Blasio Kachuchu
JF-Expert Member
- Sep 7, 2016
- 326
- 223
Rufiji. Tarehe 29 Mei 2024: Kutokana na mafuriko yaliyotokea katika msimu wa masika mwaka huu, Benki ya CRDB imekabidhi msaada wa mbegu za mahindi zenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Benki ya CRDB imekabidhi kilo 7,148.857 za mbegu za kisasa za mahindi zitakazosambazwa kwa wananchi ili wazitumie katika msimu ujao wa kilimo kuhakikisha wanakuwa na chakula cha uhakika.
Akikabidhi msaada huo uliopokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Mheshimiwa Meja Edward Gowele, Bi. Tully Esther Mwambapa ambae ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation amesema taarifa za athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokea zimewasikitisha watu wengi ndio maana imekuwa rahisi kwao kutoa msaada huo utakaosaidia kurudisha shughuli za kilimo kwa uhakika.
“Majanga yana athari kubwa zinazorudisha nyuma uchumi wa watu na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Mara zote, hutokea na kutukuta tukiwa hatujajipanga kukabiliana nayo au hatuna uwezo wa kuyazuia yasitokee.
Hii ndio sababu iliyoishawishi Benki yetu ya CRDB pamoja na kampuni zake tanzu kushirikiana bega kwa bega na Serikali kukabiliana na majanga pindi tu yanapotokea ili kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika,” amesema Tully.
Tully amesema walipopata maombi ya uhitaji wa mbegu hizo kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko, hawakufikiria mara mbili kwani waliona ni jambo jema litakalowasaidia waathirika kupunguza athari walizopitia na kurejesha hali zao kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele ameishukuru Benki ya CRDB akisema kitendo ilichokifanya cha kuwakumbuka na kuwakimbilia waathirika wa mafuriko yaliyotokea ni cha kizalendo na kinachopaswa kuigwa na wengine.
“Moyo wangu na kichwa changu kama ilivyo kwa wana Rufiji wengi leo, vimejaa shukrani nyingi. Tunawashukuru sana Benki ya CRDB kwa kutukimbilia kipindi hiki kigumu. Msaada huu wa mbegu za mahindi mnaotukabidhi leo umekuja kwa wakati muafaka kwani utatusaidia kujikwamua kutoka katika athari za mafuriko kwa kupunguza gharama za kilimo hivyo kutuhakikishia mavuno msimu ujao,” amesema Meja Gowele.
Mkuu huyo wa wilaya amesema mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu zimesababisha mafuriko ambayo yameharibu mazao yaliyopandwa shambani na hata baadhi ya biashara hivyo kuwarudisha wananchi wengi kwenye lindi la umasikini.
Kwa msaada uliokabidhiwa, Meja Gowele amewahimiza wananchi wa Rufiji kutumia huduma za Benki ya CRDB kurudisha shughuli zao za uchumi kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa janga hilo la asili na kujijenga zaidi kimapato.
“Hakuna namna nzuri ya kuiunga mkono Benki ya CRDB zaidi ya kutumia huduma zake,” amesisitiza Meja
Sambamba na msaada huo, Taasisi ya CRDB Bank Foundation imetoa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kwa wanawake na vijana wilayani humo ili kuwaandaa kwa ajili ya kunufaika na mtaji wezeshi utakaosaidia kuinua uchumi wao.
Tully amesema mafunzo hayo yanaratibiwa na Programu ya Imbeju ambayo mpaka sasa imeshawajengea uwezo zaidi ya wajasiriamali 350,000 pamoja na kuwapa mtaji wezeshi wa jumla ya shilingi bilioni 10 nchini kote.
“Kupitia programu hii ya IMBEJU leo hii tutakwenda kutoa mafunzo kwa wanawake na vijana juu ya namna gani programu hii inaweza kuwasaidia kukuza biashara zao na shughuli zao za kiuchumi ikiwamo biashara na kilimo.
Wataalamu wetu kutoka CRDB Bank Foundation watatoa mafunzo ya ujasiriamali na kuainisha fursa zinazoambatana na programu hii ikiwemo ile ya matumizi ya nishati safi kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya chakula maarufu kama mama lishe,” amebainisha Tully.
Kuhusu mafunzo kwa wajasiriamali hao, Meja Gowele amesema anaamini maarifa watakayoyapata yatakuwa na manufaa makubwa kwa washiriki, familia zao na jamii nzima kwa ujumla wake.
Gowele.
“Naomba nichukue fursa hii kuwaeleza kuhusu fursa iliyo mbele yenu ya kunufaika na Programu ya Imbeju ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali vijana na wanawake. Rufiji ina kila kitu kinachohitajika kwa mjasiriamali kujikwamua kiuchumi na Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation inatoa mafunzo na mitaji wezeshi ili kuwakomboa wananchi
Niwaombe, tuzitumie fursa hizi tutakazoelezwa leo hii kuwa umakini ili wenye sifa wapate mitaji hii na wale ambao bado hawajatimiza vigezo, wahakikishe wanavikamilisha ili kwa pamoja tuujenge upya uchumi wa wilaya yetu,” amesema Mkuu wa Wilaya Gowele.