Tuesday, July 5, 2016
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani, alisema kama polisi wana ushahidi wa viongozi wa CUF na wafuasi wao kujihusisha na matukio ya uvunjifu wa amani basi wawapeleke mahakamani.
Bimani alisema wanasikitishwa na hatua ya jeshi hilo kuwaweka ndani viongozi na wafuasi wao kwa muda mrefu bila ya kuwafikisha mahakamani kinyume na haki za binaadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kama wana ushahidi juu ya viongozi wetu ambao wanawahusisha na matukio ya uvunjifu wa amani kisiwani Pemba basi wawapeleke mahakamani,” alisema Bimani.
Bimani alisema kuwa tokea kuanzishwa mfumo wa vyama vingi Tanzania kumekuwa na unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya raia hasa wanachama wa CUF jambo ambalo alisema kuwa linafanyika kwa nia ya kukikandamiza chama hicho.
“Ikiwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo kila wakati Zanzibar imekuwa ikishuhudia kuletwa askari wengi katika kipindi cha uchaguzi,” alisema Bimani.
Hata hivyo, alisema kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, kumekuwa na hatua kadhaa za unyanyasaji dhidi ya wafuasi wa chama hicho unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Haya yote yanayofanyika ili kuzima sauti za watu, lakini tunawaambia viongozi wa CCM pamoja na vyombo vya dola, tutaendeleza msimamo wetu wa haki sawa kwa wote,” alisema Bimani.
Alisema CUF inalaani vitendo vya hujuma dhidi ya raia na mali zao unaofanywa kwa lengo la kuvipa sababu vyombo vya ulinzi na hasa wafuasi wake, pamoja na kulaani kauli za vitisho na lugha za kibabe zinazotolewa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kama vile iliyotolewa Juni 28 mwaka huu na Naibu Mkurugenzi wa Upepelezi Salum Msangi kisiwani Pemba kwa lengo la kuwanyamazisha wananchi ili kuisambaratisha CUF.