JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,868
- 6,807
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dk Yamungu Kayandabila alisema hayo alipowasilisha matokeo ya kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika Aprili 3, 2025.
Alisema pia uthibitisho umetolewa na maoni ya wakurugenzi wa kampuni pamoja na tathmini ya Taasisi ya Moody’s iliyobakiza Tanzania kwenye daraja la B1 lenye mwelekeo imara.
Chanzo: Habari Leo
=====================================
TAARIFA YA KAMATI YA SERA YA FEDHA
Kamati ya Sera ya fedha ilikutana tarehe 3 Aprili 2025, na kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi, na mwelekeo wake katika robo ya pili ya mwaka 2025. Kulingana na tathmini hiyo, Kamati imeamua Riba ya Benki Kuu kuendelea kuwa asilimia 6. Kwa muktadha huu, Benki Kuu itaendelea kutekeleza Sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 4-8. Mfumuko wa bei na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini, unatarajiwa kubaki ndani ya malengo. Hata hivyo, kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani inaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika kufikia malengo yake. Hivyo basi, uamuzi huu wa Kamati unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani.
Katika kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025, Kamati ilibaini kuwa shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi ziliendelea kuimarika, na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025. Mfumuko wa bei ulipungua na kufikia malengo ya benki kuu za nchi nyingi duniani, kutokana na kufifia kwa athari zilizotokana na mitikisiko ya kiuchumi katika vipindi vilivyopita, na utekelezaji wa sera ya fedha iliyolenga kupunguza ongezeko la ukwasi. Kutokana na mwenendo huu, pamoja na matarajio ya kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei, benki kuu katika nchi nyingi zimeendelea kupunguza riba zao za Sera ya fedha. Hata hivyo, kutokutabirika kwa sera, vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hususan zile zilizoendelea na zinazoibukia kiuchumi, pamoja na migogoro ya kisiasa vinaweza kuathiri matarajio ya ukuaji wa uchumi na kuchochea kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani.
Tanzania ilibakizwa katika daraja B1 ikiwa na mwelekeo imara. Hata hivyo, matarajio haya yanaweza kuathiriwa na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani. Kwa muhtasari, mwenendo wa uchumi pamoja na matarajio yake ni kama ifuatavyo:
- Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, hali ya ukwasi illimarika, kutokana na ongezeko la matumizi ya Serikali pamoja na kupungua kwa fedha taslimu nje ya mfumo wa benki. Kutokana na mwenendo huu, benki zilipunguza mahitaji ya mikopo kutoka Benki Kuu. Hata hivyo, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya benki ndogo zimeendelea kukumbana na changamoto ya kupata ukwasi kwa gharama nafuu na hivyo kuchangia riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki kubaki karibu ya wigo wa juu wa riba ya Benki Kuu (CBR).
- Kwa mwaka 2024, uchumi wa Tanzania ulikuwa imara, ukichangiwa na ongezeko la uwekezaji katika sekta za umma na binafsi. Ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara unakadiriwa kufikia asilimia 5.5 mwaka 2024, ukilinganishwa na matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.4, na ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023. Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na sekta ya kilimo, fedha na bima, uchimbaji wa madini, na ujenzi. Vilevile, utalii ambao hugusa shughuli nyingi za kiuchumi ulichangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi. Ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.5, katika robo ya kwanza ya mwaka 2025. Uchumi wa Zanzibar ulikua kwa asilimia 7.2 katika robo ya nne ya mwaka 2024, kutoka asilimia 2.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, ukichangiwa zaidi na shughuli za malazi na chakula, ambazo kwa kiwango kikubwa huambatana na shughuli za utalii, pamoja na biashara. Ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha katika robo ya pili ya mwaka 2025, ukifikia asilimia 6.1, Tanzania Bara na asilimia 6.5 kwa Zanzibar.
- Mfumuko wa bei ulikuwa tulivu sambamba na matarajio, kutokana na utekelezaji thabiti wa sera ya fedha na bajeti, uwepo wa chakula cha kutosha nchini pamoja na kupungua kwa bei za nishati duniani. Mfumuko wa bei ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.1 mwaka 2024, ukilinganishwa na wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023, chini ya lengo la nchi la chini ya asilimia 5, na ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa nchi za SADC na EAC. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 5.1 mwaka 2024, kutoka asilimia 6.9 mwaka 2023. Aidha, mfumuko wa bei
- Ujazi wa fedha ulikua imara, kwa zaidi ya asilimia 12 mwaka 2024, sanjari na utelekezaji wa sera ya fedha. Ukuaji wa ujazi wa fedha ulichangiwa zaidi na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukuaji wa ujazi wa fedha uliongezeka
sambamba na kuimarika kwa ukwasi. Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 12.7, ambapo sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi hususan biashara ndogo na za kati, ikifuatiwa na shughuli za kilimo, biashara na uzalishaji viwandani.
- Sekta ya fedha imeendelea kuwa imara na thabiti, ikiwa na ukwasi wa kutosha, yenye kutengeneza faida, na mtaji wa kutosha kukabiliana na mitikisiko ya kiuchumi. Ubora wa rasilimali za mabenki uliendelea kuwa wa imara, ambapo uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ulikuwa asilimia 3.6 mwezi Februari 2025, chini ya kiwango kinachokubalika cha chini ya asilimia 5.
- Utekelezaji wa sera ya bajeti katika robo ya tatu ya mwaka 2024/25, ulikuwa wa kuridhisha. Mapato ya kodi kwa Tanzania Bara na Zanzibar yalifikia lengo kama ilivyokuwa katika robo mbili zilizotangulia, kutokana na kuimarika kwa ufanisi na usimamizi wa kodi. Matumizi ya Serikali yaliendelea kufanyika kuendana na rasilimali zilizopo. Deni la Serikali limeendelea kuwa himilivu, hali inayoakisi usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya Serikali.
- Sekta ya nje imeendelea kuimarika. Katika mwaka unaoishia Machi 2025, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilikuwa takriban asilimia 2.6 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia
- Akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2025. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni 5.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takribani miezi 4.5, na inatarajiwa kubaki katika viwango hivi kwa robo ya pili ya mwaka 2025. Kulingana na kuimarika kwa urari wa malipo ya kawaida, Kamati ilibaini kuwa mabadiliko ya thamani ya shilingi katika robo ya kwanza ya 2025 ni ya msimu, na hivyo Shilingi inatarajiwa kuimarika sambamba na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini.
Kwa kumalizia, Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia Benki Kuu kuendelea kufanya maboresho katika soko la fedha baina ya benki kwa lengo la kuongeza ufanisi wa uamuzi wa viwango vya riba zinazotozwa katika soko hili; na kuendelea kufuatilia kwa karibu vihatarishi vinavyoweza kuathiri mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi ili kuchukua hatua stahiki za sera ya fedha pale inapohitajika. Maelezo ya kina ya mwenendo wa uchumi na mwelekeo wake, yatapatikana katika Ripoti ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC Report) itakayochapishwa hivi karibuni kwenye tovuti ya Benki Kuu https://www.bot.go.tz/Publications/Filter/49. Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia
kukutana tena katika wiki ya kwanza ya mwezi Julai 2025 na kuamua kiwango cha riba cha Benki Kuu kwa robo ya tatu ya mwaka 2025.
EMMANUEL M. TUTUBA GAVANA