Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,828
- 13,585
Mahafali ya 28 ya Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) kwa ajili ya kutunukiwa Astashahada na Stashada yanafanyika leo Ijumaa Desemba 15, 2023 Ilala Jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi wa shughuli hiyo ambayo inafanyika kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) ni Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo.
MKUU WA CHUO
Mkuu wa Chuo cha DSJ, Johnson Soah anahutubia, haya ni baadhi ya mambo ambayo anayazungumza:
Shughuli kubwa tunayoifanya katika hadhara ya leo ni kuwatunuku vyeti wahitimu wetu wa mwaka wa masomo 2022/2023. Kwa hakika, tunastahili kujipongeza kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi yenye taaluma, ambayo ni chachu ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Miongoni mwa faida kubwa za kuwepo kwa vyuo vya kati ni kuhakikisha kuwa vinatoa wataalam kwa fani mbalimbali ambao ni watendaji kazi na sio nadharia pekee na hivyo kukidhi mahitaji ya msingi ya jamii moja kwa moja, vinatoa elimu na mafunzo ambayo moja kwa moja yanamwezesha muhitimu kuajiriwa, kujiajiri ama kuendelea na masomo ya elimu ya juu yaani Chuo Kikuu.
Tumekuwa tunatoa mafunzo kwa vitendo katika Studio zetu za TV na Radio pamoja na utayarishaji wa gazeti. Pia tunacho chumba maalum (Multi Media Theatre) kwa ajili ya wanafunzi kufanya tathimini ya kazi zao ambapo wataonyeshwa makosa yao na kuelekezwa jinsi ya kujisahihisha ili kuboresha matangazo na vipindi vya Radio na Runinga.
Wahitimu
Mahafali ya Mwaka 2022 tulipata wahitimu wa Stashada 134, wahitimu wa Astashahada walikuwa 231 jumla yao ni wahitimu 365.
Mwaka huu (2023) tuna wahitimu 183 wa Astashada na wahitimu 126 wa Stashahada, jumla yao ni wahitimu 309.
Kwa wastani wa takwimu hizi ina maana kuwa kwa muda wa miaka zaidi ya 10 ya uhai wa Chuo, ni wazi kuwa Chuo kimetoa zaidi ya wahimu 5,000 kwenye tasnia ya utangazaji na uandishi wa habari.
Tunaamini katika msemo kuwa “Information is Power” hivyo basi tumeiongezea nchi nguvu kwenye eneo la mawasiliano na upashaji habari na hivyo kuharakisha shughuli za maendeleo.
Malipo ya Ada ni Changamoto
Mojawapo ya changamoto kubwa zinazotukabili ni pamoja ucheleweshaji wa malipo ada. Kwa kipindi sasa tumekuwa tukishuhudia Wazazi/walezi wakichelewa kulipa ada za wanafunzi kwa maelezo kuwa “hali ni ngumu’” Pamoja na kwamba ada zetu sio kubwa kulinganisha na vyuo vingine, bado wazazi/walezi wanashindwa kulipa ada kwa wakati, hali ambayo kwa kiasi fulani inakwamisha maendeleo ya Chuo.
Kukosa sehemu ya kufanyia mazoezi
Changamoto nyingine ni Wanafunzi kukosa sehemu za kufanyia mazoezi sehemu za kazi, hii inakwamisha si maendeleo na mafunzo lakini pia inasababisha usumbufu.
Pia uchakavu wa miundo mbinu, DSJ ni wapangaji wa BASATA ambayo miundombinu na majengo yake ni ya tangu Uhuru. Changamoto hii tumejaribu kuipunguza kwa kushirikiana na Uongozi wa BASATA kwa kufanya matengenezo ya lazima tu.
DSJ kuhamia Kiluvya
Ujenzi wa chuo unaendelea katika eneo la Kiluvya, Mungu akipenda na mambo yakienda sawa Mapema Mwakani yaani 2024 tutahamia.
Natoa shukrani maalumu kwa Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums kwa kuacha shughuli zako muhimu za kimeaendeleo na kuja kushiriki nasi kufanikisha mahafali haya.
Maxence Melo anazungumza
Binadamu yeyote anategemea taarifa ili afanye maamuzi sahihi, ubovu wa taarifa unaweza kusababisha maamuzi mabovu.
Ninyi kama Wanahabari mna nafasi ya kusaidia jamii kutokana na aina ya taarifa mtakazotoa kupiti taaluma yenu, Demokrasia yoyote Duniani inategemea taarifa.
Wananchi ambao hawana taarifa hawatakuwa na uwezo wa kuwajibisha Serikali zao.
Unapofanya mambo yako kawaida hautafanikiwa, unatakiwa kubadilika na kufanya vitu kwa kutumia uwezo wa ziada.
Acheni uwoga katika kila kitu, hofu yako ndio anguko lako, ukiwa na hofu na kutofanya maamuzi hapo ndipo unapoanguka.
Hata kwenye kazi, onesha kila ulichonacho kisha watu wataona uwezo wako.
Nawapongeza wahitimu wote, hamjafika hapo kirahisi, mmepambana sana, Mungu awabariki sana.