Barua ya Wazi kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzaia, Dkt. Samia Suluhu Hassan

winnerian

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
371
565
Barua kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Septemba 4, 2024


Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan,
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dodoma,
Tanzania.

Yah:
Pendekezo la Kuunda Timu ya Wataalamu kwa Ajili ya Utafiti na Uchunguzi wa Kuboresha Mifumo ya Maendeleo ya Taifa

Mheshimiwa Rais,

Kwa heshima na taadhima, naomba kutumia fursa hii adhimu kuwasilisha kwako wazo pamoja na utayari wangu, sambamba na wananchi wengine watakaoshiriki, kuunda timu ya wataalamu itakayojikita katika kufanya utafiti wa kina, uchambuzi, uchakataji wa mfumo wa upatikanaji wa maendeleo kwa haraka na hatimaye kuandaa mpango kazi weyenye mapendekezo ya mfumo bora wa kuboresha nyanja mbalimbali muhimu katika taifa letu la Tanzania.

Tunaamini kwamba mfumo madhubuti wa utafiti na uchunguzi unaweza kusaidia sana kubaini mbinu bora za kuboresha sekta za uongozi, afya, elimu, kilimo, biashara, viwanda, na maadili ya jamii kwa ujumla. Hii itachochea maendeleo na kuinua hali ya maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Kwa mfano, nyanja muhimu inayoweza kufanikisha maendeleo au kuleta umaskini katika taifa letu ni namna tunavyowapata viongozi wetu, wakiwemo wa kisiasa na wale wa sekta nyingine. Viongozi ndiyo wanaoliongoza taifa kufanikisha maendeleo au kuzorota kwake. Tukifanikiwa kuunda mfumo thabiti na madhubuti wa kuwachagua na kuwaajiri viongozi wetu, tutakuwa tumeweka msingi imara kwa maendeleo ya sekta nyingine. Viongozi wanashikilia mamlaka juu ya rasilimali za taifa na watu wake, hivyo, taifa likiwa na viongozi wengi wasio na dira au ndoto ya kweli, inapelekea kudumaa kwa maendeleo ya taifa, hata kama kutakuwa na ukuaji, basi utakua kwa kasi ndogo sana.

Timu hii itafanya utafiti na kubaini namna bora ya kuwachagua na kuwaajiri viongozi wa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na viongozi wa kisiasa (wachaguliwa na wateule) na wale wenye nafasi za kushindana kwa taaluma na elimu zao. Itasaidia sana kupata watu sahihi katika nafasi muhimu, ambao watafanya kazi kwa weledi na uzalendo, bila kutilia mkazo maslahi binafsi.

Viongozi wanapatikana kwa njia bora watakuwa na sifa bora pamoja na kujiamini katika kutimiza majukumu yao ya kitafia kwa maslahi ya wananchi wanaowaongoza na kuwatumikia. Wao ndio watakuwa wasimamizi wa mamlaka zetu ambazo ni pamoja na rasilimali za taifa. Watasidia kusimamia fedha zetu tunazozipata kwa njia ya kodi, mikopo na fadhila kutoka mataifa mbalimbali. Hii itasaidia sana kuharakisha maendeleo yetu kwani bila kuwa na viongozi wazelendo hali ya taifa letu itabaki ukiwa na bila kuwa na dira bora ya kule tunakoelekea kama taifa.

Aidha, timu hii itakuwa na jukumu kubwa la kuunda mfumo mpya wa utawala bora kwa kupima namna ya kutawanya mamlaka ya serikali kuu hadi mikoani ili kuwezesha ukuaji wa haraka wa maendeleo (mfumo wa utawala uliogawanywa, yaani Decentralized Governance System). Hali ilivyo sasa, serikali kuu na serikali za mitaa bado hazijafanikisha kikamilifu upatikanaji wa maendeleo kwa haraka. Kwa miaka mingi, maendeleo yetu yamekuwa ya taratibu, hadi kufikia hatua ya kuvaa mitumba kutoka nje, tukiona fahari kwa hilo, huku nchi ambazo hapo awali tulikuwa sawa kiuchumi, zikiwa zimepiga hatua kubwa.

Kuboresha mfumo wa utawala bora (Governance System Updating) kutatuwezesha kubaini mbinu bora za kuliacha taifa lenye nguvu na salama kwa vizazi vijavyo.

Pia, timu hii itachakata mfumo wa upatikanaji wa haki katika taifa letu. Faida za kuwa na mfumo bora wa haki katika taifa ni nyingi. Mfumo wa mahakama bora, wenye nguvu na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yake, utawezesha usimamizi wa sheria tulizojiwekea na upatikanaji wa haki kwa kila mmoja wetu bila kujali hadhi ya maisha ya mtu. Faida za kuwa na mahakama zenye nguvu na huru ni pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kujenga imani kwa serikali, kuzuia ufisadi, kukuza haki za binadamu, na kuimarisha uwajibikaji. Haya ni mambo ambayo tunayaona na kuyashuhudia kama sinema kwenye nchi zilizoendelea lakini kwetu tumekuwa nayo kama vile midoli ya kuchezea, tukiamu kuifanyia kazi na kuiweka ikawa bora hata sisi tutapata utamu ule ule ambao wenzetu walioendelea wanaupata.

Vilevile, mfumo bora wa kikodi utachunguzwa kwa kina na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na wataalamu wa kimataifa kutoka mataifa ambayo ukusanyaji wa kodi umeonyesha mafanikio makubwa. Lengo ni kuunda mfumo bora wa kikodi ambao utasaidia sana kuongeza makusanyo na hatimaye tuweze kujitegemea kwa kiasi kikubwa bila kutegemea mikopo kutoka nje ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa mzigo wa taifa hadi kushindwa kulipa gharama za miradi ya maendeleo. Mfano wa mzigo tulio nao kwasasa ni pamoja na miradi mingi mikubwa kusimama kwa kukosa fedha za uendeshaji kitu ambacho kinaendelea kuliingiza taifa kwenye madeni yenye riba kubwa (mfano ni miradi ya barabara na majengo ya taasisi za serikali) kwasasa miradi hii imekuwa mwiba mkubwa kwani makandarasi wengi wakiweo wa ndani na wa nje kutolipwa pesa kwa wakati. Vile vile miradi kama utengeneza wa meli kwenye bahari na maziwa yetu, ujenzi wa vituo vya afya na vyumba vya madarasa, miradi mikubwa ya maji n.k n.k.

Pia, timu hii itafanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi bora ya ardhi na mipango miji, ili kupata mfumo unaoendana na mahitaji ya sasa na mustakabali wa taifa letu. Hii itajumuisha kuzingatia mipango ya muda mrefu na utekelezaji wa sera ambazo zitahakikisha matumizi bora ya rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Hivi sasa, miji mingi haijapangwa kwa ubora, na kusababisha changamoto kubwa kwa wakazi wake, ikiwa ni pamoja na msongamano wa huduma za kijamii, majengo yaliyopangwa kiholela, na miundombinu isiyokidhi viwango vya ubora. Ukuwaji wa miji kwasasa katika nchi yetu ya Tanzania ni mkubwa lakini idara ya Ardhi kupitia idara ndogo ya mipango miji (Town Planner) haijakuwa na nguvu kwani bado miji mingi iliyopo na inayokuwa hakuna kinachofanyika kuhakikisha inapangwa kwa ubora na kwa kuzingatia utalaamu. Mkasanyiko wa huduma unachafua miji yetu angali tunao sasa watalaamu wengi ni ishara kwamba bado hatujapiga hatua kubwa kwenye maendeleo ukilinganisha na zama tuliopo.

Yaliyotajwa hapo juu, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa ni baadhi tu ya maeneo ambayo yatashughulikiwa na timu hii. Lengo ni kuhuisha taifa letu liwe taifa la watu imara, wenye uwezo wa kujitegemea, na si wanyonge.

Mheshimiwa Rais, naomba kusema kuwa mimi kama mwananchi wako, pamoja na wengine watakoguswa na barua hii; nina dhamira safi ya kuona taifa letu likipiga hatua kubwa za maendeleo kwa haraka na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika. Tunatambua umuhimu wa kuwa na uongozi makini, mipango thabiti, na ufuatiliaji wa karibu katika utekelezaji wa mipango hii. Hivyo basi, nipo tayari kutoa mchango wangu kwa namna yoyote itakayoonekana inafaa katika kufanikisha azma hii.

Ningependa kuomba nafasi ya kujadili wazo hili kwa kina na Wizara husika au mamlaka nyinginezo zinazohusika, ili tuweze kuanza mchakato huu mapema iwezekanavyo.

Namaliza barua yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, huruma na fadhili nyingi kwetu Watanzania na wewe Mheshimiwa Rais, kwa muda wako na utayari wako wa kusikiliza mawazo ya wananchi wako. Tuna imani kubwa kwamba chini ya uongozi wako, Tanzania itapiga hatua kubwa za maendeleo.

Wako mtiifu,
Mwananchi Mzalendo.

Pia, soma: Barua ya Wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…