DC KILAKALA AKABIDHI MILIONI 699.4 MIKOPO YA ASILIMIA 10
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala, amesisitiza juu ya matumizi sahihi ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu , akibainisha kuwa mikopo hiyo ni fursa muhimu ya kuimarisha maisha ya wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo hiyo, Kilakala ameleza kuwa matumizi mabaya ya mikopo yanaweza kuathiri maendeleo ya wanufaika na kuwataka wazingatie dhamira ya serikali ya kuwainua kiuchumi.
Naye, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Hilary Sagary amewakumbusha wanufaika kuwa mikopo hiyo si zawadi, bali ni deni linalopaswa kurudishwa kwa wakati ili wengine nao wanufaike
Pia, Amewataka wajasiriamali kuhakikisha wanazingatia mipango mizuri ya kibiashara ili waweze kurejesha mikopo na kupata nafasi ya kukopa tena kwa maendeleo zaidi.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema lengo kuu la mikopo hiyo ni kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka ngazi ya chini hadi ya juu
Ameongeza na kusema kuwa mikopo hii inalenga kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa wananchi na kuchangia maendeleo ya mji wa Morogoro kwa ujumla.
Aidha, Mwenyekiti wa Wamachinga Wilaya ya Morogoro amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya mikopo hiyo, akiwahimiza wanufaika kuzingatia nidhamu ya kifedha na kuwekeza katika biashara zenye tija. Amesema nidhamu hiyo itawasaidia kukuza mitaji yao na kuleta maendeleo endelevu.