A Disciple
New Member
- Apr 14, 2012
- 2
- 0
January 04, 2018
BARUA YA WAZI KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MHE(DR.) JOHN POMBE MAGUFULI
Mhe.Rais, kwa heshima na taadhima naomba nianze kwa kukutakia HERI YA MWAKA MPYA 2018 WEWE PAMOJA NA FAMILIA YAKO!. Ninafurahi kupata nafasi hii kuweza kukuandikia ujumbe huu baada ya kutafakari kuwa nini ambacho naweza toa kwa ajili ya nchi yangu Tanzania, hasa wakati huu tunapouanza mwaka huu mpya wa 2018.
Mhe Rais, kwa sababu wewe ndiye umebeba dhamana ya nchi hii wakati huu, nimeamua nikuandikie ujumbe wa kukutia moyo kwa niaba ya Watanzania wote.Naomba pia nikupongeze kwa juhudi zako na dhamira yako ya dhati kabisa ya kuamua kuielekeza nchi hii katika maisha ambayo ni stahiki yake.Nafahamu pia pamoja na mafanikio hapakosi changamoto.
Mhe Rais, napenda ufahamu kuwa kwa sababu ya juhudi zako, tumeanza kutembea kifua mbele kwa sababu ya heshima ambayo nchi yetu imejitwalia chini ya uongozi wako. Aidha napenda pia kukutahadharisha kuwa jitihada zako za hali na mali zimeanza kutiwa doa na mambo ambayo yanaepukika kabisa, hivyo naomba tunapoanza mwaka mpya huu penye kurekebisha parekebishwe.
Mhe.Rais, ninaishukru Serkali, Wazazi wangu na Watumishi wa Mungu kwa kunipa Elimu mchanyato ambayo imenifanya kujitambua vyema na kutambua nafasi yangu katika jamii. Kupitia neema ya Mungu inayofanya kazi ndani yangu na ufahamu nilioupata naweza tambua au kadiria kile kinachoendelea katika mazingira yangu hata wakati ambapo takwimu nilizonazo ni pungufu.
Mhe Rais, wananchi tulio wengi ukiwemo wewe mwenyewe binafsi, tulichukizwa sana na tukio la kushambuliwa kwa Mhe.Tundu Antipas Lissu, binafsi bado moyo wangu haujatulizwa. Pamoja hayo nimechagua kuendelea kuiamini Serkali yangu kuhusu uchunguzi ambao ilisema unaendelea ili kubaini waliohusika na tukio hilo, lakini cha ajabu mpaka leo hii bado uchunguzi huo unaendelea.
Mhe.Rais, iwapo Serkali inadhamira ya kweli, na bado ninaamini ina dhamira ya kweli naomba ikubali kutafuta njia mbadala ya kusaidiwa maana muda umekuwa mrefu bila mafanikio. Njia mbadala yaweza kuwa ambayo wapinzani wamekuwa wakipendekeza, ya kupata watu ambao wana teknolojia ya juu zaidi watusaidie uchunguzi huu ili kuokoa muda na kujenga ufa huu mapema iwezekavyo.
Mhe.Rais, kuna moja ya makala zangu kupitia ukrasa wangu huu binafsi niliongelea sana namna ya kutoa maoni au ushauri kwa viongozi. Nilishauri kuwa wananchi wanao uhuru wa kutoa maoni yao au kushauri lakini siyo kumlazimisha kiongozi afuate matakwa yao ambayo hayamo kwenye utaratibu, hata kama ni mazuri. Wajibu wa wananchi ni kutoa maoni yao kisha kumwachia kiongozi aweze kuamua na huo ndio maana ya uongozi ninaofahamu mimi.
Mhe.Rais, nilionya pia kuwa jambo lolote likipigiwa kelele na likawa na ukweli ndani yake lakini kiongozi akaamua kupuuza ajue kuwa yupo Mungu ambaye kwake hapuuzi mtu au kitu chochote. “Yeye huwaangazi jua na huwanyeshea mvua wema na waovu”.”Yeye ndiye anayeinua na Yeye ndiye anayeshusha”.Yeye ndiye anayetajirisha na Yeye ndiye anayefukarisha”.
Mhe.Rais, hivyo niliwasihi sana wasomaji wangu kuwa wavute subira, kwa kuwa viongozi wetu ni watu wanaomcha Mungu hawawezi kushupaza shingo pale wanapohitaji kujisahihisha mbele za Mungu aliyewapa mamlaka hayo. Nilikazia hilo kwa vile binafsi naamini hakuna mamlaka ambayo yaweza simama kama Mungu hakuipa kibali.Kujaribu kumkwamisha kiongozi ni kushindana na Mungu pamoja na kujikwamisha mwenyewe.Hali kadhalika kiongozi wa kweli kuthibitishwa au kupitishwa na watu hivyo kudhihirisha uteuzi wa Mungu na kwa maana hiyo baada ya kiongozi kujisahihisha kama akijikwaa watu waliomdhibitisha hufurahi kuona kubadilika kwake kupitia vitendo vyake vinavyodhihirisha badiliko hilo.Kwa hiyo cha msingi kama kiongozi kama umejiridhisha kuwa unahitaji kubadili vitendo au mtazamo wako fulani kulingana na maoni ya watu unaowaongoza cha msingi ni vitendo vyako kuthibitisha badiliko hilo.
Mhe.Rais, ninaamini wewe kama mwanadamu pia waweza kosea lakini huhitaji kushurutishwa na mtu kwenda kutubu, hasa katika kipindi hiki tunachokiita cha Neema. Naomba uwe huru kabisa na nikuhakikishie kuwa Mungu anakupenda jinsi ulivyo, ukijisikia kwenda mbele zake kwa kumweleza magumu yako una hiari ya kufanya hivyo muda wowote na yuko tayari kukusikiliza kila wakati maana ajua huwezi bila Yeye. Cha msingi tii sauti yake anapozungumza na wewe kupitia Roho Mtakatifu, akikudhibitishia ukweli fulani, hapo hakuna namna unahitaji kutekeleza.
Mhe.Rais, kazi ya Watumishi wa Mungu ni kukuombea ili unaposikia sauti ya Mungu usiufanye moyo wako kuwa mgumu.Watumishi wa Mungu haipo sababu ya kukuamrisha kufanya jambo lolote.Baadhi ya Watumishi wa Mungu wa kweli walinifundisha na nimeshuhudia mwenyewe katka maisha yangu ukweli huu; kuwa haipo haja ya kulazimisha jambo lolote kama unamfahamu vyema Mungu wako maana kabla hujamwambia mhusika mwambie Mungu yeye ndiye atafanya hata kabla hujatamka lolote.
Mhe.Rais, ninaupenda mstari watumishi wa Mungu wa kweli waliwahi kunifundisha kuwa,” Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki”.Nifafanue neno moja tu katika mstari huu, “hakuogofya” maana yake Yesu alikuwa na uwezo mkubwa sana ambao waliomtesa hawakujua, lakini pia yeye hakutaka wajue hali yake halisi, laiti wangelijua kuwa alikuwa ni Mungu wasingelidiliki hata kumgusa. Sasa ndiyo najiuliza kama mtumishi wa Mungu unaanzaje kutoa vitisho kuwa una uwezo kupita hata serkali?Watumishi wa namna hii huishia kutia doa hata ujumbe wanaokuwa wamemeba, watumishi wengine tunabaki njia panda kuwa ni Mungu kweli aliyewatuma au ni nani?.
Mhe.Rais, naomba nimalizie kwa kusema ni kweli kabisa watu wanaotumia lugha chafu dhidi yako na Serkali kwa ujumla wanahitaji kushughulikiwa kikamilifu lakini kwa sababu wanakupotezea na kutupotezea muda pia, naomba waachwe watumie midomo yao wanavyopenda. Serkali yako ijikite katika kuchapa kazi huku ikifanyia kazi baadhi ya mambo wanayopendekeza ambayo ni mazuri lakini hayamo kwenye utaratibu ambao serkali imejipangia.
Mhe. Rais, ninasema waachwe kwa sababu kuhakikisha midomo takribani 50mil inafikiri kabla ya kusema au kuandika ni shughuli moja kubwa sana. Shughuli hii ndiyo Watumishi wa Mungu na Wazazi wanaweza kukusaidia kwa kiasi, maana tatizo si midomo tatizo ni nini mtu amejaza moyoni.”Mtungi wa gesi uliojaa pomoni huwezi kuufunga muda wote bila sehemu ya kupumulia, vinginevyo utakuja kuripuka pasipo wewe kujua na hayo yatakuwa maafa makubwa”. Kazi hii ya kumfanya mtu afikiri kabla ya kusema au kuandika inahitaji tohara ya mioyo na ni Mungu kwa kushirikiana na watumishi wake pekee yaweza kufanikiwa. Pamoja na tohara ya mioyo hilo ni zoezi la kila siku la mtu kujikana mwenyewe. Mimi binafsi pamoja na kuwa nimepata hiyo tohara lakini bado ninalo jukumu la kuchagua kila siku kufuata utu wangu kabla ya tohara au kufuata utu wangu baada ya tohara.”Ni jambo lisilowezekana kushughulika kutibu ugonjwa wa ndani kwa njia ambazo ni za nje”.
Mhe.Rais, naomba usiwape nafasi ya kujenga umaarufu wapinzani wako, kwa mambo madogo kama haya. Umeanza vizuri sana binafsi ninaomba umalize vizuri.Kuna kipindi wakati unaanza uliwapa wakati mgumu sana wapinzani, yaani walikuwa wanapekua kurasa kuona wapinge wapi wanaishia kutoka na mambo ambayo hata wananchi walikuwa wanawashangaa.Sasa hivi umewapa kipaza sauti kwa mambo madogo, kwa hiyo nakushauri uwanyang`anye hicho kipaza sauti. Ni rahisi sana jipeleleze wapi umejikwaa kisha mwambie Mungu akusamehe, ninaamini Mungu ni mwingi wa rehema atakusamehe na atakutia nguvu mpya.
Mhe Rais, mwisho kabisa, ingawa siyo mwisho kwa umhimu, naomba nikuombe ulifikirie vyema swala la mchakato wa Katiba itapendeza sana kama utaweza kulitekeleza.Maana ni mhimu sana na litaondoa wasiwasi tulio nao kuwa nchi yaweza kurudi kwenye hali yake ya nyuma pindi tu utakapoondoka madarakani.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRICA!
Wako,
Muono wa mbali!
I`M NOT A SLAVE TO FEAR, I`M A SON OF GOD!
MIMI SI MTUMWA KUOGOPA, MIMI NI MWANA WA MUNGU!
Nakala:
Viongozi wa dini wote-Tanzania