Boniface Jacob (Boni Yai): Salamu kutoka Segerea (Ujambazini)

Teko Modise

JF-Expert Member
May 20, 2017
2,276
7,546
SALAMU KUTOKA UJAMBAZINI..

Najua ukisikia neno “ujambazini” lazima utashtuka kidogo. Nikutoe hofu neno kabisa. Neno ‘ujambazini’ ni jina la eneo kama ilivyo Posta, Masaki au Manzese.

Nikupeleke sasa Ujambazini huko. Ujambazini ni Magharibi mwa Jiji la Dar es salaam, na kusini mwa Wilaya ya Ilala, kuna sehemu maarufu inaitwa Segerea.

Segerea ni kata katika halmashauri ya Manispaa ya Ilala yenye mitaa ya Ugombolwa, Mfaume, Mgombani na Segerea yenye wakazi 83,000 na KM za mraba 9.6,

Segerea imezungukwa na Kata za Kimanga, Kinyerezi, Tabata na Kipawa. Mtaa wa Segerea kuna Gereza Kuu la Mahabusu Mkoa wa Dar es salaam linaitwa SEGEREA.

Segerea ni gereza maarufu Mkoa wa Dar es salaam. Ni Gereza Kongwe lenye mazingira ya kutisha na kuogopesha. Limezungukwa na mapori na vilima.

Mapori hayo ya kutisha na vilima hivyo vingi vilivyozunguma gereza la Segerea husababisha utulivu mkubwa sana ndani ya gereza la Segerea.

Sasa nikuchukue nikupeleke ndani ya Gereza bila amri ya mahakama, bila kesi na bila pingu mkononi. Yaani, kimawazo tu ujihisi na wewe upo Gerezani.

Ndani ya gereza Kuu la Mahabusu Dar es Salaam - Segerea kuna sehemu kubwa na maarufu kama tano;

Sehemu ya kwanza; nje ya gereza, wageni hufika na kusubiri utaratibu wa kuingia ndani kuona ndugu zao. Kuna Canteen, Duka na eneo la kukaa wageni.

Sehemu ya pili; Jengo la Utawala ambalo ndiyo ofisi ya Mkuu wa Gereza maarufu “Bwana Jela” na askari wake wanasimamia wafungwa na mahabusu ndani ya gereza.

Sehemu ya tatu; “ujambazini”, huko kuna vyumba vya Jela 10 na kila Kimoja kina idadi maalum ya watu, mfano namba 10 inachukua watu zaidi ya 200 na zaidi.

Sehemu ya nne; Upande maalum (Special Wing) wanaishi mahabusu au wafungwa ambao ni watoto chini ya miaka 18, mahabusu, wafungwa wachache

Sehemu ya tano; “PC - Private Cell”. Huko hupelekwa watu watukutu au wanaotenda makosa wakiwa ndani ya gereza nje na makosa wanayopelekwa nayo gerezani.

Huko katika private cell (PC) - kuna vyumba maalum ambavyo mtu hutengwa pekee yake na kupata mlo mmoja kwa siku. Ni kama sehemu ya kutoa adhabu.

UJAMBAZINI

Rudi nyuma siku ya alhamisi 19 September 2024 majira ya saa 4 usiku. Muda nilishushwa na msafara wa Polisi wakiwa na gari mali ya Jeshi la Polisi na Polisi kibao.

Baada ya kupokelewa na kujazwa katika Kitabu, natupa Jicho la udadisi ubaoni getini,hesabu zinasoma jumla mahabusu na wafungwa 1,011 wanaume na wanawake.

Sasa rasmu hadi hapo nipo chini ya ulinzi wa askari Magereza - Segerea. Mamwela wamenimwaga halafu wao wakasepa kwa mbwembwe kama walivyokuja.

Mapokezi katima lango la gereza kwanza wananijua kwa majina yote matatu wengine wanaiita Boniface Jacob, Mstahiki meya na baadhi wakanitambua kama Boniyai,

Wananisalimia halafu wananiacha, wanasogea pembeni wanamuuliza incharge wao, tumpeleke wapi? Jibu linatoka kwa incharge wao mpelekeni UJAMBAZINI!

Rohoni nikaguna. kwanini ujambazini? Mwisho nikakumbuka somo la utayari (The chameleon principal) “ukikutana na wahuni kuwa muhuni mwenzao.”

Kweli. Jamaa wakanipekua kisha wakaanza kuniogoza kuelekea ujambazini. akilini najiandaa kwenda kukutana na majambazi hatari na watu katili sana gerezani.

Nakaribia mlangoni pembeni dirishani naona ndani watu wamelala wanakoroma, muda huo taa zinawaka kwa mwanga mkali sana kama karabai za wavuvi.

Nyapara wa selo namba 10 kijana mmoja mrefu, anaitwa MWITA, anakabidhiwa anipokee anitafutie sehemu ya kulala ndani ya selo ambapo ndiyo kiongozi wake.

Kabla hawajaniacha wakaniuliza, Boniyai umekula? nikakumbuka kauli ya mama “ugenini siku ya kwanza usije ukavunga kuhusu chakula, utaanza vibaya”

Nikajibu sijala tangu asubuhi, nilipelekwa Mahakamani Kisutu saa 10 jioni na usiku wa Saa 3 ndiyo shauri langu lilihairishwa na hadi jumatatu ya 23 September 2024

Tukiwa wote tumesimama mlangoni, jamaa wanaulizana kama Jikoni kuna ugali na maharage, kwa bahati mbaya wanajibiwa hakuna kitu chochote kilichobakia.

Itaendelea…
 
SALAMU KUTOKA UJAMBAZINI (PART 2)

Tukiwa wote tumesimama lango la Selo namba 10 pale Ujambazini jamaa wanaulizana kama Jikoni kuna ugali na maharage, kwa bahati mbaya wanajibiwa hakuna kitu chochote kilichobakia.

Nilikuwa na njaa kweli, siyo utani. Nikakumbuka pale getini wakati wa makabidhiano na Polisi niliona Fanta Orange kwa Juu ya kabati la askari Magereza,

Nikawauliza kama naweza kupewa ile Fanta Orange nikanywa, basi itanitosha mimi kulala usiku ule. Doh! kumbe soda ya incharge wa zamu gerezani.

Wenzake wakacheka kidogo, Jamaa akanitizama kwa huruma akajua nina njaa kweli, kuona soda juu ya kabati walipoificha siyo Jambo dogo kama huna njaa huwezi kuiona

Kwa huruma ya askari magereza yule, nilipewa ile Fanta, kisha nyapara Mwita akanipokea na akanionyesha sehemu yangu ambayo naweza kulala kuanzia siku ile.

Ndani palikuwa na watu wamelala tayari mistari miwili. Kila mstari mmoja una watu takribani 100 na zaidi jumla kama watu 200 wamelala katika chumba hicho.

Mwisho wa mstari mmoja kuna nafasi ya kigodoro kimoja chenye kumiliki upana wa futi 3 chini, ndipo nikaambiwa naweza kulala pale. Nikajiegesha hapo.

Selo namba 10 (jikoni) ndiyo Jela kweli sasa,waulize wajelajela wa Segerea watakueleza. Kwanza picha linaanza kuna mbu kama millioni tano na ushee.

Watu ni wengi wamelala kwa kugeuziana vichwa, sina shuka wala nini, najiuliza inakuwaje wenzangu wanakoroma kabisa na hali hii ya mbu wengi hivi?

Bahati nzuri nilikuwa na Tshirt ndani, na nje shati la blue. Akili zikanituma shati ndiyo liwe shuka kujifunikia sehemu muhimu tu za usoni na mikononi tu.

Kwa ule uchovu wa mapambano dhidi ya watu zaidi ya 20 pale Sinza Golden folk ile siku ya tarehe 18 September 2024 nilijikuta nimelala fofofo kama wenzangu wala nisikumbuke wingi wa Mbu tena.

Saa 11 alfajiri, Ijumaa ya 20 September 2024 kengele inalia kisha sekunde chache tu mnaamka ghafla kama kuna hatari. Hakuna kuchelewesha muda gerezani.

Kwa haraka sana mahabusu/wafungwa wanakunja magodoro yao kwa haraka kisha unachuchumaa katika mstari mmoja wapo kati ya mistari miwili mirefu.

Mlango wa selo unafunguliwa kisha nyapara kwa sauti Kubwa anataja idadi ya binadamu waliolala na kuamka ndani ya selo yake. Anataja kwa sauti kubwa kabisa.

Halafu kundi kubwa na askari mlangoni linahesabu mtu mmoja mmoja akiwa anatoka kwa speed. Ukipita mlangoni speed unataja namba yako kwa sauti.

Akili zikanikumbusha JKT. Katika pilika kama zile maafande walikuwa wanatandika mkanda wa Mgongo mtu wa Mwisho Kuamka na kujipanga kwenye foleni,

Sikutaka nikaribishwe kwa kutandikwa kwa Jambo lolote sababu unaweza kuchekwa siku zote ukaonekana goigoi au mshamba. Nilikuwa fasta kufuatisha wanachofanya wenyeji wangu.

Kurupuka, amka, kunja godoro, ingia katikati ya mstari haraka ,chuchumaa, nikatoka nje kwa speed ya ngiri pekupeku bila ndala na mwili huu huu unaojua wewe.

Baada ya kumaliza zoezi la kuamka na kuhesabiwa, kigiza ndiyo kinatoweka mwanga unatokeza, Jamaa niliolala nao selo moja wanaanza kunitambua kwa sura na kunishangaa.

Ghafla nasikia shangweeee, “Boniyai,Boniyai,Boniyai” kila mtu anataka kunisalimia. Wengine Rick Ross.Watoto wa Ubungo, Manzese na Mabibo wananiita ‘Mheshimiwa Diwani au Mheshimiwa Meya’.

Machale yakanicheza kidogo,hiki kiringi wanachokianzisha gawa wafungwa Mahabusu kitaisha salama kweli? Hizi kelele za shangwe, askari watazifurahia kweli na Kuniacha salama Kweli? Hebu tuone.

Nikiwa nimezungukwa na utitiri wa Mahabusu na Wafungwa basi nanyanyua shingo yangu juu kutazama askari magereza walipo kama wananiona nakutana uso kwa uso na kundi la askari wananitizama kweli Bwana,

Yule ni nani? Baadhi wanajibu ni Boniyai wa CHADEMA. Nasikia sauti ya ukali, mtoeni huku ujambazini haraka sana, sauti ya mkuu wa zamu wa wiki hiyo.

Dakika siyo nyingi nyapara MWITA akatumwa kuniita niende kwa wale askari, kabla sijawasogelea wakaniamrisha niende ndani ya selo namba 10 nikabebe vitu vyangu haraka sana.

Kwa bahati nzuri niliwajibu wale askari, kilicho changu ndani ni sendozi tu, kwa sababu nilikurupuka peku-peku kuwahi namba baada ya kuamshwa ile alfajiri

Amri ilielekezwa mimi kutolewa ujambazini na kupelekwa Upande maalum wanaishi mahabusu au wafungwa ambao ni watoto, mahabusu, wafungwa wachache

Nilionyesha kuwabishia na kuwakatalia hadi walipo niambia ni kwa usalama wangu

Bado nilionyesha kuwashangaa kwakuwa mimi naona ile shangwe ya wahuni pale ujambazini ndiyo security yangu kubwa,hakuna anayeweza kunigusa ukizingatia wengi ni watoto wa Ubungo, Mabibo,Manzese,Tandale,Kimara,Mbezi, Magomeni,Sinza ,Bunju na Kawe sasa nani angenigusa..?

Lakini baadae waliniambia ukweli kwamba walinihofia ningeweza kuvuruga utulivu wa Gereza na kuanza kuhoji n kupeleleza kujua siri nyingi za kesi za watu kule Ujambazini,kwakuwa Ujambazini ndiyo Jela yenyewe.

Ujambazini selo zipo 10 zikiwa zina Mahabusu na Wafungwa wanaokadiriwa kuwa 600

katika hao 600 mahabusu pekee wapo 500 kule Ujambazini kote na Mahabusu 400 wote wanakabiliwa na mashitaka ya Ujambazi (armed robbery) na cha ajabu zaidi wote mashitakata yao yametokea zehemu moja, kwa "Dulla Ma-robbery" nitaeleza siku nyingine kwa upana hapa.

Basi siku hiyo ya Ijumaa ya tarehe 20 September ndiyo nilitolewa ujambazini na kupelekwa upande maalum ambao wanakoishi watoto chini ya umri wa miaka 18 na mahabusu.

Huko sasa Special Wing tupo jumla ya wafungwa na Mabahusu kama 60 Selo yangu namba mbili palikuwa na Mahabusu 4 na Wafungwa 3 jumla tulikuwa tunaishi watu 7.

Kwanini wanaita Special Wing.?
 
SALAMU KUTOKA UJAMBAZINI (Part 3)

KWAHERI UJAMBAZINI....!

Basi siku hiyo ya Ijumaa ya 20 September 2024 ndiyo siku niliyotolewa ujambazini na kupelekwa upande maalum (special wing) wanakoishi mahabusu ambao ni watoto chini ya umri wa miaka 18 ,mahabusu na Wafungwa wengine.

Huko special wing tupo jumla ya wafungwa na mabahusu kama 67. Kati ya hao, mahabusu watoto ni kama 12 tu. Selo yangu namba mbili palikuwa na mahabusu 4 na wafungwa 3 jumla tulikuwa tunaishi watu 7.

Kwanini wanaita special wing? Ni swali kila mtu anajiuliza ndani ya gereza na nje ya gereza lakini hakuna mwenye majibu kamili. Kwa sababu siku hizi hata Ujambazini kuna TV zenye ving'amuzi vya DSTV na AZAM kila Jengo.

Ujambazini kula chakula cha gerezani (ugali maharage umejitakia tu) sababu watu wa Ujambazini wanaruhusiwa kuweka order ya chakula cha canteen.

Ujambazini maji ya kuoga ni uhakika wakati wote. Ujambazini pia wanaishi mahabusu wazungu na mahabusu wa mataifa mbalimbali kama Nigeria, Ethiopia, na Uganda.

Special Wing na ujambazini tofauti kubwa ya haraka ni idadi ya watu wanaoishi Jela hizo, kwa mfano selo zote 10 za ujambazini wanalala watu idadi ya wanaokadiriwa ni 600 wakati Selo 5 za Special wing zinakadiriwa kuwa na watu 60

Wakati ujambazini kuna selo inabeba watu 200 kwa pamoja, special wing selo kubwa ilikuwa ina watu 17 na inabeba hadi watu 23 tu. Selo ndogo kama niliyokuwa nalala mimi kule special wing inabeba watu 7 hadi 11.

Kuhusu nani anatakiwa kuishi ujambazini na nani anatakiwa kuishi special wing ni swali hakuna mwenye majibu kwa kuwa vigezo vya nani awa wapi havipo wazi sana.

Ujambazini kuna wazungu kama Robert Maitland rafiki yangu yeye ana miaka 14 Ujambazini, Segerea na cha ajabu analalamika yupo Jela miaka 10 bila kifungo wala hakuna kesi inayomkabili wala hajui atatoka lini.

Duh! inatisha eeeh.. kua uyaone ndiyo hii sasa, nitakupa hii stori siku nyingine kwa kirefu zaidi. Ujambazini wameshawahi kuishi watu maarufu na matajiri kwa muda mrefu na maisha yakaenda sawa tu.

Ndiyo sababu baadhi ya huduma kama za TV na ving'amuzi kuwepo ujambazini, ni baada ya mahabusu na wafungwa wakishua kupelekwa kule na kujinunulia mahitaji hayo au kuboresha sehemu zao za kuishi kama vile tiles vyooni na kadhalika.

Basi shangwe. Upendo na heshima kutoka kwa mahabusu wa ujambazini ulifanya niondolewe ujambazini na kupelekwa kwenda kuishi special wing ndani ya selo namba 2.

Washikaji wa Ujambazini wakawa wananifuata bado kuja kunipa hadithi za kesi zao na mambo mablimbali ambayo walikuwa wanahisi ningeweza kuwasaidia

Hata hivyo baadae gereza likaweka ulinzi mkali wa askari zaidi ya watatu katika geti la kuingia special wing ili watu wa ujambazini wasikutane na mimi na mimi nilipigwa mkwara hakuna kutoka nje ya geti la special wing kwenda ujambazini bila ruhusa ya askari Magereza.

Nilikuwa nikitoka special wing kwenda popote lazima niwe chini ya escort ya Askari au nyapara, yote kunizuia kukutana na watu wangu wa ujambazini

SELO NAMBA 2, SPECIAL WING

Kwa historia naambiwa alikuwa anaishi Mzee Rugemarila hata umaridadi wa kuweka wavu wa kuzuia mbu (mosquito net) na maboresho ya tiles choo cha selo namba 2 ni jitihada za Mzee Rugemarila kwa fedha zake binafsi.

Ukienda selo namba nne special wing utaambiwa alikuwa anaishi Habinder Seth na Selo namba tano ni maarufu kama selo ya Freeman Mbowe.

Selo namba mbili ndani tulikuwa na watu saba. Wanne wafungwa (Chi, Lee, Aboubakar na Sam na Watatu ni mahabusu Mimi, Reu na Kimaro, familia hii ya selo namba 2 nimeishi nayo kwa muda mfupi lakini nitaikumbuka daima kwa maisha yale ya furaha, upendo na faraja.

Chi na Lee ni wafungwa tena manyapara lakini ni raia wa china. Lee anaongea kingereza na kiswahili kwa taabu sana, ni mtu mzima anajua mambo mengi sana na kila muda selo tulikuwa tunamskiliza kuhusu stori zake na masomo mbalimbali kuhusu,maisha,biashara na habari za fursa Duniani.huyu ni rafiki ambaye namsubiri kwa hamu nje akimaliza kifungo chake 2027

Wakati Chi ni mchina pia lakini kwa sasa anaongea kiswahili kama mndengereko wa Chumbi au Mzaramo wa Samvu la Chole au Homboza. Kwa mara ya kwanza nilikutana na Chi nilipopelekwa gereza la Keko kwa wiki 3 mwaka 2014 wakati nilkiwa na kesi Kisutu ambayo hata hivyo kesi hiyo ilikuja kufutwa baadae

Mimi na Chi tulikuwa tunaishi wote special wing, Gereza la Keko, wakati huo alikuwa hajui Kiswahili kabisa. Miaka 10 baadae tumekutana tena Gereza la Segerea. Safari hii yeye ndiye alinikumbuka na kuniambia tulikuwa wote Keko.

Chi anasema hakunikumbuka kwa Jina wala sura yangu, anasema amenikumba kwa stori ndani ya gereza. Mtu anayeweza kukusanya kiringi cha wafungwa na mahabusu gerezani akaanza kupiga nao stori kama anafahamiana nao au kuishi nao miaka 20 iliyopita.

Hadi watu ndani ya Jela wanasahau kwenda kula sababu ya stori, akawaza ashawahi kuonana na mtu kama mimi Keko kisha akaniuliza kama ndiye mimi, nikamjibu ndiyo nilikuwa ni mimi na washtakiwa wenzangu Sabula na Mramba lakini mimi ndiyo nilikuwa mtengeneza genge la hadithi na stori maarufu pale special wing ya Keko 2014.

Ndani ya Selo namba 2, special wing sikuwahi kuwa na huzuni, majuto au upweke.Tuliishi kwa amani na furaha sana kama ndugu wa damu.

Ingekuwa inaruhusiwa kisheria kurudi gerezani basi ningeweka ratiba angalau kwa mwaka niende mwezi mmoja au miwili niishi na wale watu wangu wa nguvu. Mungu wetu awatunze sana.
 
SALAMU KUTOKA UJAMBAZINI (PART 4)

Ndani ya selo namba 2,special wing sikuwahi kuwa na huzuni, majuto wala upweke.Tuliishi kwa amani na furaha sana kama ndugu wa damu

Segerea maji ya "NUA" ni dili. Haya maji ya DAWASCO ndiyo wanaita maji ya "NUA". Mtu kukuruhusu utumie maji yake ya akiba kwenye madumu ya njano, ujue amekuheshimu sana.

Lakini mimi nilibahatika siku ya kwanza Jamaa wa selo namba 2 wakanionyesha madumu ya maji mengi sana kama 15 kisha wakaniambia ukihitaji kuoga au kufua maji chukua hapa kwa kuwa huna vyombo kiongozi wetu.

Nyie nyie nyieeeeee si mnakumbuka 19 September nilitoka mahakamani Kisutu usiku na kupelekwa gerezani usiku kwa mara ya kwanza? Mheshimiwa Hakimu akahairisha kesi hadi Jumatatu ya 23 September 2024 ambapo ilikuwa siku ya maandamano

Kule Jela siku hiyo mapema sana tuliambiwa kuwa hatutokwenda Mahakamani kwa sababu ya Maandamano yaliyotangazwa na CHADEMA.Siku hiyo hakuna Mahabusu gerezani alitoka kwenda Mahakama ya aina yeyote ile.

Hapo nje ya Jela siku hiyo Difenda za Manjagu zilikuwa Kibwena na Mamwela shazi mpaka jau,ulinzi na doria ni kama ikulu ya Marekani (white house)

Basi Jamaa zangu wa Segerea walikuwa wanashangilia sana wakisikia siondoki siku hiyo kwenda kupata dhamana Mahakamani.

Watu wa Ujambazini au Special Wing walitaka niendelee Kubakia nipige nao story na kilatu anielezee kuhusu kesi yake na namna ninavyoweza kumsaidia.muda ndiyo tatizo sasa.

Siku zile chache waliona hazitoshi kumaliza foleni yote kumskiliza kila mtu .

Siku ambayo siku pelekwa Mahakamani ndiyo kesi lilihairishwa kutoka 23 September hadi 26 September 2024 ambapo ‘removal order’ ilikuja gerezani nifikishwe Mahakamani Kisutu kusikiliza Uamuzi mdogo kuhusu dhamana yangu.

Binafsi nakumbuka siku hiyo nilifika uwanjani pamoja na Mahabusu wengine,tayari kwa ajili ya upekuzi na kuitika majina kisha mnasubiri majina ya mahakama mnayopelekwa kila mahabusu mmoja.

Niliposikia wanaitwa mahabusu wa kwenda Mahakama ya Kisutu, Kivukoni, Kinondoni, Ilala na mimi nilisogea nikijua ni safari moja na wenzangu.

Askari waliniambia mimi sipo kwenye safari ile bali nitafuatwa na askari maalum wa KM (Kikosi Maalum).Hivyo, sitopanda gari pamoja na wenzangu,baada ya muda wenzangu wote wakiwa wameshapelekwa katika Mahakama zao na mimi nikiwa nimebakia pekee yangu chini ya mti,ghafla niliona kundi la askaribhao wa KM linaingia lango Kuu la gereza.

Jamaa walikuwa Ntu za Mazoezi,wameshiba,warefu alafu wapo serious muda wote.

Kisha nikaitwa Boniyai.. Boniyai.. Boniyai… Twende sasa. Jamaa walionifuata walikuwa serious sana, kila mmoja nikimtizama usoni naona kabisa kuna maneno atakuwa kapewa kwamba mimi ni mtu mbaya sana

Kwanza mikononi nikala pingu yangu, Doh! kwa mara ya kwanza nikajiona nilivyokuwa napendeza na bangili za silver nzito mikononi mwangu ambazo zilikiwa zimekutanisha mikono yangu mbele ya uso wangu kama Jambazi au gaidi

Rohoni nikasema no sweat, yote maisha tu na Wahenga walisema ukiwa ngariba usiogope mkojo.

Siku hiyo Kisutu tulifika mapema sana. Saa 4 nilikuwa pale,kama kawaida yangu,ndani ya Mahabusu ya Mahakama za Kisutu nikiwa naendelea kupiga story na watu (mahabusu) waliokuja Mahakamani Kisutu kutokea Magereza Mengine ya Keko na Ukonga na kuwapa vituko vya Jela zao wakati naishi huko zamani.

Kushtuka ni saa 10 : 00 Jioni na bado sijaitwa Mahakamani kusikiliza uamuzi, machale yakanicheza hapa leo narudi tena Segerea. Nilipokwenda chumba namba moja cha Mahakama ya Kisutu baada ya mpambano wa hoja na vifungu vya kisheria, nilitakiwa kurudi tena Segerea kusubiri uamuzi kusomwa tena siku ya 01 October 2024.

Wakati mzuri sana Selo namba 2, Special Wing..! (GOOD MOMENT)

Ni hiyo siku ya 26 September 2024, akili yangu yote ilijua siku hiyo nitapewa dhamana kwa uamuzi wa Mahakama, Kisutu kwa hiyo asubuhi sikunywa uji wala sikubeba "paseli" kama wengine wanavyobeba chapati, bagia au maandazi kuja kula katika chumba cha mahabusu ya Mahakama pale Kisutu, Si unajua Watuhumiwa tukitoka gerezani haturuhusiwi kununua chakula cha kutoka nje pale Kisutu

Basi nishapangiwa zangu tarehe 01 October ndiyo ning'ae tena mbele ya Hakimu mfawidhi Mahakama ya Kisutu. Narudishwa zangu na Kikosi Maalum (KM) kama kawa ,kikosi kutoka Keko kinachokuja kunichukua Segerea na Basi langu moja likiwa na watu kama 20 hivi wote wapo serious na kazi na Mijegejo ya maana mkononi.

Si mlikuwa mnawaona nyie wenyewe?
Wengine wanapanda juu ya Jengo la Mahakama ya Kisutu. Wengine wamevaa soksi usoni, wamepiga groves mikononi na bunduki nzito mikononi ,basi miye taratibu njiani narudishwa zangu ktk makazi ya muda Segerea.

Siku hiyo ya 26 September 2024 nilirudishwa zangu gerezani muda ukiwa umeenda sana. Ni saa 2 usiku ndiyo tunatoka Mahakama ya Kisutu na tumboni sijaweka kitu tangu asubuhi

Basi kwa ujinga wangu wakufikiri ningeruhusiwa kwa dhamana siku hiyo sikula kitu, sasa ngoma imedunda na nina njaa kama Mama aliyetoka Kujifungua leba.

Jamaa wale wa Kikosi Maalum (KM) wamenifikisha salama. Wamenifungua pingu zao. Wamenikabidhi Ngome kisha wao wakasepa zao.Sasa Askari wa Segerea wananipeleka selo namba 2. Muda unaenda saa 3 usiku, siku hiyo.

Nakumbuka siku hiyo walikuwa wanamsisitiza Dereva awahi kuwarudisha Keko wawahi mechi ya Simba SC na Azam FC ambayo ilkuwa inachezwa Zanzibar

Pale selo namba 2 Jamaa zangu akina Chi, Lee, Sam ,Aboubakar, Kimaro na Njau ile naingia mlangoni kitu cha kwanza naona kila mmoja anakoroma. Duh! pozi lote hata la Kuulizia mkate na soda likaniisha.

Nikaingia kuoga chap na njaa yangu.Narudi kwenye kigodoro changu najisema wameshalala hawa wanakoroma, siyo vizuri kuwasumbua watu kwa kuwaamsha na huwaharibia usingizi wao.

Ukizingatia najua thamani ya Usingizi wa gerezani. Unaweza kuamshwa usiupate tena hadi asubuhi, kwa kujikuta unawaza familia yako au biashara zako nje zinaendaje.

Basi kinyonge sana, nikiwa na njaa kali sana, nikajilaza na kujifunika shuka langu. Kumbe washenzi
wale hawakuwa wamelala kweli aiseee.

Walinisikia tangu geti kubwa linafunguliwa na nikiwa naulizwa kwa sauti na Askari, Je nalala selo namba ngapi ..? na yule askari wa kutunza funguo.

Ghafla Jamaa zangu wakaamka kwa lelele wakisema kwa pamoja “Welcome Boniyaiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii”

Kumbe walikuwa wanaigiza wamelala tu wahuni wale,lakini kwa sura zao na lile shangwe lao niliona kabisa Jamaa zangu walivyofurahi Mimi kunyimwa dhamana yangu ili kuendelea kuishi nao pale gerezani.

Daaaaaaaaah wananikubali na kunipenda sawa,Sasa ndiyo watake niendeleee kuwa gerezani?

Surprise kubwa kwangu ,kumbe Jamaa walibakisha chakula aiseeee,nasikia Aboubakar aliwaambia wenzie kuwa anahisi siachiwi kwa dhamana siku ile,
Jamaa wakaniwekea chakula aiseeee,chapati na kuku makange na Pepsi ya Take away. Upendo uliwoje..?

Jamaa wanafuraha kuniona kama vile nimeishi nao miaka 10, kumbe wiki kadhaa tu ndani ya Jela.

Mwingine ananifungulia soda na mwingine anatoa chapati, huku mwingine kaenda kunichukulia maji ya kunawa kwenye jagi na ndoo ya kunawia.

Kwa njaa yangu,nakula chapati na makange rosti huku nawasilimulia kilichotokea Mahakamani. Chi ananichekesha anasema, kuna watu walitaka kuchukua godoro langu mchana wakijua sirudi, yeye akawakataza kwa sababu alijua nitarudi tu.

Ukiwa selo namba 2,special wing huwezi kumuwaza anayekukomoa asikupe dhamana wala aliyekuleta gerezani , yani ni utani, furaha,vicheko na upendo tu.

Sasa mimi niliposhiba fadhila zangu ilikuwa nikuwaburudisha na utani wangu kama walionizoea nao,wasione nimerudi kinyonge. Kwanza nikasimama kisha nikapandisha bukta yangu juu (mayenu)

Si nikaanza kuporomosha show kwa kuimba wimbo wa DDC Mlimani Park Orchestra "nawashukuru wazazi wangu"

"Nawashukuru wazazi wangu wakati wowote
Ushauri wao umeniletea mafanikio mema
Sasa naishi na watu vizuri, eh
Sasa naishi na watu vizuri, eh-eh

Huku niliko wazazi wangu sina ndugu
Lakini kutokana na husia wenu wazazi wangu
Najiona kama niko nyumbani, eh
Najiona kama niko nyumbani, eh, mama

Nawashukuru wazazi wangu wakati wowote
Ushauri wao umeniletea mafanikio mema
Sasa naishi na watu vizuri, eh
Sasa naishi na watu vizuri, eh-eh

Huku niliko wazazi wangu sina ndugu
Lakini kutokana na husia wenu wazazi wangu
Najiona kama niko nyumbani, eh
Najiona kama niko nyumbani, eh, mama.."

Basi waswahili wenzagu wanaujua na wao wakajikuta tunaimba wote kwa furaha na kelele wimbo huo huku pembeni wale Wachina wanapiga ndoo na Bakuli kama "Drums", bila kujali muda wa kulala saa 3 : 00 Usiku ulikuwa umeshafika.

Unafanya mchezo nini? Uishi na watu mpaka wakumbuke jamaa kaondoka bila chakula, anaweza kurudi na njaa wakununulie chakula tena bila ya kuwa na mawasiliano nao kuwa utarudishwa tena.

Kwanini usijikute unawakumbuka wazazi wako kwa malezi mazuri ya kukufunza kuishi na watu vizuri na ukajikuta unaishi popote na mtu yeyote kama upo nyumbani ingali upo mbali ..?

Itaendeleaaaaa...!
 
Back
Top Bottom