BBC SWAHILI: Kwanini CCM imeweza kusalia Madarakani kwa miaka yote?

magnifico

JF-Expert Member
Jan 14, 2013
11,449
25,633
Katika mojawapo ya mahojiano aliyowahi kufanya miaka ya nyuma, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipata kuulizwa anadhani nini hasa ilikuwa siri ya Baba wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere, kudumu muda mrefu madarakani.

Bila kupepesa macho, Rais huyo alitoa jibu moja tu; He tamed the army (aliweza kulidhibiti jeshi). Hilo ndilo jibu lililokuja haraka kichwani kwake na pasi na shaka yoyote, atakuwa amejifunza mengi kiasi kwamba sasa yeye ndiye Rais aliyekaa madarakani kuliko mwingine yeyote miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki -akimzidi hata Mwalimu Nyerere aliyekaa miaka 24

Nyerere alikuwa Rais wa Tanzania lakini hakuwa akiongoza kupitia mapinduzi ya kijeshi. Aliongoza kwanza kupitia chama cha TANU kilichopigania Uhuru wa Tanganyika na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoundwa kufuatia kuungana kwa TANU na Afro Shiraz (ASP) cha Zanzibar mwaka 1977. Kuunganishwa kwa vyama hivi kulitokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 na nia ya kuwa na chama kimoja kinachotawala kupitia mfumo huo

Endapo chama cha CCM kitashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kitakuwa kimekaa madarakani kwa takribani miaka 60; na kuwa chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu kuliko kingine chochote miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

CCM ni miongoni mwa vyama vichache vya ukombozi ambavyo bado vimesalia madarakani takribani miaka 50 baada ya nchi nyingi za Afrika kuwa huru.

Vyama vya aina yake ambavyo bado vimesalia madarakani ni kama FRELIMO cha Msumbiji, SWAPO cha Namibia, MPLA cha Angola, ANC cha Afrika Kusini. Miongoni mwa hivyo, hakuna ambacho kimekaa madarakani kuizidi CCM.

Washirika wa CCM katika harakati za ukombozi; vyama kama vile UNIP cha Zambia, UPC cha Uganda, KANU cha Kenya na vingine vya Afrika Magharibi na Kaskazini ama vimeondolewa madarakani na kugeuka kuwa vyama vya upinzani vilivyodhoofu au kuondoka kabisa katika ramani za kisiasa.

Nini hasa kimeifanya CCM kudumu muda wote huo wakati wengine wakipotea katika ramani?


Uongozi wa Julius Nyerere
Kete ya kwanza ya CCM ni aliyekuwa kiongozi wake kwa takribani miongo mitatu ya kwanza, hayati Mwalimu Nyerere. Rais huyu wa kwanza wa Tanzania alifanya mambo ambayo hatimaye yamesababisha CCM iendelee kubaki madarakani. Yeye ndiye mpishi wa mambo mengine ambayo yamekifanya chama hicho kiwe hapo kilipo sasa.

Wakati rafiki zake, Milton Obote wa Uganda na Kwame Nkrumah wa Ghana wakiondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi, Nyerere alinusurika na tukio la Maasi ya Jeshi ya mwaka 1964. Alichofanya Nyerere ni kulivunja jeshi lililokuwapo ambalo alilirithi kutoka kwa wakoloni na kutengeneza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Jeshi hilo lilitengenezwa na kufumwa katika itikadi ya ukombozi, ujamaa na lisilo na ukabila, udini huku askari wakipandishwa vyeo kutokana na umahiri wao na si kwa vigezo vingine. Matokeo yake, jeshi hilo la kizalendo halikumsumbua tena kama ambavyo wenzake wengi barani Afrika.

Ni Nyerere ndiye aliyepandisha hadhi lugha ya Kiswahili ambayo iliwaunganisha Watanzania na kuwa lugha ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, CCM kikaweza kuwa chama kilichoweza kufika nchi nzima kwa viongozi wake kuzungumza lugha moja inayoeleweka kwa wananchi. Ziko nchi ambazo hata mawasiliano ya vitu vidogo ni ya taabu kwa sababu watu ndani ya serikali, majeshi na kwenye vyama hawazungumzi lugha moja na wakaelewana.

Nyerere hakuwa malaika lakini mtindo wake wa uongozi ulimfanya aheshimiwe na wengi wa Watanzania. Baba huyu wa Taifa hakuwa fisadi, alikuwa mzungumzaji mzuri kwenye majukwaa na kupitia maandishi yake na hakuonekana kuwa na upendeleo wa wazi wazi kwa watu wa dini, kabila au eneo alilotoka.

Nyerere pia ndiye aliyesimika mfumo wa utawala wa Tanzania ambapo Rais anakuwa ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Haya ni mamlaka makubwa sana kupewa mtu mmoja. Mfumo huu unampa Rais - kiongozi wa chama tawala; CCM tangu Uhuru, madaraka makubwa ya uteuzi wa viongozi wa vyombo vya serikali na dola na chama hicho kimekuwa kikitumia faida hiyo ipasavyo nyakati za uchaguzi.

Kubadilisha marais
Ukiondoa Nyerere, hakuna Rais mwingine wa Tanzania ambaye ametawala kwa zaidi ya miaka kumi. CCM imekuwa na utaratibu wa kuheshimu Katiba ambapo Rais aliye madarakani atatawala kwa miaka kumi tu na kumwachia mwingine.

Katibu Mtendaji wa kwanza wa CCM wakati ilipoanzishwa, Pius Msekwa, alipata kuniambia kwamba viongozi wanaokaa madarakani muda mrefu matokeo yake huchokwa na wananchi wao hata kama hakuna jambo baya walilofanya.

Kwa kuhakikisha wateule wake wanakaa madarakani miaka kumi tu, CCM imehakikisha Watanzania wamekuwa hawachoki kwa kuona sura moja tu kwa miaka zaidi ya kumi. Mara nyingi, mgombea anayechukua nafasi ya aliyetangulia anakuwa na sifa na haiba tofauti na mtangulizi wake.

Nyerere alikuwa mwanafalsafa, mhafidhina na mcheshi, mbadala wake Ali Hassan Mwinyi akawa mtu rahimu, muungwana na mpenda mabadiliko, Mkapa akawa makini na mshaufu huku Jakaya Kikwete akiwa tena mcheshi, mtu wa watu na muungwana wa pwani. Baada ya miaka yake kumi, John Magufuli amechukua nafasi yake naye ni tofauti na mtangulizi wake kwa haiba na utendaji kazi.

Mgawanyo wa Keki ya Taifa
Namna pekee ya kuelewa hili ni kuangalia nchi jirani ya Kenya.

Wakati nayo ikielekea kutimiza miaka 60 ya Uhuru wake mwaka 2023, imefanikiwa kuwa na marais wanne; Jomo Kenyatta, Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Hiyo maana yake ni kuwa Wakikuyu wametoa marais watatu miongoni mwa marais wanne waliowahi kutawala nchi hiyo.

Ni Moi pekee ambaye hakuwa Mkikuyu -akitoka katika kabila la Wakalenjini.

Jambo hili limekuwa likizua hali ya sintofahamu na kuhisi kutengwa kwenye mgawo wa keki ya taifa miongoni mwa makabila mengine makubwa nchini humo kama vile Wajaluo, Waluhya, Wakalenjini na watu wa makabila ya pwani ya Kenya.

Hali ni tofauti kwa Tanzania. Nyerere alikuwa Mzanaki kutoka Kaskazini mwa Tanzania, Mwinyi anatoka Zanzibar, Mkapa anatoka Kusini, Kikwete akatoka Pwani na Magufuli anatoka Kanda ya Ziwa.

Marais wote wa Tanzania wametoka katika makabila tofauti miongoni mwa zaidi ya 120 yaliyopo.

Hii maana yake ni kuwa hakuna upande au kabila la Tanzania linaloweza kusema limeongoza kwa kutoa marais wengi. Kitendo cha kuwa na Rais madarakani humaanisha kwamba watu wa eneo analotoka Rais huweza kufaidika kwa namna moja au nyingine na uwepo wa kiongozi miongoni mwao. Inaweza isiwe waziwazi lakini pasi na shaka, kuna kipande cha keki ya taifa kitamegwa kwa kuzingatia ukweli wa Rais kutoka katika eneo fulani.

Uchaguzi mwingine unapofika, kuna wana CCM wataunga mkono mgombea kwa sababu anatoka katika eneo analotoka na hivyo kwamba hata kama haitakuwa kwa kiasi kikubwa; walau wanaweza kujikuta kuambulia kipande kutoka katika Keki ya Taifa.

Unaweza kusoma
Mambo matano unayopaswa kuyafahamu kuhusu uchaguzi wa Tanzania
Mwingiliano wa Dola na CCM
Ingawa kisheria Tanzania inaongozwa kupitia mfumo wa vyama vingi, mstari mwembamba sana unatenganisha CCM na watendaji wa serikali na vyombo vya dola. Hata vyombo ambavyo kwa kawaida vingetakiwa kutoa haki kwenye washindani wa kisiasa, vinaonekana kuwa na uhusiano na CCM.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, alijitokeza kutaka kuwania Urais kupitia CCM.

Mwaka huu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alitangaza nia ya kutaka apitishwe na CCM kuwania urais wa Tanzania.

Nchini Tanzania, watumishi kama wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanatakiwa kuwa watumishi wa umma lakini vyeo vyao hivyo vya kiserikali vinawapa fursa ya kuingia kwenye vikao vya CCM kwa mujibu wa nyadhifa zao.

Inapofika nyakati za uchaguzi, ofisi hizi za umma kimsingi hubadilika na kugeuka za CCM kwa maana ya matumizi ya rasilimali watu na nyingine.

Katika nchi ambazo kuna mgawanyo wa madaraka na vyombo vya utoaji haki vinavyojitegemea, si rahisi kusikia Jaji Mkuu mstaafu akijiingiza kwenye uchaguzi kuomba kupitishwa na chama awe mgombea wake urais.

Kwa hiyo, CCM imekuwa ikifaidikika na mfumo huu wa kufanya siasa na uchaguzi ulioizunguka.

Tanzania itafanya uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu

Suala la Katiba
Katiba ya Tanzania ilitengenezwa mwaka 1977; nyakati zilezile wakati CCM ikiundwa. Katiba hii ndiyo inampa Rais mamlaka na madaraka aliyonayo ikiwamo kuteua viongozi wa taasisi zinazosimamia uchaguzi.

Wakati wa utawala wa Rais Kikwete, Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba , ilikusanya maoni ya Watanzania wote kuhusu Katiba mpya na ilipendekeza mambo ya kubadili kwenye Katiba ili kuongeza uwajibikaji na kupunguza madaraka ya Rais yaliyomo katika Katiba ya sasa.

Hata hivyo, mapendekezo hayo yalipingwa na wabunge wa Bunge la Katiba waliokuwa upande wa chama tawala kwa vile ilionekana kama inataka kupunguza madaraka na mamlaka ya Rais. Matokeo yake ni kwamba Watanzania wamebaki na Katiba ileile ya mwaka 1977 iliyotungwa wakati chama kikiwa kimeshika hatamu.

Afrika Kusini, Kenya, Malawi na Zambia wamefanya mabadiliko ya Katiba zao wakati wakienda kwenye chaguzi zao na matokeo yake yakawa mazuri kwa wapinzani. CCM, pamoja na mambo mengine, inaendelea kubaki madarakani kwa sababu Katiba iliyopo ilitungwa kwa lengo la kuisimika ibaki madarakani milele.

Ndiyo sababu, kuna wanaoamini kwamba kama vyama vya upinzani vina lengo kweli la kuing'oa CCM madarakani, sehemu ya kwanza wanayotakiwa kuipigania ni kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya Katiba ya Tanzania inayotumika sasa.
 
Itafika wakati vyama mbali mbali duniani vitakuja Tanzania lengo likiwa kusoma city adimu kama consistency, deliverance, sustainance, diversity etc toka Kwa CCM. LONG LIVE CHAMA CHA MAPINDUZI!!
 
Back
Top Bottom