezo wa kumtosa Jonas kujiokoa lakini Jonas hakuwa na nafasi ya kuitosa Simba kwa ajili ya kujiokoa.

Simba wamemtosa Jonas wakiamini kwamba si mali kitu tena. Lakini zaidi wamemtosa katika nyakati ambazo wanaamini kwamba hata hao watani zake Yanga na Azam hawawezi kumfukuzia tena Jonas. Kila unapopiga hesabu unagundua kwamba katika eneo ambalo Simba wamezidiwa na Yanga na Azam ni eneo la kiungo.

Hata kama Yanga au Azam wataamua kumchukua Jonas basi itakuwa kwa ajili ya kuongeza idadi tu katika eneo ambalo tayari wapo vizuri. Siku hizi wakubwa hawana muda tena wa kutambiana kijinga katika kula makapi ya mtu mwingine. Jonas alipaswa kunusuru maisha yake ya soka akiwa ndani ya Simba.

Hakuweza kufanya hivyo licha ya wote sisi kuamini kwamba alikuwa na kipaji kikubwa kuliko akina Mzamiru na Kanoute. Maisha ya kileo hayamsubiri mtu na Simba imeamua kufanya maamuzi sahihi kwa ajili yao baada ya kuona wamepitwa kwa kiasi kikubwa na watani wao ndani ya miaka miwili. Wameamua kusafisha.

Na hii ina maana gani? Simba imeachana na wachezaji iliokosea kuwasajili ndani na misimu miwili iliyopita, lakini pia imeamua kuachana na wachezaji wakongwe kama Jonas, Erasto Nyoni na Gadiel Michael ili waache kuishi kimazoea. Nilifahamu hili tangu awali kwamba Simba walikuwa wamepania kutembeza panga haswa katika dirisha hili na kusaka wachezaji mahiri kwa ajili ya kuishusha Yanga pale ilipo.

Na hii ina maana pia tunaendelea kupunguza idadi ya wachezaji mahiri wazawa katika vikosi vikubwa ambavyo tunatazamia viimarishe wachezaji zaidi kwa ajili ya kuwa na kikosi imara cha timu ya taifa. Wao ndio ambao wanashiriki katika mechi nyingi za kimataifa na wapo katika nafasj nzuri zaidi za kutuimarishia wachezaji wetu.

Mchezaji kama Jonas anapoondoka katika kikosi cha Simba kisha akatimkia katika timu ya kawaida ni wazi kwamba anakosa ushiriki wa mechi nyingi za kimataifa tofauti na alipokuwa na Simba ambapo alikuwa anaimarika kila kukicha. Hauwezi kuliona hili kama unatumia jicho la kishabiki. Hata hivyo hauwezi kuwalaumu Simba. Wanapambana na maslahi yao kama timu.

Lakini hapo hapo inatukumbusha namna gani maisha ya mwanasoka yalivyo mafupi. Ni mafupi haswa. Hawa wachezaji wakiwa katika ubora wao huwa wana maringo mengi na wakati mwingine huwa wana mambo mengi ya ajabu nje ya uwanja. Wasichofahamu ni kwamba mwanasoka akifikisha miaka 31 tu anaitwa mzee.

Wanasoka wengi wanaojitambua huwa wanafanya mambo mawili. Kwanza wanajijenga kimaisha nje ya uwanja, lakini pili wanahakikisha wanajitunza na kupambania vilivyo kazi yao mpaka dakika ya mwisho. Mpaka pale ambapo mwili utakataa. Na unapocheza katika kiwango cha juu, ukiwa na timu kubwa kama Simba unaongeza ari ya kupambana zaidi.

Naweza kuingia katika dhambi ya kutomuamini Jonas. Siamini kama alipambana kama vile ambavyo Juma Kaseja, Aucho, George Kavilla na wengineo ambao wamepambana vilivyo kuongeza muda wao katika soka. Naamini hata kesho Jonas akiamua kupambana bado anaweza kuwa mzuri. Tatizo ameruhusu muda umpite kiurahisi.

Pale Afrika Kusini kuna mchezaji anaitwa Elias Pelembe 'Domingues' ambaye ni raia wa Msumbiji. Mwaka 2006 Taifa ilikwenda kucheza na timu ya taifa ya Msumbiji na alitusumbua kweli kweli. Nakumbuka katikati ya uwanja alikuwa akimnyanyasa Athuman Idd 'Chuji' ambaye alikuwa anakabiliana naye.

Leo Pelembe ana miaka 39 na anacheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini akiwa na klabu ya Royal AM baada ya kubadilisha klabu kadhaa nchini humo. Kumbuka wakati huo Chuji alikuwa katika ubora wake na hatukujua kama kutatokea mchezaji anayeitwa Mkude. Leo Chuji amestaafu muda mrefu sasa na Mkude ndio huyo anaondoka katika timu kubwa, lakini bado Pelembe anacheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini na timu yake ya taifa.

Lakini najaribu tu kuwakumbusha namna ambavyo hakuna mahusiano makubwa kati ya wachezaji na klabu hizi. Nimekuwa nisikia watu wakilalamika kwamba Jonas hajaagwa kwa heshima pale Msimbazi. Kwamba labda hakustahili kupewa 'Thank you' kama walivyopewa wachezaji wengine.

Hakuna uhusiano mkubwa kati ya mchezaji na klabu
Huu unapaswa kuwa uhusiano wa mfanyakazi na mwajiri. Siku ikifika unaondoka tu. Haijalishi umefanya mambo mangapi. Kitu cha msingi kwa Mkude ni kama alijenga maisha yake vizuri nje ya uwanja. Ukweli ni kwamba haijalishi Simba imemuaga kwa namna gani kitu cha msingi ni namna alivyoitumia Simba kujijenga.

Kungeweza kuwa na uwezekano hata wa yeye kuiacha Simba katika mataa akiwa katika ubora wake. Mbona hatutazami upande huo? Wakati huo tungesema kwamba Jonas ameikosea heshima Simba? Hapana.

Angekuwa ametafuta maisha yake kama ambavyo Simba inasaka maslahi yake kwa sasa. Tuwafundishe wachezaji wetu kuwa viburi wa maisha yao tu. Wasitegemee sana fadhila kutoka katika hizi timu. Wao sio mashabiki.

Mwisho wa siku, nadhani Jonas bado ana nafasi. Kama Yanga, Azam na Singida watamfikiria bado litakuwa jambo jema kwake. Lakini kama hawatamfikiria bado anaweza kufanya kile ambacho Saidoo Ntibanzokinza alifanya alipoachwa na Yanga. Alikwenda timu ya kawaida akafanya mambo makubwa akarudi timu kubwa.
Mpira upo katika himaya yake. Kwanza akiri katika nafsi yake kwamba adui mkubwa wa maendeleo yake ni yeye mwenyewe. Akiamua anaweza kuondoka na adui huyu. Vinginevyo kwa sasa ametuacha tukiwa tunafakari tu, ni mwisho wa enzi zake au?

CREDIT: MWANASPOTI
 
Huyu mwandishi siku zote huwa ana personalize habari zake, very unprofessional ..atatafuta tu namna ya kuku attack hata kwa kung'ata na kupuliza.. ana kawivu wivu flani hivi... akikujua kidogo hasa kwenye maisha ya mtaani utamkoma.. aliwahi kufanya hivi kwa kina Pawasa huko nyuma.. aache uswahili.. maisha ya mtaani kinondoni yaishie huko huko, asiyafanye kuwa habari ya soka..
 
Huyu mwandishi siku zote huwa ana personalize habari zake, very unprofessional ..atatafuta tu namna ya kuku attack hata kwa kung'ata na kupuliza.. ana kawivu wivu flani hivi... akikujua kidogo hasa kwenye maisha ya mtaani utamkoma.. aliwahi kufanya hivi kwa kina Pawasa huko nyuma.. aache uswahili.. maisha ya mtaani kinondoni yaishie huko huko, asiyafanye kuwa habari ya soka..
Huyu chinga ni mnafiq sana
 
Huyu mwandishi siku zote huwa ana personalize habari zake, very unprofessional ..atatafuta tu namna ya kuku attack hata kwa kung'ata na kupuliza.. ana kawivu wivu flani hivi... akikujua kidogo hasa kwenye maisha ya mtaani utamkoma.. aliwahi kufanya hivi kwa kina Pawasa huko nyuma.. aache uswahili.. maisha ya mtaani kinondoni yaishie huko huko, asiyafanye kuwa habari ya soka..
Ungeona wakati wa sakata la Feitoto alikuwa anaongea tofauti na ukisoma Makala ya Mkude eti mchezaji ana muda mfupi huwa linawapata wajinga
 
Angekuwa ametafuta maisha yake kama ambavyo Simba inasaka maslahi yake kwa sasa. Tuwafundishe wachezaji wetu kuwa viburi wa maisha yao tu. Wasitegemee sana fadhila kutoka katika hizi timu. Wao sio mashabiki.
Sahihi kabisa, Feisal apongezwe sana kwa kujitambua mapema.....
 
Back
Top Bottom