The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 746
- 2,093
Moja kwa moja kwenye mada. Huenda mimi si hadhira sahihi kwa baadhi ya maudhui fulani ambayo wengine wanayapenda huko mtandaoni. Hata hivyo, maudhui yanaposambazwa waziwazi mtandaoni, mtu yeyote anaweza kuyaona na watengeneza maudhui hawawezi kujua kwa uhakika kama maudhui yao yatafikia tu hadhira iliyolengwa.
Kwa hiyo ni jambo la kawaida kabisa kwamba maudhui yale yale yanaweza kuonekana kuwa ya kukera kwa baadhi ya watu, yanaweza kuwa ya kufumbua macho kwa wengine. Jinsi tunavyotafsiri maudhui yoyote katika upokeaji wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii pia inaweza kutofautiana kulingana na mitazamo yetu.
Mimi naamini kuwa si maudhui yote yanayostahili kuchapishwa au kusambazwa, ingawa pia naelewa kuwa si watumiaji wote wa mtandao wanasambaza maudhui mabaya kwa makusudi.
Uhalisia ni kwamba katika dunia ya smartphones watengeneza maudhui ya mtandaoni wamekuwa na ushawishi mkubwa, hasa kupitia majukwaa kama vile Instagram na TikTok, ambako maudhui ya video yanatazamwa na kusambazwa kwa kasi kubwa. Hata hivyo, suala hili halijakosa changamoto, hususan pale ambapo utu wa watu wanaohusika kwenye video hizo hauzingatiwi.
Hawa ‘content creators’ mara nyingi hutengeneza video zenye lengo la kupata umaarufu na ushawishi wa haraka bila kuzingatia madhara wanayoweza kupata wale wanaotokea kwenye video hizo kama vile kuathirika kisaikolojia na hata kuingia kwenye msongo wa mawazo baadaye.
Maudhui ya mtandaoni mara nyingi huchukuliwa kama ya burudani au vichekesho, lakini mara nyingi yanajikita kwenye kashfa, fedheha, au hata unyanyasaji. Tunapo-scroll mtandaoni tunaona namna ambavyo ‘content creators’ wanawarekodi watu bila ridhaa zao, kuwaweka kwenye hali ya aibu, au kuwakashifu hadharani, hali ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa ya kisaikolojia kwa wahusika.
Mifano ya hali hizi inajumuisha watengeneza maudhui wanaochapisha video za watu wenye mwonekano wa kipekee, kasoro za kimwili, au tabia za ajabu bila ridhaa yao. Kwa mfano, kuna matukio kadhaa ya watu wenye changamoto za kimaumbile au ulemavu kufanyiwa mzaha mtandaoni, hali inayoweza kuwa chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo na kudhoofisha hali ya kisaikolojia ya mhusika.
Hali hii inachangiwa na ukweli kwamba maudhui haya hupokelewa na idadi kubwa ya watazamaji ambao wanaweza kuchangia kutoa maoni ya dhihaka au kukashifu zaidi, hali inayoongeza presha kwa mhusika aliye kwenye video.
Maudhui yanayomfedhehesha mtu yanaweza kuwa na athari za muda mrefu, hasa katika enzi hii ya mtandao ambako maudhui yanabaki mtandaoni kwa muda mrefu na huweza kusambaa haraka sana.
Katika baadhi ya nchi duniani kumekuwa na juhudi za kuwalinda wahusika wanaotumiwa kwenye video bila ridhaa yao. Kisheria, matumizi ya picha au video za mtu bila ridhaa yanaweza kufikishwa mahakamani kwa msingi wa ukiukaji wa haki za faragha, lakini utekelezaji wa sheria hizi kwenye majukwaa ya kidijitali bado unaelezwa kuwa ni changamoto.
Ni wazi kuwa ‘content creators’ wanapaswa kuwa na wajibu wa kimaadili katika kutengeneza na kusambaza video zao. Hii inahitaji kuwa na utamaduni wa kuzingatia utu, ridhaa, na haki za faragha za watu wanaohusishwa kwenye maudhui hayo. Watengeneza maudhui wanahitaji kuelewa kwamba mtu anayekuwa kwenye video, hata kwa dakika chache tu, anaweza kuathirika kwa muda mrefu.
Kushindwa kuzingatia utu wa watu sio tu kwamba kunavunja misingi ya maadili ya kijamii, bali kunaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya na kijamii kwa wahusika. Hivyo, ni jukumu la kila mmoja kuzingatia utu, heshima, na faragha ya watu.