Desemba 16, 2022.Dar es Salaam: -Mwaka 2022 umekuwa mwaka mzuri kwa tasnia ya muziki wa Tanzania, tukishuhudia kuibuka kwa wasanii mbalimbali wanaochipukia, wasanii wakijituma zaidi ya kawaida kwenda kwenye viwango vya juu na kutambulika kimataifa.
Mwaka umeshuhudia wasanii takriban sita wa Tanzania wakijiunga na ‘Boomplay Golden club’. Hii ni klabu mahususi kwa wasanii waliopata wasikilizaji zaidi ya milioni mia moja Boomplay huku Tanzania ikiwa nchi ya pili kwa kuwa na wasanii wengi baada ya Nigeria.
Katika kufunga mwaka huu mzuri katika tasnia ya muziki, App namba moja kwenye utoaji wa huduma ya kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika, Boomplay, imetoa takwimu zake za kila mwaka ambazo zimekuwa zikisubiriwa kwa hamu.
#BoomplayRecap2022 hutoa muhtasari wa matumizi ya muziki na uchambuzi kuhusu ladha na machaguo ya wasikilizaji ndani ya mwaka. Pia, huwawezesha watumiaji wa App kupata orodha zao binafsi za nyimbo bora, wasanii, albamu na aina ya muziki.
Boomplay Recap inawasilisha data na uchambuzi kuhusu matumizi ya muziki Boomplay huku ukaguzi ukifanyika katika kipindi mahususi.
Inaangazia na kugawanya data za muziki kulingana na nchi husika, wasanii na watumiaji na kwa kufanya hivyo, hutoa taswira halisi ya usikilizaji wa muziki na tabia za kujihusisha na muziki kwa tasnia za ndani barani Afrika.
Usahihi na umuhimu wa data na chati za Boomplay kama picha sahihi ya matumizi ya muziki inategemea msingi wa watumiaji wa Boomplay, ambao kwa kiasi kikubwa ni demografia ya tabaka la chini na la kati ambayo ni sehemu kubwa zaidi ya watu katika bara.
Hivyo ni jumuishi na hunasa ladha ya muziki wa ndani na tabia za watumiaji wa muziki. Usikilizaji wa muziki Boomplay umekua kwa mwaka wa 2022 kwa asilimia 248, ukichangiwa na watumiaji wake milioni 88 wanaotumia App kila mwezi na ongezeko la idadi ya nyimbo Boomplay zaidi ya milioni 90.
Kwa mwaka wa 2022, Boomplay Recap kwa kila nchi inaangazia kategori mbalimbali kama vile;- Wasanii Bora wa Kiume, Wasanii Bora wa Kike, Wasanii wanaovuma zaidi, Nyimbo na Albamu zilizosikilizwa zaidi, miongoni mwa nyinginezo, huku Recap ya wasanii ikitoa takwimu za mwaka 2022 za wasanii binafsi, ikiwa ni pamoja na usikilizwaji wa jumla, masaa ya usikilizwaji, Wimbo uliosikilizwa zaidi na Nchi ambayo msanii amesikilizwa zaidi.
Kwa upande mwingine, watumiaji wa App ya Boomplay (Boombuddies) watapata taarifa binafsi kuhusu matumizi yao ya muziki na ushiriki wao kwenye App ya Boomplay kupitia ‘Users Recap’ ambayo inaangazia safari yao ya muziki kwa mwaka 2022 kwa kutoa maelezo kama vile idadi ya nyimbo walizosikiliza, aina ya mziki wao pendwa, muziki mpya, wasanii maarufu, nyimbo walizozirudia mara kwa mara na taarifa nyingine binafsi za kuvutia.
Kulingana na taarifa kutoka kwenye Boomplay Recap Tanzania, Diamond Platnumz, Harmonize na Marioo ndio wasanii watatu wa kiume walioongoza kusikilizwa zaidi kwenye kipengele cha ‘Wasanii wa Kiume waliosikilizwa zaidi’ huku kwa upande wa wasanii wa kike, Zuchu, Nandy na Maua Sama wakiwa kwenye kipengele cha ‘Wasanii wa kike waliosikilizwa zaidi’. Ni vyema kutambua kuwa Zuchu amekuwa akiongoza kipengele hiki kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa.
Katika kipengele cha wimbo uliosikilizwa zaidi Boomplay kwa mwaka 2022 ni wimbo wa Jay Melody ‘Nakupenda’. Wimbo wa Marioo ‘Naogopa’ aliomshirikisha Harmonize ukikamata nafasi ya pili huku ‘Utu’ wa msanii Alikiba ukikamata nafasi ya tatu.
Komando wa Yesu anaongoza katika kipengele cha nyimbo za Injili kupitia wimbo wake uliopata umaarufu mkubwa unaofahamika kama ‘Yamebadilika’ ‘Neema Semfukwe anashika nafasi ya pili na wimbo wake unaofahamika kama ‘Ndio’ huku Ni wewe wa Mathias Walichupa ukinyakua nafasi ya tatu. 'Ni wewe' ni wimbo ulioingia kwenye kipengele hiki kwa mara ya pili mfululizo sasa.
Wasanii wa Tanzania walioshamiri zaidi kwa mwaka 2022 ambao wamekuwa na mwaka mzuri wa ukuaji ni pamoja na;- Jay Melody, Marioo na Phina kwa kila mmoja kuwa na wimbo ambao umepata wasikilizaji zaidi ya milioni 10.
‘Nakupenda’ ya Jay Melody ikiwa na wasikilizaji zaidi ya milioni 44.5, Mi Amor ya Marioo ikiwa na wasikilizaji zaidi ya milioni 32.7 na Phina ‘Upo Nyonyo’ ikiwa na wasikilizaji zaidi ya milioni 10.8M.
Baadhi ya mambo mengine kulingana na data za wasikilizaji wa Tanzania kwa 2022, ni pamoja na wimbo uliopendwa na Watanzania siku ya kwanza ya mwaka 2022 ambao ni wimbo wa Diamond Platnumz ‘Unachezaje’.
Katika Siku ya Wapendanao ya mwaka 2022, Wimbo wa ‘Mwambieni’ wa Zuchu ndio wimbo uliosikilizwa zaidi. Wimbo unaopendwa kusikilizwa nyakati za asubuhi ni wimbo wa Christina Shusho ‘Shusha Nyavu’ na wimbo unaopendwa zaidi wa usiku wa manane kwa mwaka 2022 ni wimbo wa Marioo la Mi Amor wenye maadhi ya acoustic.
Boomplay imekuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya usikilizaji wa muziki barani Afrika. Imedhamiria kutumia ushirikiano wa kimkakati na mipango ya maendeleo ili kuwezesha mfumo wa muziki kidijitali wa Afrika kutambua uwezo wake.
Ushirikiano wa hivi karibuni na Redio ya Generations ya nchini Ufaransa na Kampuni ya mawasiliano ya TIGO Tanzania ni hatua ya kukuza maendeleo ya utamaduni wa usikilizaji muziki kidijitali na utumiaji wa muziki kwa njia ya halali huku ukipanua wigo wa wasanii kimataifa na kusaidia tasnia ya muziki wa Tanzania kuwa na manufaa zaidi na yenye manufaa kwa pande zote.
Playlists za #BoomplayRecapTZ2022 kwa sasa zinapatikana kwenye App ya Boomplay kwenye maadhi au aina tofauti za muziki, zikijumuisha wasanii wote na nyimbo zao na zaidi ili watumiaji wafurahie na kuhuisha nyimbo na matukio wanayopenda ya 2022. Playlists hizo zinapatikana kwenye sehemu ya ndani ya App ambayo imepewa kichwa cha ‘Boomplay Recap 2022’.
2022 Boomplay Recap Tanzania. Fuatilia mazungumzo kupitia #BoomplayRecapTZ2022 #BoomplayRecap2022
Wasanii wa Kiume walioongoza 2022
1. Diamond Platnumz
2. Harmonize
3. Marioo
Wasanii wa Kike walioongoza 2022
1. Zuchu
2. Nandy
3. Maua Sama
Nyimbo zilizoongoza kusikilizwa 2022
1. Nakupenda-Jay Melody
2. Naogopa-Marioo ft Harmonize
3. Utu-Alikiba
Wasanii walioshamiri 2022
1. Jay Melody
2. Marioo
3. Phina
Albamu zilizoongozwa kusikilizwa 2022
1. First of All-Diamond Platnumz
2. Love Sounds Different-Barnaba
3. Only One King-Alikiba
Nyimbo zilizoongoza kwenye chati
1. Naogopa-Marioo ft Harmonize
2. Nakupenda-Jay Melody
3. Utu-Alikiba