Adolf Hitler, Jean Bokassa, Idi Amin, Mobutu Seseko, Mussolin, na wengineo wengi wanaofahamika duniani, kuingia madarakani na kumudu kwao kuwa madikteta kunatokana na wananchi wa nchi zao kukumbwa na umaskini uliokithiri na kuchochwa na kutokuwa na Imani na mfumo wa uendeshaji wa serikali katika nchi zao.
Nchi zilizowahil kuzalisha madikteta mara zote madikteta hao ama huchaguliwa na wananchi au hupindua serikali zilizopo madarakani kwa ahadi ya kwenda "kusafisha uozo" uliopo serikalini. Na Historia inaonesha Madikteta hao wakiingia madarakani hulazimisha ama hufanya hila za kutaka kusifiwa kwa kila jambo walifanyalo kwa hoja kwamba wanafanya kwa maslahi ya taifa.
Lakini baadaye wapambe wao huanza kutengeneza Propaganda kuwa kwa jinsi Dikteta huyo anavyosafisha uozo hakuna haja ya kuwa na uchaguzi ama kumpinga mtu safi mwenye nia ya kuirejesha jamii kwenye njia sahihi. Pia huinogesha propaganda yao kwamba kufuata sheria ndiko kulikoifikisha jamii kwenye uozo uliopo.
Ikishafika hapo sheria huwa ni huyo kiongozi na wapambe wake na kama ikibidi mahakama kuhusishwa basi hutolewa maagizo mahususi kwa mahakimu "ili kulinda maslahi mapana ya taifa". Kwa bahati mbaya Madikteta wote huingia madarakani wakati wananchi wa nchi husika wakiwa na msongo wa mawazo na uchovu wa fikra uliosababishwa na mfumo wa siasa uliopo, kiasi kwamba wakosoaji wao huonekana kama ni adui wa jamii.
Ni Madikteta ambao huumbwa na jamii na wala wao siyo wanaoiumba jamii wanayoitawala!!