DC KINONDONI AWASHUKIA WAHUJUMU WA MIUNDOMBINU YA MWENDOKASI
*49 watiwa mbaroni
*5 wapata dhamana
*1 apanda kortini
* 43 kulala weekend mahabusu
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo amekutana na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tatizo la uhujumu wa miundombinu ya Mwendokasi.
Katika taarifa yake Mh. Hapi ameeleza kuwa katika kipindi cha siku mbili watu 49 wamekamatwa na polisi wilayani Kinondoni wakiwemo wamiliki wa magari, bajaji na bodaboda kwa makosa ya kuingilia miundombinu ya Mwendokasi kinyume cha sheria. Kati yao watuhumiwa 43 watapelekwa mahakamani siku ya jumatatu ijayo hali inaowafanya kuyatumia mapumziko ya Juma wakiwa mahabusu.
Mh. Hapi amewataka wananchi wa Kinondoni na hasa madereva kufuata sheria, vinginevyo watakabiliana na rungu la dola.
Aidha, Mh. Mkuu wa Wilaya ameagiza Polisi wilayani Kinondoni kuendelea na zoezi la kuwakamata wale wote wanaogeuza vivuko vya barabara za DART kuwa sehemu za kulala na kujisaidia.
"Tumewaagiza Polisi kuwakamata wote wanaolala na kujisaidia kwenye vivuko vya barabara. Hata wale ambao wamesimama kule juu saa za usiku bila kazi yoyote wakamatwe na washitakiwe kwa sheria za uzembe na uzururaji. Wengine hawa ni vibaka na wengine ndio wanaolala na kujisaidia huko usiku." Alisema Hapi.
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli akizungumza na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam alizungumzia juu ya uhujumu wa miundombinu ya mwendokasi na kuagiza watu hao kushughulikiwa ipasavyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya aliutaka uongozi wa DART kuchukua tahadhari za kiusalama katika vituo vya mabasi ili kuzuia uwezekano wa kutokea tishio la usalama. Hapi aliwataka DART kuweka utaratibu wa kuwakagua abiria kwa mashine za mikono za ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaopanda mabasi hayo.