Doctor Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,057
- 2,621
DR. IRENE C. ISAKA, DG WA NHIF
Hadi mwishoni mwa mwaka 2021 ni 15% ya Watanzania walikuwa wanapokea huduma za tiba kwa njia ya bima ya afya.
Takwimu hizi zilijumuisha 8% kupitia taasisi ya NHIF, 6% kupitia taasisi ya iCHF, na 1.3% kupitia mifuko ya bima inayoendeshwa na watu binafsi.
Sasa Mamlaka ya Taifa ya Bima ya Afya ya Tanzania (NHIF) imeanza kutekeleza mkakati wa kupanua huduma ya bima.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa tarehe 17 Desemba 2024, mamlaka hii imezindua vifurushi vinne vipya vya huduma za bima ya afya kwa raia wote wenye uwezo wa kuchangia gharama za tiba (Kiambatanisho A)
Vifurushi hivyo vinavyounda piramidi lenye ngazi nne ni kama ifutavyo:
- Kifurushi cha SERENGETI chenye huduma 1,800. Mchango wa mwanachama kwa mwaka ni TZS 660,000 (Kiambatanisho B)
- Kifurushi cha NGORONGORO chenye huduma 440. Mchango wa mwanachama kwa mwaka ni TZS 240,000. (Kiambatanisho C)
- Kifurushi cha TOTO AFYA KADI MTAANI, kwa ajili ya mtoto aliye chini ya miaka 17 anayesajiliwa mmoja mmoja mitaani. Mchango wa mtoto mmoja kwa mwaka ni TZS 150,000 (Kiambatanisho D)
- Na kifurushi cha TOTO AFYA KADI SHULENI, kwa ajili ya mtoto aliye chini ya miaka 17 anayesajiliwa pamoja na wenzake shuleni kama kundi moja. Mchango wa kila mtoto aliye katika kundi husika ni TZS 50,400. Kifurushi hiki kilifutwa na sasa kimerejeshwa upya (KIAMBATANISHO D)
Uzinduzi wa vifurushi hivi vipya ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya bima ya afya kwa raia wote inayolenga kuwapunguzia watu tatizo la maisha yao ya kila siku kuyumbishwa na gharama za matibabu zinazolipiwa kwa fedha taslimu.
Sera hii ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kutekeleza Ajenda ya Dunia Kuelekea mwaka 2030 iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015, hasa katika lengo namba 3.8 linaloongelea utoaji wa huduma za afya kwa watu wote ("universal health coverage --UHC)"
Kwa mujibu wa sera hii haki ya kila binadamu mgonjwa kupata matibabu inatokana na ukweli kuwa kila mtu anayo haki ya kuwa na afya bora kadiri inavyowezekana.
Hivyo, sera hii inasisitiza kuwa mfumo wa huduma za bima ya afya kwa wote lazima ufanikishe malengo matano yafuatayo:
- Kuhakikisha kuwa kila raia, kila mahali alipo na kila wakati akiugua anapata huduma ya tiba anayoitaka yeye, katika mipaka ya ukomo wa rasilimali za kitabibu zilizopo (accessibility);
- Kuhakikisha kuwa huduma za tiba zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora vilivyobainishwa kitaalam (quality); na
- Kuhakikisha kuwa kanuni za haki ya kijamii zinazingatiwa katika kubuni na kutekeleza vifurushi vya huduma za bima ya afya. Yaani, kuhakikisha kuwa watu wote wenye uwezo sawa wa kipato wanapata huduma sawa, na wagonjwa wote wenye vipato tofauti wanapata huduma tofauti, kila mahali na kila wakati, katika namna inayotabirika (social justice/equity)
- Kuhakikisha kuwa hakuna tabaka la watu linaachwa nje ya huduma za tiba kwa sababu tu ya kutokuwa na fedha za kuchangia gharama za matibabu (inclusivity)
- Na kuhakikisha kuwa mfuko wa bima ya afya unao uwezo na utayari wa kutoa huduma siku hadi siku, wiki hadi wiki, mwezi hadi mwezi na mwaka hadi mwaka (sustainability).
Aidha, kwa sababu hizi sehemu ya taarifa kwa umma iliyotolewa na uongozi wa NHIF inatamka kwamba:
"...mfuko wa NHIF unawahamasisha wananchi kuendelea kujiunga na Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa huduma za matibabu wakati wote bila kikwazo cha fedha kupitia mtandao mpana wa zaidi ya vituo 10,000 vya kutolea huduma za afya vilivyosajiliwa na mfuko nchi nzima. "
Maana ya wito huu ni kwamba, wananchi wote wenye uwezo wa kuchangia gharama za kuendesha mfuko wa huduma za tiba tunatakiwa kujiunga na mfuko wa NHIF na kuanza kuchangia kabla ya kuugua ili wltuweze kuwa na uhakika wa matibabu bila ulazima wa kuwa na fedha taslimu mkononi pale tutakapougua.
Hata hivyo, wito huu maana yake ni kwamba, vifurushi hivi haviwahusu raia wasio na uwezo wa kuchangia gharama za kuendesha mfuko wa huduma za tiba.
Kundi hili ndio kiini cha changamoto kuu inayoikabili serikali yenye jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna raia anaachwa nyuma hadi kufa kwa sababu ya kukosa fedha ya matibabu.
Tangu enzi za hayati Magufuli serikali ilikuwa ikipambana sana kubuni utaratibu wa kukusanya mapato yatakayotumika kuendesha mfuko wa bima ya afya utakaowagusa watu hawa pia.
Wakati ule, Tanzania ilikuwa na watu 55,000,000.
Na ilibainika kuwa, hadi Desemba 2018 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za mkononi wanaopiga simu za sauti 40,621,499; wanaotumia data/intanet 23,142,960; na wanaotuma na kupokea fedha 23,367,826.
Kutokana na takwimu hizi ilkuwa wazi kwamba, wastani wa miamala ya simu kwa kupiga simu ya sauti kwa kila mtumiaji kwa mwezi (Average Revenue per User per month--ARPU/Month) ilikuwa ni TZS 16.362/=;
Aidha ARPU/mwezi ya watumiaji wa data ilikuwa ni TZS 374; na ARPU/mwezi ya miamala ya fedha ilikuwa ni TZS 8,528,970.
Kwa kuigiza mantiki ya kutumia TANESCO kukusanya makato ya REA (3%) na EWURA (1%), ilipendekezwa kuwa makampuni ya simu yanaweza kutumika kukusanya makato ya NHIF (0.5%) yaliyopendekezwa.
Mahesabu yalionyeshwa kwenye jedwali lifuatalo hapa chini.
Kutokana na takwimu hizi ilihitimishwa kwamba Taifa lingeweza kutoa bima ya afya kwa raia wote milioni 55, kwa kutumia mfumo wa kuchangia gharama, ambapo serikali ingemchangia kila mtu TZS 218,210/= kutokana na chanzo hiki cha mapato. (Tazama jedwali hapo juu)
Hii maana yake ni kwamba, kwa njia ya kuchangia, kila raia akichangia kiasi cha kujazia upungufu baada ya serikali kuchangia TZS 218.210/= kwenye mfuko wa bima ya afya.
Utafiti wa kujua kiasi gani mwanachama achangie ulikuwa bado unaendelea hadi Magufuli alipofariki.
Sheria ya bima ya afya kwa wote namba 13/2023 imetungwa baada ya kifi chake pia.
Sera hii inasema kuwa kila mwajiriwa, katika sekta binafsi na serikalini, atachangia kwa lazima.
Pia sera hii inatambua uwepo wa kundi la watu wasiojiweza kabisa. Lakini haielezi mkakati mahsusi ya kuwagusa watu hawa.
Hivyo, kwa kuzingatia matakwa ya mche mraba wa huduma za afya kwa wote (universal health coverage cube), wito wangu kwa serikali ni kwamba, pamoja na uzuri wa vifurushi hivi vilivyotangazwa, bado kazi ya kufanya ipo. Hivyo:
(1) Juhudu ziendelee kufanyika ili kupanua huduma kwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za bima ya afya vilivyosajiliwa na mfuko nchini ili tuweze kusogeza huduma karibu na wananchi wengi zaidi.
(2) Juhudi ziendelee kufanyika ili kuhakikisha kuwa idadi ya huduma zilizo katika kila kifurushi zinaongezeka siku hadi hadi siku, na idadi ya vifurushi ikiwa inaongezeka siku hadi siku pia.
(3) Na juhudi ziendelee kufanyika ili kuhakikisha kwamba mchango wa kifedha kutoka serikalini kutokana na kodi unaongezeka siku hadi siku ili gharama zinazochangiwa na wananchi kutoka mifukonj mwao kwa ajili ya tiba zipungue siku hadi siku.
Kwa sasa watanzania wanaopata huduma za matibabu kwa njia ya bima ya afya hawazidi asilimia 15 ya raia wote. Bado safari ni ndefu.
KIAMBATANISHO A: PRESS RELEASE
KIAMBATANISHO B: KIFURUSHI CHA SERENGETI
KIAMBATANISHO C: KIFURUSHI CHA NGORONGORO
-- Tazama Kiambatanisho B
KIAMBATANISHO D; KIFURUSHI CHA TOTO AFYA KADI