Dkt Mpango ataka ubunifu wa vijana uzingatiwe katika matumizi ya nishati safi ya kupikia

Pfizer

JF-Expert Member
Mar 25, 2021
532
753
Na Irene Gowelle

Baku, Azerbaijan.

Ili kufikia malengo tarajiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, Makamu wa Rais, Mhe.Dkt Philip Mpango amesema ni muhimu uvumbuzi na ubunifu wa vijana ukazingatiwa. Kauli hiyo ya Dk Mpango, inakuja kuweka msisitizo wa matumizi ya mbinu za ubunifu ili kuifikisha Afrika na Dunia katika lengo la matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia.
IMG-20241114-WA0035.jpg

Hoja ya matumizi ya bunifu hizo kwa mujibu wa Dkt Mpango, inalenga kurahisisha gharama za nishati hizo kwa wananchi ili wote wawe na uwezo wa kununua na kutumia nishati safi ikiwemo wale wa maeneo ya vijijini.

Dkt Mpango ametoa kauli hiyo jana, alipohutubia kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa pembezoni uliolenga kuwaleta pamoja viongozi,watunga sera na wadau mbalimbali kujadili changamoto zilizopo barani Afrika katika kufikia matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP29 unaoendelea mjini Baku, nchini Azerbaijan.

Katika hotuba yake Makamu wa Rais amesema ni muhimu uongozi wa Afrika kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia, huku akihamasisha uvumbuzi kwa vijana.

“Kutokana na idadi kubwa ya vijana Afrika, ni lazima tutumie ubunifu wao katika kutengeneza suluhisho la matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Dkt Mpango.

Amependekeza matumizi ya mbinu zitakazowawezesha wananchi kulipia nishati kulingana na matumizi, ili kuwawezesha wengi kumudu gharama zake.

Tukio hilo, lililoandaliwa na Tanzania na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), huku likihudhuriwa na viongozi mashuhuri waliosisitiza umuhimu wa uongozi thabiti na ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kufanikisha lengo la matumizi ya nishati safi kwa Waafrika wote.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kamishna wa Miundombinu na Nishati wa Umoja wa Afrika, Dkt Amani Abou-Zeid, alitoa wito wa kuhamishia mnyororo wa uzalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia ili kuchochea uchumi wa ndani, kuwawezesha wananchi na kuongeza upatikanaji wa nishati.

“Tunawataka wadau wote kushirikiana katika kujenga mnyororo wa nishati unaotegemea rasilimali za ndani ili kuhakikisha mabadiliko ya nishati safi ya kupikia yanaenda kwa haki na kusaidia ukuaji wa kijamii na kiuchumi,” amesema Dkt Abou-Zeid.

Naye Damilola Ogunbiyi Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya nishati endelevu kwa wote amesema “utekelezaji wa miradi ya umeme ni lazima uende sambamba na utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia. Tuchukue uzoefu wa uongozi wa Tanzania katika kutekeleza agenda ya nishati safi ya kupikia kupitia miradi ya kufunga mifumo hiyo katika Taasisi ikiwemo shule zenye Programu ya kulisha wanafunzi”.

Pamoja na mambo mengine, tukio hilo lilidhamiria kuhamasisha mazingira bora ya sera na uwekezaji katika nishati safi ya kupikia, ikiwemo kutekeleza ahadi zilizowekwa katika Azimio la Nairobi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Katika azimio hilo viongozi wa Afrika walikubaliana kuboresha mazingira ya kisheria na kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia.

Akizungumza katika tukio hilo, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki amesema Afrika haiwezi kuwa na mpito kamili wa nishati bila kushughulikia pengo la matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Karibu Waafrika bilioni moja bado wanategemea mafuta yasiyo salama na yenye kuleta uchafuzi wa mazingira katika mapishi,” amesema.

Ameahidi benki hiyo itaipa ufadhili wa dola bilioni 2 katika kipindi cha miaka 10, kauli ambayo ilitolewa pia katika COP28.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nishati la Kimataifa (IEA), Dkt Fatih Birol alisema ni muhimu kuhakikisha Waafrika wote wanapata teknolojia za nishati safi ya kupikia, akisisitiza ni jambo linalowezekana ndani ya muongo mmoja.

Ameongeza IEA inafanya kazi kwa karibu na Tanzania na nchi nyingine ili kuendeleza hilo, huku ikihamasisha hatua zaidi kutoka kwa wadau wote.

Katika hatua nyingine tukio hilo pia lilishuhudia kuzinduliwa kwa ripoti ya kupitia changamoto za nishati safi ya kupikia, iliyotolewa na Kamisheni ya Nishati ya Umoja wa Afrika (AFREC).

Ripoti ambayo inatoa mwanga kuhusu teknolojia, mifumo ya kifedha na sera zinazohitajika ili kusaidia mpito wa Afrika kuelekea matumizi ya nishati hiyo katika kupikia.
IMG-20241114-WA0038.jpg
IMG-20241114-WA0040.jpg
IMG-20241114-WA0042.jpg
IMG-20241114-WA0037.jpg
IMG-20241114-WA0035.jpg
IMG-20241114-WA0034.jpg
IMG-20241114-WA0033.jpg
IMG-20241114-WA0031.jpg
IMG-20241114-WA0029.jpg
IMG-20241114-WA0027.jpg
IMG-20241114-WA0026.jpg
 
Back
Top Bottom